Miradi ya TnK, UCHUMI imewakwamua wanawake, vijana katika lindi la umaskini

Wednesday July 13 2022
MRADI PIC1

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Tixon Nzunda (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CARE International Tanzania, Prudence Masako (wa pili kulia), Meneja Mradi wa shirika la CARE International Tanzania, Hakika Mtui (wa kwanza kulia) wakisikiliza maelezo kutoka kwa vijana wajasiriamali wakati wa maonyesho yaliyofanyika katika hafla ya mkutano wa wadau wa mradi wa UCHUMI.

By Maliki Muunguja

Vijana na wanawake waishio vijijini wanazaiishi ndoto zao usingizini kutokana na kukabiliwa na umaskini uliokithiri, vijana wakikosa ajira na wanawake wakimaliza miongo ya kubaki nyuma kimaendeleo majumbani mwao.

Ni changamoto iliyobisha hodi mlangoni kwa Shirika la CARE International Tanzania na kubuni suluhisho la miradi miwili inayoendana ya TnK na UCHUMI.

Mradi wa TnK (kwa kirefu: “Tajirika Na Kilimo”) ni mkakati wa miaka minne (2018-22) wa ukwamuaji maisha ya wakulima wadogo na wafugaji kupitia kuwajengea ujuzi wa mbinu bora za kilimo na ufugaji kibiashara ili wazalishe kwa ubora, wingi na tija.

Na ule wa UCHUMI (yaani “Ujana ni Uchumi Imara”) umejikita katika kuwawezesha vijana, hasa wanawake kuinua uchumi wao kupitia mafunzo ya ufundi stadi katika fani za ufundi umeme wa majumbani, mapishi na uokaji, uzalishaji wa mboga mboga na matunda, ufugaji kuku na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

MRADI PIC

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CARE International Tanzania, Prudence Masako akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa mradi wa UCHUMI

Licha ya miradi hii kutekelezwa kwa pamoja, makala haya yanautazama zaidi Mradi wa TnK ambao umebeba dhima na matarajio makubwa zaidi kwa jamii hizo na watekelezaji wake. Kwa kuthamini nguvu ya taasisi zingine katika kuinua sekta ya kilimo, CARE International Tanzania ilishirikiana na VETA na SAGCOT kuendesha mradi wa Tajirika na Kilimo kwa utimilifu na ufanisi wa hali ya juu.

Advertisement

Pia wasimamizi wa mradi walifanya kazi kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa katika kurahisisha ufikiwaji wa walengwa wa mradi.

Mafunzo yaliyokuwa yanatolewa katika mradi huu yalijikita katika maeneo makuu matatu; kilimo cha mbogambo-ga matunda, kilimo cha mazao mchanganyiko na ufugaji.

CARE International Tanzania haikutaka kuwa na vikundi vya wakulima na wafugaji tu waliowezeshwa mbinu za kilimo na ufugaji wa kisasa pekee, lakini ilitaka kuona sehemu ya jamii hizo pia zinatumia vyema mapato yatokanayo na shughuli zao na hivyo iliongeza ujuzi wa uwekaji akiba na kukopa kwa baadhi ya wanufaika wa mradi huo (hususan vijana na wanawake).

Mradi wa TnK umetekelezwa katika mikoa mitatu ya Iringa, Njombe na Morogoro licha ya mkoa wa Njombe kutokuwa sehemu ya makala haya.

Ufugaji

Katika eneo la ufugaji, kumeshuhudiwa hatua za maendeleo zilizopigwa na kikundi cha wafugaji kuku cha Agape kilichopo katika kata ya Ifunda, wilaya ya Iringa Vijijini, mkoani Iringa.

Margareth Sikahanga (65), mzaliwa wa mkoa wa Njombe aliyekulia Iringa mjini, anakiwakilisha vyema kikundi cha Agape katika ufugaji kuku.

Elimu yake ni mhitimu wa darasa la saba. Yeye ni mjane, mama wa watoto watatu, bibi wa wajukuu 11 (wa kike wakiwa tisa na wa kiume wawili) na mwanachama wa kikundi hicho, ni shuhuda wa namna maisha yake yalivyochukua taswira mpya ndani ya miaka miwili ya utekelezaji wa TnK.

“Mimi nimekulia katika familia ya wakulima. Hata baba yangu wakati anafariki aliniachia wosia wa kutoacha kufuga kwani itanisaidia kupata chakula na fedha kwa ajili ya kuendesha maisha. Hivyo mradi ulivyokuja ilikuwa rahisi kushiriki kwa kuwa pia nilikuwa na nia.Kabla ya mradi, nilikuwa nafuga kuku kwa mazoea, walikuwa wanakufa hovyo na nilikuwa sifahamu shida ni nini.

MRADI PIC3

Kikundi cha Kuweka Akiba na Kukopa cha Mradi wa TnK cha Jitegemee kilichopo katika kata ya Doma, Wilaya ya Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro. Kikundi hiki kilipata mafunzo ya mradi wa TnK

Walivyokuja watu wa CARE International Tanzania, walitupatia kuku 100 lakini kwa kuwa hatukuwa na uwezo kama kikundi kuwalisha kwa pamoja tuligawana kila wanachama.Katika awamu ya kwanza nilipata kuku 14 ambao niliwafuga mpaka wakakomaa ambapo niliwauza na kupata jumla ya shilingi 140, 000.

Katika awamu nyingine niliongeza kuku wengine 100, nikauza na kupata shilingi milioni moja,” anaeleza Margareth.

Anasema katika awamu ya pili, alitoa gharama kwa ajili ya chakula na ununuzi wa kuku wengine takriban Sh700, 000 katika ile shilingi milioni 1 na iliyobaki akaingiza katika matumizi mengine ya nyumbani.

Katika awamu hii alinunua kuku 200 ambao anao mpaka sasa, akitegemea kuwauza na kupata fedha nyingi zaidi ya zile alizopata katika uzao wa kwanza na wa pili.

“Tulifikiwa na watu wa Halmashauri ambao walitueleza kuwa hatukuwa tukifuga bali ‘tulikuwa tunalala na kuku’ kwa sababu ya udogo wa mabanda yaliyokuwa yanatumika kufugia hivyo tulipewa mkopo wenye thamani ya shilingi milioni kumi kwa baadhi yetu na tuliweza kugawana miongoni mwetu na binafsi nimeweza kujenga banda kubwa,” anaeleza Margareth ambaye sasa anasubiri maofisa wa mamlaka husika kuja kukagua ujenzi huo kabla ya kuwaruhusu kuanza kuyatumia kwa ufugaji wa kisasa.

Licha ya ufugaji wa kuku wa kisasa, Margareth pia alifikiria mbali zaidi kwa kuamua kufuga pia kuku wa kienyeji (akiwatenga dhidi ya wale wa kisasa) na kufanikiwa kupata kuku 70 ambao aliwauza na kupata Sh700,000, fedha iliyosaidia kukuza mtaji wake wa kuku.

Pia kupitia mafunzo ya mradi huu wa TnK kwa Mama Sikahanga pia anafuga nguruwe ambapo anatarajia baada ya miezi kadhaa ataanza kuuza.

Sambamba na hilo, anauza pia viroba vya mbolea ambapo fedha inayopatikana inaendelea kusaidia biashara yake mama ya kuku.

Margareth si mbinafsi, anakiri kuwa mafunzo aliyopata ameweza kuyagawa kwa baadhi ya watu ambao hawakuwa sehemu ya mradi.

“Kuna kijana mmoja ambaye alivutiwa na mradi wangu na nilimwelekeza akaja kwangu nikamuuzia kuku watano, nimekuwa nikifuatilia na kumrekebisha pale anapokesea.”Kilio chake ni kwa Halmashauri kuwapatia mikopo inayoweza kutosheleza mahitaji ya kila mwanachama.

“Pia, tunahitaji masoko ya uhakika ya kuku, maana kwa sasa tunauza kidogo kidogo na wakati kiwango cha uzalishaji kinapanda” anaeleza Margareth.

Kilimo cha mazao mchanganyiko

Ukitaka kuona namna somo la kilimo cha viazi, maharagwe na njegere lilivyofanya kazi, tembelea katika kijiji cha Ilogombe, kata ya Kibengu, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa. Branika Mpinge (25), ameza-liwa na kukulia Mufindi.

Ni mke na mama wa mtoto mmoja. Ana elimu ya kidato cha nne. Baada ya kumaliza shule, alijiunga rasmi katika shughuli za kilimo cha njegere, maharagwe na viazi mviringo. Anasimama kama shuhuda mkuu wa namna mradi wa TnK ulivyobadili maisha yake kupitia shamba darasa la kilimo cha mazao mchanganyiko.

“Kabla ya mradi huu wa TNK kuja, nilikuwa ninalima njegere kwa mazoea tu; yaani nilikuwa nikilima ekari moja, ninaweza kuvuna magunia hata 30, kikiwa ni kiwango kidogo kulingana na mbegu zilizokuwa zikitumika shambani. Baada ya mafunzo, sasa ekari moja inaniwezesha kuvuna hadi magunia 60 kwa kupanda kitaalamu na kutumia mbinu bora za kilimo,” anasema Branika.

Branika anasema moja ya mafanikio makubwa aliyoyapata kutokana na kulima njegere kibiashara ni kujenga nyumba yake, kununua shamba lingine la ukubwa wa ekari moja na cherehani.

Pia yeye na mumewe wanafikiria kufungua saluni ya kiume na anajivunia kuwa na mume anayemsaidia katika shughuli zake ikiwemo kumpa mawazo na upangaji wa mipango ya uendeshaji wa shughuli zote za kilimo.

Kwa upande mwingine, yeye na mumewe walifanikiwa kujiunga na vikundi vya kuweka na na kukopa (VSLA) vya Muungano na Upendo ambavyo vinawawezesha kuwa na nidhamu ya fedha kupitia kuweka akiba.

“Zamani kabla sijajiunga, nilikuwa nikipata fedha naitumia kununua nguo bila mpangilio lakini sasa hivi natambua thamani ya fedha kwa kuweka na kukopa kupitia vikundi hivi.

“Ninaomba tuongezewe ujuzi katika kilimo cha viazi, kwani vimekuwa havitupi kipato tunachokitarajia kutokana na kushambuliwa na wadudu pori ikilinganishwa na njegere na maharagwe,” anatoa rai.

Branika anakiri kuwa ushiriki wake katika mafunzo ya mradi huo yamechangia kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ambavyo kundi kubwa la wanawake hukumbana navyo wakiwa majumbani.

“Wakati wa mafunzo, mume wangu aliniruhusu kuhudhuria madarasa hayo na kuwa mstari wa mbele kunifuatilia.”Janga la Uviko-19 halikumwacha Branika salama kwani shughuli za kilimo katika kipindi cha usambaaji wa ugonjwa huo zilisimama na kwa kiasi kikubwa kusababisha hata upatikanaji wa mazao duni kutokana na kutegemea vibarua ambao nao waliamua kukaa pembeni kwa hofu ya kuambukizana ugonjwa huo.

“Njia tuliyoitumia ilikuwa ni kukodisha trekta na watu wachache waliokuwa tayari kuvuna kwa niaba yangu kwa kuwa kilimo chetu asilimia kubwa kulikuwa ni cha jembe la mkono.”

Branika anaona kuwa soko la uhakika bado imekuwa changamoto kwake licha ya kuendelea kuzalisha njegere kwa ubora unaohitajika.

Kilimo cha mbogamboga

Kikundi cha wakulima wadogo wa nyanya cha Jitegemee kilichopo katika kata ya Doma iliyoko wilaya ya Morogoro Vijijini kimeubeba mkoa wa Morogoro kupitia Kilimo hiki na wanakikundi wake wengi wamejikwamua kimaisha.Hussein Omari (31) ni mzaliwa wa mkoa wa Morogoro. Ni mume na baba wa watoto watatu. Shughuli zake ni za kilimo.

Ni moja ya wanakikundi cha Tupendane ambaye amekuwa mfano wa kuigwa.Omari ambaye amekulia katika familia maskini alijikita katika kilimo kama sehemu ya kujikomboa kimaisha.

Kabla ya mradi alikuwa akilima nyanya kwa njia zisizo za kitaalamu ambapo alijikuta akilima eneo kubwa katika shamba na kupata mavuno kiduchu.

“Mwanzoni nilikuwa nalima ekari tatu na kupata kreti 200 ambazo niliuza kila kreti kwa shilingi 7000 mpaka 15,000 kutegemeana na msimu na kupata kuanzia Sh1.4 mpaka 3 milioni. Baada ya mafunzo nilipunguza eneo la ulimaji kutoka ekari tatu hadi moja na kufanikiwa kuvuna kreti 350 kwa msimu mzima na kupata shilingi 4.5 milioni.

Sehemu ya fedha hiyo nilitumia kwa matumizi ya nyumbani ikiwamo kununua nguo, chakula, kiwanja na nyingine kuweka akiba.”Omari pia yupo katika kikundi cha kuweka akiba na kukopa ambapo alijiunga tangu mwaka 2008 kabla ya mafunzo ya TnK kuja.

Kabla ya kujiunga na kikundi hicho alikuwa hana nidhamu ya fedha lakini baada ya kujiunga ameona faida yake kubwa ikiwemo kuchukua mkopo kwa ajili ya pembejeo na madawa ya kilimo.

Rai yake kubwa ni kuongezewa ujuzi katika eneo la uongezaji thamani zao la nyanya kupitia elimu ya usindikaji na ujenzi wa viwanda vya kusin-dika mazao ya kilimo.

Vikundi vya kuweka akiba na kukopa vya vijana (YSLA)

Kikundi cha kuweka na kukopa cha Vijana cha Tupendane kilichopo Morogoro Mjini kinaongoza njia katika kutambua umuhimu wa kuweka akiba na kukopa kwa vijana chini ya ulezi wa TnK.

Fairuna Magati (28) ni mwenyekiti wa kikundi hicho ambaye anafafanua kuwa mradi huo waliupokea kwa furaha na umebadilisha maisha yao kwa kiasi kikubwa.

“Kabla ya mradi nilikuwa sijui faida ya kuweka akiba ya fedha zangu, nilikuwa nikipata Sh7,000 naenda zangu kununua nguo na mahitaji mengine lakini hivi sasa hata nikipata shilingi 1,000 ninaweka katika kikundi najua nitapata zaidi baadaye” Anasema Fairuna.

Wasimamizi wa mradi wasimulia

Mkufunzi na mwezeshaji wa mradi wa TnK, Makarani Abdulaziz, ambaye ni miongoni mwa wawezeshaji wa awali wa mradi wa kilimo na ufugaji anasema uzoefu alioupata ni mkubwa kwani aliona mwitikio mkubwa wa wanawake katika mkoa wa Iringa na wanaume wakiwapiku wanawake kwa mkoa wa Morogoro.

“Kutokana na ukweli kwamba mkoa wa Morogoro ulikuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika tulijitahidi kuhakikisha tunawapa mafunzo kwa kadri kwa kuzibgatia hali zao na kuchukuliana nao ili wanufaike kama wengine.”

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini, Florence Mwambene anabainisha kuwa Halmashauri ilikuwa na kazi ya kukusanya vijana wenye vigezo ambao walikwenda kufundishwa mbinu mbalimbali za uelimishaji jamii (yaani Community Based Training) ambapo baada ya mafunzo walishirikiana na maofisa maendeleo ya jamii na maofisa wa mradi kuhakikisha vikundi vinaibuliwa na vinafunzwa mbinu mbalimbali za kilimo na biashara.

“Baada ya kuibuliwa, vikundi hivyo vimeendelea kulelewa na Halmashauri kwa kuvipa vyeti vya utambuzi kuanzia ngazi ya vijiji na kata,” anaeleza Ofisa Maendeleo huyo. Anasema kuwa kwa sasa Halmashauri ina vikundi takriban 90 vya mradi vilivyopatiwa mafunzo.

Kati ya vikundi 90, 20 viliomba kuongezewa ujuzi wa ufugaji kuku na ng’ombe, nguruwe, mapishi, mapambo na ufundi umeme.

Kwa upande wa Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Bi Natujwa Melau anasema kuwa malengo ya mradi katika wilaya ya Mvomero yamefanikiwa kwa kuwa vikundi vilivyoundwa vilichagua shughuli za kufanya vyenyewe bila shuruti na vimeweza kuona matunda makubwa ya mradi.

“Zaidi ya asilimia 65 ya miradi iliyochaguliwa na vikundi mbalimbali ilikuwa ni ile ya mifugo na hayo ni mafanikio katika eneo langu la mifugo.

”Meneja wa Kongani la Kilombero wa SAGCOT, John Banga anasema kama taasisi inayoangalia ukuaji wa kilimo, ilikuwa rahisi kuridhia kushirikiana na CARE International Tanzania katika mradi wa Tajirika na Kilimo kwa kuwa wanazungumza lugha moja ya kuendeleza sekta ya kilimo.

Anasema kuwa, SAGCOT ilibeba jukumu la kuhakikisha mradi unakwenda sambamba na wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo wa kilimo wakifanya kazi kwa malengo ya kuona namna gani wakulima wanakuwa wanufaika wakubwa katika ngazi zote.

Serikali, CARE wanena

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tixon Nzunda ameviagiza vyuo vya ufundi stadi, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini kuanza kutekeleza mara moja mitaala ya kilimo, biashara na uchumi, ambayo tayari imekamilika lengo likiwa ni kuongeza ujasiriamali, kipato na kuimarisha uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Katibu mkuu huyo alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa masuala ya kilimo na uchumi katika tukio la tathmini na ufungaji wa miradi ya ‘Tajirika Na Kilimo Na UCHUMI’ mnamo tarehe 22/04/2022.

Aidha alisema kuwa miradi hiyo ya Tajirika na Kilimo (TnK) na Ujana ni Uchumi imara (UCHUMI) ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa ubia kati ya CARE International Tanzania, VETA na SAGCOT center Ltd, imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi hususani wale walioko katika vikundi vya kuweka na kukopa ambavyo vimewezeshwa ambapo kundi kubwa la wanufaika hao ni wan-awake na vijana.

Meneja msimamizi wa miradi hiyo toka CARE International Tanzania, Samuel Chambi alisema kuwa miradi hiyo ya TnK na UCHUMI imekuwa ikihamasisha kwanza watu kukaa katika vikundi kisha kuingia katika mafunzo na kujengewa uwezo kuhusu kilimo biashara na uzalishaji wenye tija walengwa wakiwa wanawake na vijana.

Aidha Chambi alibainisha kuwa miradi hiyo ya Tajirika na Kilimo na UCHUMI imekuwa fursa kwani imewapatia wanawake na vijana zaidi ya 2,200 mafunzo ya ujuzi na vijana zaidi ya 15,000 mafunzo ya ujasiriamali, stadi za maisha, jinsia na usawa ambapo imebainika kwamba fursa hizi zimetumika vyema kuchangia kupunguza tatizo la umaskini kwa vijana kwakuwa walengwa wamewezeshwa kuanzisha kilimo biashara na wengine ufugaji ili kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa CARE International Tanzania, Bi Prudence Masako amesema kuwa shirika linalenga kuwafikia watu mil-ioni 200 duniani lengo likiwa ni kupunguza umaskini na kuleta haki kufikia mwaka 2030.

Hata hivyo alisema, CARE International Tanzania imekuwa ikiangalia ni namna gani jamii inaweza kutumia rasilimali zilizopo ili kujikwamua kiuchumi hususani kwa wanawake ambao wengi wao wamekuwa wakishindwa kujitetea na kukosa haki zao za msingi ili kuweza kutumia rasilimali zinazowazunguka kujikwamua kiuchumi.

Advertisement