Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mongella: Watoto wa kiume wasisahaulike

Muktasari:

 Mongella amesema vijana wa kiume, wanawake ndiyo mama, hivyo nguvu kubwa pia inahitajika katika kuwawezesha vijana wa kiume

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe nchini, Getrude Mongella amesema katika kutengeneza safari ya mwanamke pia vijana wa kiume wasisahaulike.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa taasisi inayowasaidia wanawake kisheria ya Safari ya Mwanamke Foundation, jana mwanasiasa huyo amesema: “Vijana wa kiume tutawapoteza na ikifikia mahali tukawapoteza, basi hata hawa watoto wa kike tunaohangaika nao watapata shida kwa sababu wataolewa na wanaume wasiojielewa.”

 Mongella amesema vijana wa kiume, wanawake ndiyo mama zao na jambo hilo analichukulia kwa uzito, hivyo nguvu kubwa pia inahitajika katika kuwawezesha vijana wa kiume.

Rebeca Gyumi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msichana Initiative, amesema msingi wa hilo umejielekeza kwenye kuangalia jitihada zinazowekezwa kwa mtoto wa kike kama jitihada za kibaguzi.

Amesema jitihada za kumuwezesha mtoto wa kike kupata fursa zaidi zinapaswa kuangaliwa kwa jicho la tofauti.

Gyumi amesema kuna changamoto nyingi anazopitia mtoto wa kike ndio maana kuna jitihada mahususi za kumuangalia mtoto huyo.  Pia, amesema kwa maono yake mtoto wa kiume yupo tayari katika fursa mbalimbali. 

“Fursa mbalimbali mtoto wa kiume tayari yupo mfano hata kwenye ushiriki wa siasa. Si kwamba mtoto wa kiume anahitaji juhudi kumuwezesha lakini kwa watoto wa kike inahitajika jitihada kwa sababu tayari kuna tamaduni za kijinsia, zitakazomfanya mtoto wa kike aanze kujiuliza maswali ajiingize au la,” amesema Gyumi alipotafutwa na Mwananchi Digital.

Mwanaharakati wa haki za wanawake, Glory Olomi ambaye kwa sasa yupo nchini Ujerumani amesema anachokiona uwezeshwaji usiwe wa ulinganifu na wanaume.

“Nafikiria katika kizazi kijacho inawezekana zikatokea harakati za kuwainua tena wanaume, kwa sababu kwa sasa wanawake wanazaliwa wanakutana na milango na nafasi zao zikipambaniwa zaidi.

“Lazima kuwe na uzani sawa ila tukitaka kuwasha mishumaa ya wanawake huku tunazima ya wanaume au kuwabeza hatutatengeneza usawa,” amesema Olomi. 

Mwanasaikolojia Modester Kimonga amesema suala la kusahaulika kwa mtoto wa kiume maana yake taarifa zake zinakuwa hazifiki jambo amblo linaloweza kumnyong’onyeza.

“Piga hesabu miaka kumi inayokuja kama kila kitu atawekewa mtoto wa kike na kusahaulika kwa mwanamume mawazo yake tutayakosa. Hivyo tunapaswa kuwekeza nguvu pande zote ili kupata matokeo bora,” amebainisha Kimonga.

Mkurugenzi wa Safari ya Mwanamke Foundation, Georgia Kamina amesema wanawake wanapitia changamoto katika maisha yao sasa, hivyo taasisi hiyo  inataka kutatua vikwazo vinavyomkwamisha kufikia malengo yake ya kimaisha hususani kisheria.

“Lengo la kuianzisha ni kuwawezesha wanawake na mabinti wa Kitanzania hususani kisheria,” amesema Kamina.