Mjadala Chato kuwa mkoa washika kasi

Muktasari:

  • Waziri wa zamani, Profesa Anna Tibaijuka amesema wazo la Chato kuwa mkoa halitekelezeki, kwani hakuna vigezo vinavyoifanya wilaya hiyo kuwa mkoa.

Dar es Salaam. Waziri wa zamani, Profesa Anna Tibaijuka amesema wazo la Chato kuwa mkoa halitekelezeki, kwani hakuna vigezo vinavyoifanya wilaya hiyo kuwa mkoa.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza aliyesema Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Geita (RCC) kuridhia uudwaji wa mkoa huo na Baraza la Madiwani la Geita kupinga inaonyesha mgongano wa wazi.

“RCC ni jopo la wateule. Mkoa na wilaya mpya ni fursa ya uteuzi. Kwa madiwani uundwaji wa mkoa mpya ni kero na mzigo kwa wananchi na wapiga kura wao, ndio maana wamepinga.

Lakini mkoa mpya unaopendekezwa ni kama mimba iliyotungwa nje ya kizazi, tusipokuwa wakweli tutahatarisha maisha ya mama (Kagera, Geita, Kigoma na Mwanza),” alisema Askofu Bagonza.

Awali akinukuu habari iliyochapishwa na mtandao wa gazeti hili kuhusu mapendekezo ya mkoa wa Chato kuwa na Wilaya tano, Profesa Tibaijuka alisema katika mazishi ya Rais wa tano, John Magufuli, wazee wa Chato walimuomba Rais Samia Suluhu Hassan mkoa wakidai ni ahadi ya mtangulizi wake. “Rais kwa hekima akasema ataangalia vigezo.

Kama mbunge mstaafu jirani Muleba Kusini najua vigezo havipo. Wazo halitekelezeki. Wazee jirani na sisi naamini tutapewa nafasi kushauri,” aliandika Profesa Tibaijuka kupitia mtandao wa Twitter.

Kutokana na andiko hilo, kundi mojawapo la mtandao wa kijamii wa WhatsApp lilimuomba Profesa kufafanua kauli yake na kusema ramani inaonyesha Chato ni sehemu ya Wilaya ya Biharamulo Mkoa wa Kagera kiuhalisia na kihistoria na kwamba mengine ni kulazimisha.

“Naendelea kusisitiza hakuna hoja yoyote ya kiuchumi kuunda mkoa wa Chato. La sivyo basi tuelimishwe. “Ila kama mnapenda siasa za upendeleo wa sehemu fulani ama kwa kuwa mkubwa aliwahi kuzaliwa pale au mtu apewe nafasi kwa sababu ni mtoto wa kiongozi endeleeni kuwabebesha wananchi mizigo ya kulipa kodi kusudi wateule wajichane,” alisisitiza Profesa Tibaijuka.

Alisema Mkoa wa Geita ulianzishwa kwa kusudi la Chato iwe Makao Makuu na hata hivyo ikakosa vigezo mwaka 2010. “Miaka 11 baadaye Chato eti ina vigezo kuwa Makao Makuu ya Mkoa wake wenyewe? Tupo makini na maendeleo yetu kweli? Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan tunataka kweli kumtwisha zigo la kuamua jambo hili?” Alihoji.

Profesa Tibaijuka alisema anazikataa hoja zinazotolewa za kuwaletea maendeleo Kakonko, Biharamulo, Ngara na Muleba inayokatwa vipande. “Mkoa unaweza kuleta maendeleo gani kwa wilaya yake wakati unategemea bajeti ya Serikali Kuu. Mkoa una mapato gani zaidi ya kutumia kodi? Maendeleo yanatokana na uwekezaji na uwezeshaji kwa wananchi.

Siyo watumishi wa Serikali tena baadhi bila maadili wanaweza kuishia kuwabugudhi wananchi badala ya kuwa msaada,” alisema.

Alisema njia pekee kumuenzi hayati Magufuli ni kurekebisha mambo ambayo kama binadamu hakufanya vizuri na kwamba mengine yote ni ubinafsi.

Shija Richard, Mhasibu kitaaluma alisema mzizi wa tatizo linaloibuka kuhusu ukinzani wa kuanzishwa Mkoa wa Chato nyuma ya pazia umegubikwa na sababu za kikabila hasa ugomvi wa kiasili kati ya Biharamulo na Chato.

Mei 29 mwaka huu, kikao maalumu cha ushauri cha Mkoa wa Geita, kiliridhia kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato na kupendekeza mkoa huo mpya kuwa na wilaya tano, huku mkoa mama wa Geita ukibaki na wilaya tatu.

“Miundombinu iliyowekwa Chato siyo kigezo cha kuunda mkoa, bali ikamilishwe na kuitafutia matumizi mbadala ya kitaifa.” aliisema Tibaijuka.

Kikao hicho kilichokuwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule kilipendekeza mkoa mpya wa Chato kuwa na wilaya ya Chato, Bukombe zilizopo mkoa wa Geita kwa sasa na wilaya mbili za mkoa wa Kagera ambazo ni Biharamulo na Ngara, huku ikimega kata tatu kutoka wilaya ya Muleba pamoja na baadhi ya maeneo kutoka wilaya ya Kakonko iliyopo mkoani Kigoma.

Kuanzishwa kwa mkoa huo kunatokana na ombi la mwakilishi wa wazee wa wilaya ya Chato, Samwel Bigambo, alilolitoa kwa Rais Samia Machi 26, wakati wa mazishi ya Magufuli.

Mwakilishi huyo alisema Magufuli aliwaahidi kuwa wilaya ya Chato ingekuwa mkoa. Mkoa mpya wa Chato utakuwa na tarafa 18, kata 87, vijiji 360 huku ukiwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 30,215.85, lenye watu 1,557,139.