Mkandarasi apewa siku 25 kukamilisha mradi Korogwe

Muktasari:

  • Vijiji 27 vya Tarafa ya Mombo wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga, vitanufaika na mradi wa umeme unaogharimu zaidi ya Sh150 milioni.

Korogwe. Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amempa siku 25 mkandarasi wa Kampuni ya Tontan inayotejenga miundombinu ya umeme katika vijiji 27 vya Halmashauri ya Wilaya Korogwe, kuhakikisha umeme unawaka kabla ya Desemba 31.

Akizungumza na wananchi wa katika katika Kijiji cha Sharaka, Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, leo Jumatano Desemba 6, 2023, Naibu Waziri huyo ameagiza mkandarasi huyo kutopewa kazi nyingine na wizara hiyo.

Amesema kazi alizopewa mkandarasi huyo katika kijiji hicho, zimekuwa zikisuasua na mara kwa mara ameongezewa muda kwaajili ya kumaliza mradi lakini hakuna matokeo chanya.

"Wizara tumeshaongea sana na huyu mkandarasi ila haonyeshi juhudi zozote kumalizia kazi anazopewa, hivyo akimaliza hii asipewe nyingine na akabidhi Desemba 31; akishindwa tutajua tunamchukulia hatua gani ila kijiji hiki mradi lazima ukamilike," amesema.

Kwa upande wake Mhandisi miradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) Mkoa wa Tanga, Balisidya Mluya amesema mpaka sasa katika vijijini 118 vya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni 27 tu ndio bado mradi haujafika na kwamba juhudi zinafanyika ili vijiji hivyo vipate umeme.

Amesema kuwa mara nyingi mkandarasi huyo hutoa sababu za mvua na kwamba walipofuatilia, waligundua ana wafanyakazi wachache na vifaa vichache.

Mkandarasi wa Kampuni ya Tontan, Ramayana Molel anayejenga mradi huo, amewaomba radhi wananchi huku akiahidi ifikapo Desemba 31, mwaka huu, atahakikisha umeme unawaka katika vijiji husika.

"Naomba wananchi mnisamehe kwa hili nitahakikisha nina tekeleza agizo la Naibu Waziri, mpaka Desemba 31; mwaka huu, Kijiji cha Sharaka umeme utawaka na zoezo litaendelea katika vijiji vingine," amesema Mollel.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Korogwe, Ali Waziri kwa upande wake amewataka wananchi ambao mradi umepita kwenye maeneo yao, kuhakikisha wanatunza miundombinu yake na kuilinda.

Mkazi wa Makuyuni Samweli Joseph ameishukuru Serikali kwa mradi huo wa umeme, huku akidai kuwa pamoja na mambo mengine walikuwa wanatembea mpaka kilomita saba kwaajili ya kwenda kuchaji simu na kusaga unga, adha ambayo wana imani itakwisha baada ya mradi kukamilika.