Mkandarasi mwendokasi Mbagala aomba aongezewe miezi saba

Muktasari:

  • Zikiwa zimebaki siku nane kabla Mkandarasi anayejenga barabara ya mabasi yaendayo haraka kutoka Gerezani hadi Mbagala kuukamilisha, amewasilisha maombi yakutaka  kuongezewa muda wa miezi saba.

Dar es Salaam. Mkandarasi anayejenga barabara ya mabasi yaendayo haraka awamu ya pili kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu, ameomba kuongezewa muda wa miezi saba ili aweze kuukamilisha.

Barabara hiyo inayojengwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Sino Hydro ilipaswa kukamilika Machi 27, mwaka huu ambapo ujenzi wake umefika asilimia 89 wakati Februari ulipaswa kuwa ufikia asilimia 95.

Februari 27 mwaka huu Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa alipotembelea mradi huo alisema katikati ya Aprili mradi huo utakamilika kwa asilimia 100, awali walipata changamoto ya daraja la juu kwa sababu walichelewa kuwapa eneo.

Akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu leo Jumamosi Machi 18, 2023 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Rogatus Mativila amesema baada ya kupokea maombi hayo wanaendelea kuyafanyia kazi kuhusu uhalali wake.

"Tathmini iliyofanywa inaonyesha kuwa gharama ya mkataba huu itaongezeka kutoka Sh217 bilionii hadi Sh253 bilioni ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 16" ameeleza Mativila.

Amesema sababu nyingine za kuongezeka kwa garama hizo ni pamoja na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali zaidi ya makisio ya awali pamoja na maboresho ya usanifu.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso ameishauri Serikali kuiga mtindo unaotumiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika mikataba yake.

Amesema barabara zinazojengwa kumekuwa na utaratibu wa kuongeza garama zaidi kutokana na utaratibu unaotumika kuingia mkataba na makandarasi.

 "Fuateni utaratibu unaotumika na TRC ili barabara zinazojengwa zisiwe na gharama kubwa, kila kinachoonekana kuongezeka au kukamilisha nje ya wakati vyote hivi ni suala la gharama,"amesema Kakoso.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Chukuzi Profesa Makame Mbarawa

alisema ipo mikataba ya aina tofauti, ikiwemo ile ambayo bei inaweza kubadilika lakini mingine bei haiwezi kubadilika.

"Tumepokea ushauri wa kamati tutaenda kukufanyia kazi kwa namna maelekezo yatakavyokuja,"amesema Profesa Mbarawa.