Miongozo 15 imetolewa kupambana na corona nchini

Miongozo 15 imetolewa kupambana na corona nchini

Muktasari:

  • Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima amesema tangu kuanza kwa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, wizara hiyo imetoa miongozo 15.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima amesema tangu kuanza kwa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, wizara hiyo imetoa miongozo 15.


Akizungumza bungeni leo Jumanne Mei 11, 2021 wakati akiwasilisha bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2021/22 ya wizara hiyo, Dk Dorothy amesema miongozo hiyo ililenga namna bora ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.


“Tumetoa miongozo 15 ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni, kutumia vipukusi (sanitizer) mara kwa mara, kufanya mazoezi pamoja na lishe bora ikiwemo matunda na mbogamboga.”


“Vilevile, Serikali imekuwa ikijielekeza kuwalinda wote walio katika makundi ya hatari zaidi dhidi ya ugonjwa huu kama vile wazee na wenye magonjwa ya muda mrefu,” amesema.


Dk Gwajima amesema afua nyingine zilizoendelea kutekelezwa na Serikali ni pamoja na kuhamasisha jamii kuimarisha matumizi ya tiba asili, kujifukiza, uvaaji wa barakoa za kushona na zile za viwandani hasa zinazotengenezwa ndani ya nchi na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya.


Amesema katika hatua za kuimarisha udhibiti wa ugonjwa huo jumla ya wasafiri 6,446,710 walifanyiwa  uchunguzi katika maeneo yote ya mipakani.


“Wizara katika jitihada za kuimarisha udhibiti wa magonjwa yenye hatari ya kusambaa kimataifa imeanzisha mfumo wa kidigitali wa ufuatiliaji wa afya za wasafiri. Mfumo umeanza mwezi Aprili, 2021 na unapatikana katika wavuti afyamsafiri.moh.go.tz,” amesema.