MO Dewji aunda jopo la kumshauri Ramaphosa

MO Dewji aunda jopo la kumshauri Ramaphosa

Muktasari:

  • Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amemteua mfanyabiashara kijana nchini, Mohamed Dewji (Mo) kuwa kwenye jopo lake la watu watano kumshauri kuhusu masuala ya uchumi na uwekezaji.

Dar es Salaam. Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amemteua mfanyabiashara kijana nchini, Mohamed Dewji (Mo) kuwa kwenye jopo lake la watu watano kumshauri kuhusu masuala ya uchumi na uwekezaji.

Dewji, ambaye hivi karibuni Jarida maarufu la Forbes limemtaja kuwa bilionea kijana wa 13 kati ya 18 barani Afrika, ameingia kwenye jopo hilo ambalo lengo ni kupanga mikakati ya namna bora ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya Afrika Kusini.

Taarifa kwa vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa Mo Dewji, anayemiliki kampuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL), atakuwa kwenye chombo hicho kwa kipindi cha miaka mitano.

Imesema kuwa uamuzi wa Ramaphosa kumteua Mo Dewji kuwa mshauri wake umetokana na kuvutiwa na jitihada za mfanyabiashara huyo maarufu nchini, kubobea kwenye masuala ua uchumi, huku akiifanya MeTL kuwa miongoni mwa kampuni bora Afrika.

Pia, uteuzi huo umeelezwa kuwa unatokana na Ramaphosa kuthamini na kutambua mchango wa Mo katika uwekezaji ambao umekuwa kichocheo kwa uchumi wa mataifa mbalimbali Afrika.

“Ninayo furaha kubwa kukujulisha kwamba, nimekuteua kwenye Baraza la Ushauri la Rais kuhusu uwekezaji ambalo lina jukumu kubwa kuhakikisha Afrika Kusini inapiga hatua kiuchumi na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

“Imani yangu ni kuwa kwa kutumia umahiri na uzoefu wako kwenye masuala ya biashara, utashirikiana vyema na wajumbe wengine katika kutupa mwanga ili kuongeza tija kwenye ukuaji wa uchumi na kuvutia wawekezaji zaidi,” imesema taarifa hiyo.

Afrika Kusini ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yenye uchumi imara na unaopiga hatua kwa kasi na mikakati ya Rais Ramaphosa ni kuona sera na jitihada zake zinaongeza tija kwenye ukuaji wa uchumi na uwekezaji mpya.

Baraza hilo la ushauri litakuwa jukwaa la kuchakata mawazo, vikwazo na kuangalia njia bora za kukuza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, wadau wa maendeleo na mawakala wa uwekezaji ili Afrika Kusini ipige hatua katika maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia.

Kutokana na uteuzi huo, Mo Dewji atapata fursa ya kuhudhuria vikao mbalimbali vitakavyoandaliwa ndani na nje ya Afrika Kusini vitakavyohusisha wafanyabiashara, viongozi wa Serikali ikiwa ni ukuzaji wa uchumi na kuwavutia wawekezaji.