Minada wa vitalu vya uwindaji waingiza Sh19.2 bilioni

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja akizungumza na vyombo vya Habari kuhusu ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada katika kikao kilichofanyika leo ukumbi wa Chuo Cha Taifa Cha Utalii jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii,Dk. Francis Michael na kulia ni Dk. David Manyanza Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri kuhusu ugawaji a Vitalu vya Uwindaji.
Muktasari:
- Ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada waiingizia faida Serikali ya Sh19.2 bilioni kutoka Sh5 bilioni.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema ugawaji vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada ulioanza mwaka 2019, umesaidia kuingiza Serikali kiasi cha Sh19.2 bilioni kutoka Sh5.24 bilioni zilizokuwa zikipatikana kabla ya kuwepo kwa mfumo huo.
Masanja ameyasema hayo jana Januari 23 jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada wa sita uliofanyika Januari 12 hadi 18, 2022.
Masanja amesema tangu mwaka 2019 mfumo huo ulipoanza rasmi hadi sasa jumla ya minada sita ya vitalu vya uwindaji wa kitalii imefanyika kwa njia ya mtandao na imeingiza kiasi hicho cha Bilioni 19.2.
“Katika mnada wa sita ambao ulifanyika Januari 12 hadi 18 mwaka huu ulihusisha jumla ya vitalu 75 vya uwindaji wa kitalii, vitalu 49 umiliki wake unamalizika Desemba 31, 2022.
“Vitalu 26 ni vile ambavyo vilikuwa wazi, jumla ya kampuni 39 zilishiriki mnada huo na kati ya hizo 26 sawa na asilimia 54.2 zilishinda vitalu vya uwindaji wa kitalii 45.
Amesema mnada huu wa sita jumla ya kiasi cha Sh14.32 bilioni zilikusanywa, ambapo Sh392.7 milioni zilitokana na ada ya maombi ya ushiriki na Sh 13.86 bilioni zilitokana na ada ya vitalu.
Hata hivyo, amesema Serikali iliamua kugawa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada kwa lengo la kuongeza uwazi na kuruhusu nguvu ya soko kuonesha thamani halisi ya rasilimali muhimu ya nchi ya vitalu hivyo.
“Kwa mfano kitalu kimoja daraja la tatu ambacho kilikuwa kiuzwe kwa njia ya zabuni wa Sh. 41.58 milioni kimeuzwa kwa Sh. 462 Milioni ambayo ni mara 11 ya bei ya zabuni. Daraja ya pili kilikuwa kiuzwe Sh. 69.3 Milioni kwa njia ya zabuni ila kimeuzwa zaidi ya Sh. 577Milioni,” amesema Masanja.