Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mramba, Yona sasa kufagia hospitali Dar

Muktasari:

Mramba aliyewahi kuwa waziri wizara mbalimbali ikiwamo ya Fedha na Yona ambaye pia aliwahi kwa waziri katika wizara mbalimbali ikiwamo ya Nishati na Madini walihukumiwa adhabu hiyo Julai 6, 2015 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.5 bilioni, kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya M/S. Alex Stewart Government Business Assayers ya Uingereza.

Dar es Salaam. Mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona waliokuwa wakitumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela, wamebadilishiwa adhabu kuwa kifungo cha nje na sasa watakuwa wanafagia Hospitali ya Sinza, Palestina kwa saa nne kila siku.

Mramba aliyewahi kuwa waziri wizara mbalimbali ikiwamo ya Fedha na Yona ambaye pia aliwahi kwa waziri katika wizara mbalimbali ikiwamo ya Nishati na Madini walihukumiwa adhabu hiyo Julai 6, 2015 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.5 bilioni, kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya M/S. Alex Stewart Government Business Assayers ya Uingereza.

Jana, Mahakama hiyo iliamuru wafungwa hao wabadilishiwe kifungo kutoka gerezani na kuwa cha nje kumalizia sehemu ya adhabu yao ya miaka miwili iliyobakia kwa kufanya huduma za kijamii.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Cyprian Mkeha alisema wafungwa hao watakuwa wakifanya shughuli za usafi katika Hospitali ya Sinza Palestina kwa muda wa saa nne kila siku kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa.

Utaratibu huo utaendelea hadi Novemba 5, mwaka huu watakapomaliza adhabu yao hiyo.

Hadi wanabadilishiwa adhabu hiyo jana, tayari walikuwa wameshatumia kifungo hicho jela kwa kipindi cha mwaka mmoja kasoro siku moja.

Uamuzi wa kuwabadilishia adhabu mawaziri hao wa zamani, ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Uongozi wa Jeshi la Magereza, kuwa Mramba na Yona ni miongoni mwa wafungwa wenye sifa za kupewa kifungo cha nje.

Maombi na orodha ya wafungwa hao wenye sifa za kupewa kifungo cha nje iliwasilishwa mahakamani hapo Desemba 5, 2015 chini ya kifungu cha 3 (1) cha Sheria namba 6 ya mwaka 2002 ya Huduma kwa Jamii.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu yeyote aliyetiwa hatiani kwa kosa ambao adhabu yake haizidi miaka mitatu na faini au bila faini, Mahakama inaweza kumpa adhabu ya kufanya shughuli za kijamii.

Hata hivyo, vigezo au sifa za mfungwa kustahili kupewa adhabu ya kifungo cha nje na kufanya huduma za kijamii ni pamoja na umri (miaka 75), kuwa na familia, kama kosa lake ni la kwanza na kama anajutia kosa hilo.

Vigezo au sifa nyingine ni kama yuko tayari kufanya shughuli za kijamii bila kulipwa, kama kuna uwezekano wa kupatikana kwa mtu wa kumsimamia wakati akitumikia adhabu ya kufanya kazi hizo za kijamii.

Mahakama baada ya kupokea maombi hayo kutoka kwa Magereza iliyawasilisha kwa Idara ya Ustawi wa Jamii ili kujiridhisha kama wanastahili adhabu hiyo.

Baada ya uchunguzi wa idara hiyo, jana Mramba na Yona waliitwa mahakamani hapo na baada ya Hakimu Mkeha kujiridhisha aliamuru wakamalizie adhabu yao nje ya gereza kuanzia jana.

Hata hivyo, kuanza kwa adhabu hiyo mpya kwa mawaziri hao wa zamani kunategemea Magereza kukamilisha taratibu zake za kiutawala.

Kesi ya msingi

Mramba, Yona pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Grey Mgonja wote kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na jumla ya mashtaka 11 ya kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.

Walidaiwa kuwa wakiwa watumishi wa umma walitumia vibaya madaraka yao kwa nafasi zao na kuisababishia Serikali hasara ya kiasi hicho cha pesa.

Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Jaji John Utamwa, Jaji Sam Rumanyika na Saul Kinemela, lakini wakati wa hukumu jopo hilo lilitofautiana na hivyo kuwa na hukumu mbili.

Hukumu ya kwanza ilikuwa ya wengi (wawili) ambayo iliwatia hatiani Mramba na Yona na kumwachia huru Mgonja, iliyosomwa na Jaji Rumanyika na hukumu ya wachache (mmoja) ambayo hata hivyo, haikusomwa siku hiyo.

Mramba na Yona walitiwa hatiani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na katika kosa la kuisababishia Serikali hasara walihukumiwa kulipa faini ya Sh5 milioni kila mmoja.

Baadaye walikata rufaa Mahakama Kuu, wakipinga hukumu hiyo na adhabu hiyo.

Wakati wakikata rufaa, Serikali pia kwa upande wake ilikata rufaa dhidi yao ikipinga adhabu waliyoepewa ya kulipa fidia ya Sh5 milioni badala ya kulipa hasara yote waliyoisababisha.

Pia, Serikali ilikata rufaa dhidi ya Mgonja ikipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu kumwachia huru.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa jana na Jaji Projest Rugazia aliyekuwa akisikiliza rufaa hizo zote, alikubaliana na hoja moja ya rufaa ya Mramba na Yona kuwa adhabu waliyopewa ni kubwa lakini akatupilia mbali hoja za rufaa za kutaka hukumu iliyowatia hatiani ibatilishwe.

Jaji Rugazia alikubaliana na hoja ya kwamba kwa mujibu wa mashtaka yaliyowatia hatiani ya matumizi mabaya ya ofisi na kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha Kanuni za Adhabu (PC) ambacho Mahakama ilikitumia walipaswa kupewa adhabu ya kifungo cha miaka miwili na si mitatu.

Hivyo, Jaji Rugazi aliwapunguzia adhabu hiyo hadi miaka miwili jela, huku akitupilia mbali rufaa ya Serikali dhidi ya Mgonja kwa kuwa hapakuwa na ushahidi wa kumtia hatiani.

Licha ya kuwapunguzia adhabu hiyo, Jaji Rugazia alieleza kushangazwa na sheria nyingine jinsi zisivyokidhi matakwa kwa kutoa adhabu ndogo kulinganisha na makosa husika.