MPox yawa tishio duniani, panya wahusishwa
Muktasari:
- Wakati virusi vya homa ya nyani, maarufu ‘Mpox’ vikizidi kusambaa nchi mbalimbali duniani, wataalamu wa uchunguzi wa virusi na vimelea vya magonjwa wamebaini chanzo kipya cha virusi hivyo ni pamoja na panya wa msituni na si nyani pekee.
Dar es Salaam. Wataalamu wa uchunguzi wa virusi na vimelea vya magonjwa wamebaini chanzo cha virusi vya homa ya nyani, maarufu ‘Mpox’ ni pamoja na panya wa msituni na si nyani pekee.
Taarifa hizo zinatolewa baada ya miaka mingi kuaminika kuwa chanzo pekee cha homa hiyo ni nyani wanaopatikana Afrika ya Kati na Magharibi.
Aina mpya ya homa ya nyani imesababisha mamia ya vifo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na imeenea katika maeneo ya Afrika ya Kati, Mashariki na mabara kadhaa duniani.
Hayo yamebainishwa jana Jumamosi, Agosti 24, 2024 na Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Profesa Hamis Malebo wakati akizungumza katika mdahalo ulioendeshwa na Wizara ya Afya kupitia mtandao wa X uliokuwa na mada isemayo; ‘Elimu kuhusu ugonjwa wa Mpox, Jikinge; iweke Tanzania salama dhidi ya Mpox.’
“Wataalamu wa uchunguzi wa virusi na vimelea vya magonjwa wameonyesha shaka na jina la homa ya nyani, kwa sababu sasa hivi imegundulika rasmi nyani siyo chanzo pekee cha virusi hivi, ila ni pamoja na panya wa msituni waliopo katika misitu ya Afrika ya Kati na Magharibi,” amesema.
Profesa Malebo amesema mlipuko wa hivi karibuni ndiyo mkubwa kuwahi kutokea kuliko yote ya awali kwa kuwa una idadi kubwa ya wagonjwa ukilinganisha na mingine, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Takwimu za WHO zinaonyesha kwamba kwa mwaka huu 2024, kipindi cha miezi sita iliyopita wameripotiwa wagonjwa 1,854 barani Afrika na hao ni asilimia 36, jumla ya watu 5,199 wameathirika,” amesema na kuongeza;
“Kati ya hao asilimia 95 wametokea DRC ikimaanisha kwamba katika wagonjwa 1,854 barani Afrika 1,754 wametoka DRC na mpaka sasa kuna vifo 500 vimesharipotiwa kwa ugonjwa huu.”
Mkurugenzi msaidizi wa elimu ya afya kwa umma, Wizara ya Afya Dk Norman Jonas amesema vipele hivyo vinavyouma na kuwasha, pia hutengeneza mbonyeo baada ya kupona na kwamba kwa upande wa matibabu wagonjwa hutibiwa kutokana na dalili.
“Mwingine anaweza kupata vipele na homa kidogo na akapewa dawa kwa ajili ya ngozi na kuondoa homa aliyoipata, lakini mwingine anaweza kupata ugonjwa mkali na wengine huweza kuleta athari mpaka kwenye figo na ini,” amesema.
Amesema Wizara imejipanga na inapotokea mgonjwa ni jukumu kuhakikisha anapata maji ya kutosha, lishe bora, “Tunamtenga asiendelee kupata maambukizi mapya au asipate shida zaidi kwenye ngozi yake. Mpaka sasa tumejipanga na tumeshatoa elimu katika vyombo vya habari, vyombo vya usafiri, mwendokasi, mabasi, mikusanyiko, hospitalini na tupo mbioni kufika katika usafiri wa SGR,”amesema Dk Jonas.
Maabara yajipanga
Tangu kutokea kwa mlipuko huko DRC, Tanzania imekuwa ikijipanga katika hatua kadhaa za kudhibiti ugonjwa huo kwenye mipaka, ikiwemo kuandaa maabara kuwa na uwezo wa utambuzi kama asemavyo Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL), Dk Nyambura Moremi.
Amesema kutokana na kujibadilisha kwa virusi hivyo, maabara zipo tayari kutambua na wataalamu wameshapatiwa elimu kuhusu utofauti wa virusi vya Clade 1 inayopatikana Congo na Clade 2 inayopatikana Afrika Magharibi.
“Unapima mlolongo wa vinasaba, Tanzania tuna uwezo wa kutambua aina ya kirusi na ukanda vilipoonekana. Virusi hivi vimeanza kujibadilisha vinasaba, vinazaliwa vitoto ndani ya clade one inaonekana hatari zaidi mwanzoni tulikuwa tunaambiwa kwamba pengine ipo daraja B vina madaraja, uhatari wake unaweza kufikia daraja A kwenye ugonjwa mkali muda wowote,” amesema.
Amesema maabara ya Taifa ina uwezo wa kupima sampuli hizo kwa kuwa ipo ngazi ya usalama ya tatu kiubora kwa maabara ya Taifa na Kibong'oto ipo daraja la 3 pia.
Akielezea tabia ya virusi hivyo, Dk Nyambura amesema hupatikana kwenye damu na maji maji ya mgonjwa.
“Tafiti zilizopo zina ushahidi kwamba virusi zaidi vinapatikana kwenye vile vipele, ukija na vile vipele wataalamu wetu baada ya kujikinga watakitumbua na kuchukua ‘swab’ (majimaji) kama tulivyofanya kwenye Uviko19, na wanaweza wakalitoa gamba tukalichukua pia kama sampuli,” amesema Dk Nyambura.
Amesema kwa sasa mafunzo yanaendelea ingawa bado hakuna mgonjwa aliyehisiwa wala kubainika na kwamba mikakati mizuri imewekwa, “Kuanzia ngazi ya wilaya na mkoa, Uviko19 ilitusaidia tunasafirisha sampuli ndani ya saa 24 na ndani ya saa 4 kipimo kitabaini, pia tunazo maabara jongezi kukiwa na uhitaji mkubwa tuna uwezo wa kupeleka.”
Kwa upande wake Mkuu wa Huduma za Dharura, Wizara ya Afya, Dk Erasto Sylvanus amesema mpaka sasa timu za afya mipakani zinafanya kazi zikishirikisha vyombo vyote vya Serikali.
“Waziri wa Afya ameeleza hili jambo si la Afrika ni la watu wote, haimaanishi tubweteke tunapaswa tuweke bidii kwenye ugunduzi, tayari tumeanza na hatujapata mgonjwa mpaka sasa.”
“Suala jingine ni dawa na vifaa tiba, Serikali imewekeza na ikiwa atatokea mgonjwa tumejipanga kutoa tiba lakini kudhibiti ugonjwa usisambae,” amesema.
Akielezea athari baada ya ugonjwa, Dk Sylivanus amesema mgonjwa wa Mpox anapopona kama alipata vipele vikubwa huwa vinaacha makovu, wengi huwa yanaisha na wengine kutokana na mwili ulivyopokea huwa wanabaki nayo.
“Kuna tafiti zimeonyesha kwa wale ambao kinga zimeshuka mengine yanachukua muda kuja kuisha na wale ambao makovu hayo yametokea madogo na muda mfupi, mengi huwa yanaacha alama ndogo kwenye ngozi,” amesema.
Wakati huohuo, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha limetoa tamko lake likiwataka waumini wawe na tahadhari za kiafya dhidi ya homa ya nyani.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Askofu Mkuu wa jimbo hilo, Mhasham Isaac Amani imeeleza kuwepo kwa hali ya dharura kutokana na uwepo wa homa hiyo katika baadhi ya nchi jirani, kutokana na mwingiliano mkubwa, hivyo kuwataka kuchukua tahadhari.
Amewataka waumini kuepuka kusalimiana kwa mikono, akisitisha kushikana mikono wakati wa kutakiana amani kwenye misa hata nje.
“Tuepuke kukumbatiana, tucheze muziki kwa kutogusana, kutumia vitakasa mikono, sabuni na maji tiririka kila mahali ambayo yanawekwa kila mara. Tufuate miongozo iliyotolewa na WHO ni matumaini yangu kwamba tahadhari hizo zitazingatiwa kiaminifu, katika roho ya kujitambua, kuwajibika na kushirikiana katika Kristo kwa matendo,” amesema Mhasham Amani.