Mmiliki shule iliyoua watoto kwa ukuta ashikiliwa na polisi

Saturday November 21 2020
By Aurea Simtowe

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linamshikilia mmiliki wa Joy Unit Day Care, ambayo darasa lake liliangukiwa na ukuta na kusababisha vifo vya watoto watatu, likimtuhumu kuendesha bila kibali shule hiyo ya chekechea iliyoko Mtaa wa Kisiwani Kata ya Bonyokwa.

Wakati mmiliki huyo, Atuganile Mbosolelo akikamatwa, pia marehemu Neema Nelson na Blaston Gedi waliofariki katika ajali hiyo, walizikwa jana makaburi ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam na Makanyagio mkoani Iringa.

Akizungumza na Mwananchi jana, kamanda wa polisi wa Ilala, Janeth Magoni alisema wamebaini kuwa shule hiyo, ambayo Serikali iliifunga kwa kuchora rangi nyekundu juzi, haina usajili baada ya kumhoji.

“Tumemkamata, tunaye,” alisema Kamanda Magoni.

“Katika mahojiano yake tumebaini kuwa alikuwa anaendesha kituo kile kwa miaka mitatu bila ya kibali, japokuwa anasema alikuwa katika hatua za kutafuta usajili lakini sheria ni lazima ichukue mkondo wake.

“Lakini bado tunaendelea kumtafuta mmiliki wa nyumba iliyosababisha vifo vya wanafunzi hao. Mpaka sasa tuko katika hatua nzuri, tumemjua.”

Advertisement

Alisema Atuganile atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

“Lakini anaweza kuachiwa kama atakidhi vigezo vya dhamana kwa mujibu wa sheria,” alisema kamanda wa polisi.

Kamanda huyo wa Ilala aliwataka wananchi kuwapeleka watoto wao katika vituo vinavyotambulika na kusajiliwa na Serikali kwa sababu ni salama na hivyo kuepuka athari za matukio kama hayo.

Tukio hilo lilitokea Jumatano wakati ukuta wa nyumba jirani na kituo hicho ulipoangukia darasa na kusababisha maafa ya watoto hao watatu na kujeruhi wengine sita.

Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, uokoaji ulikuwa changamoto, hasa kutokana na barabara kupitika kwa shida na hivyo magari kulazimika kusimama mbali kusubiri wanaookolewa.

Awali alipokuwa akizungumza na Mwananchi siku ya tukio Novemba 18, 2020, mmiliki huyo aliye na miaka 10 katika fani ya ualimu wa shule ya msingi, alisema aliambiwa kuripoti kituo cha polisi siku inayofuata kwa ajili ya mahojiano.

Alisema aliamua kufungua darasa la awali katika eneo la nyumba anayoishi baada ya kuamua kujiajiri na lengo lake kuu likiwa ni kumiliki shule baadaye.

“Polisi walipokuja, mimi nilikuwa hospitali (kupeleka majeruhi), lakini baadaye niliporudi waliniambia kesho uje kwa ajili ya kutoa maelezo,” alisema Atuganile katika mahojiano na Mwananchi siku ya tukio.

Kwa mujibu wake, siku ya tukio darasani kulikuwa na wanafunzi 19 kati ya 29 aliowasajili na mmiliki alisema baadhi wamekuwa hawafiki shuleni mvua zinaponyesha.

Advertisement