Mkoa wa Njombe wakamilisha sensa

Muktasari:

  • Mkoa wa Njombe umemaliza dodoso kuu la sensa ya watu kwa zaidi ya asilimia 100 kabla ya siku zilizopangwa kukamilika.

Njombe. Mkoa wa Njombe umemaliza dodoso kuu la sensa ya watu kwa zaidi ya asilimia 100 kabla ya siku zilizopangwa kukamilika.

 Sensa ya Watu na Makazi ilianza Agosti 23, 2022 na itakamilika kesho Jumatatu.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Agosti 28, 2022 na Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka baada ya kupokea taarifa ya uandikishaji wa sensa ya watu na makazi wilaya Makete.

Amesema halmashauri tano za Mkoa wa Njombe zimekamilisha sensa ya watu na makazi kwa asilimia mia moja hivyo imebakia moja ambayo itamaliza leo.

Amesema mkoa huo kesho asubuhi Jumatatu utakabidhiwa rasmi taarifa kutoka katika halmashauri zote za mkoa wa Njombe za ukamilishaji wa sensa ya watu na makazi.

"Kila halmashauri kesho itakabidhi taarifa rasmi ya ukamilishaji wa sensa na kuweza kupongezana kwamba tumemaliza kabla ya wakati kama ambavyo tulitarajia," amesema Mtaka.

Ameipongeza wilaya ya Makete kwa niaba ya halmashauri zote za mkoa wa Njombe pamoja na wananchi kwa kutoa ushirikiano mkubwa na kuwezesha kukamilisha sensa kwa wakati.

Aidha, amewapongeza makarani wote wa sensa mkoa wa Njombe kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kukosekana kwa changamoto yoyote ikiwemo ya ulevi, kisa chochote cha kufanya sensa iweze kuharibika.

"Hatukupata matukio yoyote ya mtu kuibiwa kishkwambi, kuharibikiwa na hata kwenye mazingira magumu waliokwenda visiwani wameweza kujiongeza ili kuhakikisha wanafanikisha sensa," ameongeza Mtaka.

Naye Katibu tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omary ameipongeza wilaya ya Makete kwa kukamilisha sensa ya watu na makazi kwa zaidi ya asilimia 110 ya waliotarajiwa wameweza kuandikishwa.

Amesema Wilaya ya Makete ilijipanga vizuri kwa makarani kufanya kazi yao usiku na mchana ili kuwafikia wananchi ambao wengi wao ni wachapakazi.

"Kwahiyo walikuwa wanaongeza saa za kufanya kazi zaidi wakati wa jioni, wakati watu wametoka kufanya kazi na kuwawahi kabla hawajatoka kwenda shambani," amesema Judica.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Makete, Juma Sweda amesema katika makadirio waliyofanya ya kuandikisha kaya 27,000 wao wameweza kuandikisha sensa ya watu zaidi ya kaya 30,000.

"Tumeandikisha kaya zaidi ya zile ambazo tulikuwa tunategemea tupo zaidi ya asilimia 110.3 ya kazi yote iliyofanyika" amesema Sweda.

Mratibu wa sensa wilaya ya Makete, Aloyce Mwalukisa amesema uhamasishaji ulifanyika kwa kiwango kikubwa na kwa mafanikio makubwa hivyo kusababisha mwitikio wa wananchi katika kushiriki sensa kuwa mkubwa.

"Wananchi wametoa ushirikiano mzuri kwa makarani na kufanya sensa iende vizuri bila vikwazo" amesema Mwalukisa