Moto wateketeza ghala Tanga

Muktasari:

  • Ghala lililokuwa limehifadhia shehena za bidhaa za magendo ambazo zimeshindwa kulipiwa ushuru na wafanyabiashara limeteketea kwa moto katika Bandari ya Tanga huku chanzo kikiwa bado hakijajulikana.

Tanga. Ghala lililokuwa limehifadhia shehena za bidhaa za magendo ambazo zimeshindwa kulipiwa ushuru na wafanyabiashara limeteketea kwa moto katika Bandari ya Tanga huku chanzo kikiwa bado hakijajulikana.

Ghala hilo linalomilikiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Tanga, lilikuwa na vitu mbalimbali yakiwamo mabalo ya vitenge 370, sukari, mchele, mafuta ya kupikia na pikipiki.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio leo Jumapili Oktoba 23, 2022, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba amesema alipata taarifa ya kuteketea kuwa ghala hilo usiku na kufika eneo la tukio.

Amesema kuwa walihakikisha kuwa wanazima moto huo ndipo watafanya uchunguzi ili kubaini chanzo kilichosababisha moto huo.

"Kwa Sasa tunahakikisha usalama wa mali zilizobaki katika eneo hilo baada ya hapo tutaunda timu maalumu ya kufanya uchunguzi wa kina wa chanzo cha tukio hilo na sababu za kuzuka kwa moto huo kabla ya kuchukuwa hatua zaidi," alisema RC Mgumba.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tanga, Fatma Ngenya amesema kuwa walipokea taarifa za moto kutoka Mamlaka ya Bandari Tanga saa nane na nusu usiku na walifanikiwa kufika eneo la tukio.