Mshtuko wanasoka na dawa za kulevya

Muktasari:

 Wanasoka wamekumbwa na mshtuko kufuatia taarifa za kukamatwa kwa Kocha wa makipa wa Klabu ya Simba, Muharami Sultan (40) akidaiwa kuwa na dawa za kulevya.

  

Dar es Salaam. Wanasoka wamekumbwa na mshtuko kufuatia taarifa za kukamatwa kwa Kocha wa makipa wa Klabu ya Simba, Muharami Sultan (40) akidaiwa kuwa na dawa za kulevya.

Muharami ni miongoni mwa watuhumiwa 11 wa dawa za kulevya waliokamatwa na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) wakidaiwa kuwa na kilo 34.89 za heroine na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa bangi.

Hatua hiyo imezua mshutuko na mijadala miongoni mwa wanamichezo kutokana na kuwepo kwa matukio kama hayo yanayojirudia.

Mbali na kocha wa makipa wa Simba ambaye klabu hiyo imemkana, wengine waliokamatwa ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Dar es Salaam, Kambi Zuberi Seif na John John, maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka kwenye kituo hicho.

Wengine ni Said Matwiko, mkazi wa Magole, Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa Kisemvule, Rajabu Dhahabu (32) mkazi wa Tabata, Seleman Matola Said (24), mkazi wa Temeke Wailes, Hussein Pazi (24) mfanyabiashara na Ramadhani Chalamila (27) mkazi wa Kongowe.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya alisema watuhumiwa hao walikamatwa na dawa za kulevya aina ya heroine katika maeneo mbalimbali nchini.

Ingawa Kusaya hakueleza zaidi jinsi walivyokamatwa, gazeti hili limedokezwa Muharami alikamatwa takribani wiki mbili zilizopita kwenye kambi ya timu hiyo, Mbweni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam akiwa kwenye majukumu ya timu ilipokuwa ikijiandaa na moja ya mechi za Ligi Kuu.

Mmiliki wa Cambiasso alikamatwa wiki tatu zilipopita kwa mujibu wa mtu wa karibu na kituo hicho ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe.

Cambiasso ni moja ya akademia za soka zilizojipambanua kwa muda mrefu, ikiwa na historia ya kuibua na kuendeleza vipaji vya soka.

Si tatizo la Simba

Baada ya DCEA kutoa taarifa hiyo, mijadala iliibuka kwa kasi katika mitandao ya kijamii, huku Simba ikitoa taarifa kujitenga na kadhia hiyo.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alilieleza Mwananchi kuwa suala la Muharami ni lake binafsi na halihusiani na klabu hiyo.

“Watu watulie, kocha Muharami alikuwa kwa muda Simba,” alisema Mangungu.

“Alikuwa kwenye benchi letu kwa mechi kadhaa, ikiwemo ya Malawi (Simba ilicheza na Nyassa Big Bullets) na kwenye mechi na Angola (Primeiro de Agosto), lakini yule ni kocha wa Cambiasso. Kilichotokea ni masuala yake binafsi,” alisema Mangungu, aliyewahi kuwa mbunge wa Kilwa, Mkoa wa Lindi.

Taarifa ya Simba baadaye ilifafanua kuwa Muharami hakuwa muajiriwa wa klabu hiyo.

“Simba ilimuomba na kukubaliana na Muharami kuwanoa makipa wetu kwa muda wa mwezi mmoja, wakati huo klabu ikiendelea kutafuta kocha wa magolikipa. Kwa mantiki hiyo klabu haihusiki na tuhuma zinazomkabili kocha huyu,” ilieleza taarifa hiyo.

Baadaye mchana jana, timu hiyo ilimtangaza Chlouma Zakaria, raia wa Morocco kuwa kocha wa makipa.

Matukio michezoni

Hii si mara ya kwanza kwa wanamichezo kudaiwa na wengine kupatikana na hatia zinazohusiana na dawa za kulevya.

Tukio kama hilo limewahi kuikumba familia ya michezo mwaka 2008, pale timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa ilipokamatwa nchini Mauritius ikituhumiwa kula njama na kusafirisha heroine.

Timu hiyo ilikwenda nchini humo kuweka kambi kujiandaa na Olimpiki ya msimu huo, iliyofanyika China.

Bondia Emmilian Patrick, aliyekuwa amefuzu Olimpiki na kocha Nassor Michael waliachiwa huru miaka kadhaa baadaye, wakati bondia mwingine, Petro Mtagwa aliyekwenda kama msaidizi wa mazoezi na wengine wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 15 nchini humo tangu Agosti 20, 2016.

Hapa nchini, aliyekuwa rais wa Chama cha Ngumi, Alhaji Shaban Mintanga pia aliachiwa huru.

Septemba 2013, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Joseph Kaniki na bondia Mkwanda Matumla walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa nchini Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Wawili hao walikuwa wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kwenda Paris, Ufaransa.

Wanamichezo hao baadaye walihukumiwa miaka saba na nusu jela.

Taswira ya michezo shakani

Wadau mbalimbali wamezungumzia tukio hilo, akiwemo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Ally Mayay aliyesema ingawa bado ni tuhuma, lakini kwa viongozi linapaswa kuwaamsha na kuwakumbusha suala la maadili kwa watu wanaoshughulika nao.

“Hilo ni suala binafsi, lakini linapogusa wadau wa tasnia fulani kuna mguso fulani, hivyo niwakumbushe tu viongozi na wadau wengine kwenye michezo kuzingatia maadili na watu wanaofanyanao kazi.

“Kama mtu yuko kwenye tasnia iliyosababisha awe maarufu, basi hana budi kuzingatia suala la maadili kwa ukubwa wake, japo kuna ‘ishu’ binafsi, lakini ni vema tukazingatia maadili.

“Ndiyo sababu kuna watu ili kuingia ubia au makubaliano huwa wanaangalia kwanza historia ya nyuma,” alisema Mayay, aliyewahi kuchezea Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars.

Alichokieleza Mayay kinaungwa mkono na Nassor Michael, aliyewahi kukamatwa kwa tuhuma kama hizo mwaka 2008 nchini Mauritius na baadaye kuachiwa, aliyesema matukio hayo kwenye michezoni yana athari kubwa, akijitolea mfano yeye alipokamatwa akiwa ndiye mkuu wa msafara wa timu ya Tanzania.

“Hadi kuachiwa huru ni Mungu tu, mimi ndiye nilikuwa mkuu wa msafara kwenye ile safari, lakini hadi tunakamatwa hotelini sikujua chochote, alianza kuachiwa Emmilian, baadaye mimi kwa kuwa hatukuwa hata na cha kujitetea mahakamani, wenzetu walibaki kule na hadi sasa wanatumikia kifungo.

“Ila ninachoweza kusema matukio haya si mazuri, yanachafua taswira ya michezo inapobainika ni kweli tukio hilo limetendeka,” alisema Nassor, kocha na bondia wa zamani wa timu ya Taifa.

Bondia mwingine aliyeomba hifadhi ya jina alisema mara nyingi wanamichezo huwa wanashawishiwa na watu ambao si wanamichezo na kujikuta wakiingia kwenye mkumbo huo.

“Nakumbuka mimi niliwahi kufuatwa hotelini na mdada mrembo, alinishawishi nibebe dawa nikiwa nakwenda kupigana nje ya nchi, ila namshukuru Mungu nilikiepuka kikombe hicho. Si picha nzuri inapobainika ni kweli na kutiwa hatiani, bora zibaki kuwa tuhuma tu,” alisema.

Biskuti za bangi

Katika hatua nyingine, Kamishna Jenerali wa DCEA, Kusaya katika mkutano wake na wanahabari alisema mamlaka hiyo imemkamata Abdulnasir Haruon Komba (30), mkazi wa Kaloleni Arusha akiwa na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa bangi akiwa anaziuza katika eneo la Kaloleni.

Alisema mwingine aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Hassan Ismail (25), mkazi wa Olasiti jijini Arusha, anayesadikiwa ndiye mtengenezaji wa biskuti hizo zenye dawa za kulevya. Alisema wanunuzi wakubwa wa biskuti hizo ni wanawake ambao wamekuwa wakizitumia na zinawasababishia athari, ikiwemo kupata ugonjwa wa akili na ugumba.

Kusaya alisema wanawake hao wanapotumia biskuti hizo, athari nyingine wanazokutana nazo ni kupata ugonjwa wa figo, maini, mapafu na saratani mbalimbali.

“Wanapokula biskuti hizo wanadai kusikia raha sana, lakini athari yake ni kubwa na unapokula inakimbilia kichwani, matokeo yake unapata matatizo ya afya ya akili,” alisema Kusaya.

“Ukamataji huu unafanyika kufuatia operesheni endelevu tunazozifanya katika maeneo mbalimbali nchini, mwanzo tulimkamata mtu mmoja hadi kufikia idadi hiyo (watu 11) na watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika,” alisema Kusaya.