Mmarekani aeleza ugumu kujifunza Kiswahili akisema ‘choo’ badala ya ‘chuo’

Muktasari:

  • Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (Unesco) lilitangaza Julai 7 kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili Duniani, mwaka huu ni mara ya pili maadhimisho hayo kufanyika duniani kote.

Dar es Salaam. Mwanafunzi wa Marekani kutoka Jimbo la Calfonia, Christa Andeson amewaacha washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili lililofanyika ubalozi wa Marekani nchini Dar es Salaam, wakiangua kicheko baada ya kueleza ugumu aliowahi kukutana na akisema ‘choo’ badala ya kusema neno ‘chuo’.

Christa ameeleza hayo leo Juni 27, 2023 wakati akichangia kwa njia ya mtandao kutoka Marekani. Amesema mipango yake aliyoanza mwaka huu kwa kuanza kusoma Riwaya ya Vuta N’kuvute.

Akizungumza katika maadhimisho hayo ya siku ya Kiswahili, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Consolata Mushi amesema lugha ya Kiswahili imetandaa zaidi duniani ambapo hivi sasa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili wamefikia milioni 500.

“Serikali imefanya juhudi mbalimbali kuhakikisha tunawatumia diaspora katika kusaidia kufundisha Kiswahili duniani,” amesema Mushi ambaye pia ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili

Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Robert Raines amesema Kiswahili sasa siyo tu lugha ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki bali imekuwa lugha ya dunia.

Amesema Marekani imekuwa ikiweka mkazo katika kujifunza lugha ya Kiswahili ili kuendana na mabadiliko ya utamaduni duniani.

Mkuu wa Utawala Ubalozi wa Marekani nchini,  Shan Kenedy ambaye pia ni mwanafunzi aliyejifunza Kiswahili, amesema zaidi ya Wamarekani 100,000 wanazungumza lugha ya Kiswahili katika nchi hiyo.

“Tangu lugha ya Kiswahili itangazwe kuwa lugha ya kimataifa, zaidi vyuo zaidi 100 vinafundisha lugha ya Kiswahili,” ameeleza.

Amesema katika vitu vingi ambavyo wanapenda kujifunza Kiswahili ni kutokana kuwa na semi nyingi ambazo zinawasaidia kufahamu stadi mbalimbali za maisha.

Amesema wapo Wamarekani wengine hapa nchini wanasoma Kiswahili kwa ajili ya kuwawezesha kushiriki miradi mbalimbali ya maendeleo.

Vilevile amesema kwamba sababu nyingine inayowafanya wapende kujifunza Kiswahili ni kuonyesha upendo kwa Watanzania na wafanyakazi wengine wanaofanya kazi katika ubalozi huo.

Akizungumza katika mdahalo huo, Joramu Mkumbi amesema Marekani ina mchango mkubwa katika kukuza Kiswahili duniani kutokana kutumika katika Nyanja mbalimbali za Sanaa kama vile filamu na muziki.

Washiriki wa mdahalo huo walikuwa ni Kituo cha Mafunzo cha MS TCDC Arusha, wafanyakazi, wanafunzi wa Kiswahili wa Ubalozi wa Marekani, Shirika la Wamarekani wa Kujitolea (Peace Corps).

Pia, maadhimisho hayo yaliwashirikisha wanaharakati wa lugha ya Kiswahili, Abdul Fumau ambaye ni mshairi chipukizi pamoja na Seko Shamte anayejishughulisha na kutayarisha filamu.