Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msongola Dar mguu sawa El-Nino

Wananchi wa Yangeyange wakijaza kifusi kwenye moja ya kivuko cha mtaa huo maarufu Chakenge.

Muktasari:

  • Wananchi wa Kata Msongola, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam wameamua kujihami na madhara yatokanayo na mvua za El-Nino kama zilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), ambapo Sh23 milioni zimetumika kujenga madaraja mitatu.

Dar es Salaam. Wananchi wa Kata Msongola, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam wameamua kujihami na madhara yatokanayo na mvua za El-Nino kama zilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), ambapo Sh23 milioni zimetumika kujenga madaraja mitatu.

 Wananchi hao wakishirikiana na Mwenyekiti wa Mtaa wa Yangeyange, Mrisho Goha, wamechukua hatua hiyo kama kama sehemu ya wao kushiriki shughuli za kujitolea bila kungoja Serikali.

Mwananchi Digital limetembelea maeneo hayo leo Jumamosi Oktoba 21, 2023 na kujionea harakati zilizokuwa zikiendelea za kujaza vifusi kwenye moja ya maraja hayo, katika eneo la Chakenge Mtaa wa Yangeyange, Kata ya Msongola.

Akizungumzia ujenzi huo Goha amesema wameshatengeneza vivuko vitatu katika maeneo yanayojaa maji ambayo ni Serunge kwa Chopa, Kwa Mpelela na Chakenge kwa kushirikiana na wananchi ambapo kwa upande wa Chakenge wananchi wamechangia Sh7 milioni kwa ajili ya ujenzi wa eneo lao.

Amesema ili kuendelea na ujenzi huo baadhi ya wakazi wa eneo la Chakenge waliamua kukusanya michango kwa bodaboda na magari yaliyokatisha katika eneo hilo, kama njia ya kupata fedha za vifaa amvavyo vimetumika katika ujenzi huo.

"Niliongea na wananchi kuhusu mvua zilizotangazwa na TMA tukakubaliana nini cha kufanya kwa awamu ya kwanza, huku tukiendelea kupambana namna ya kupata msaada kutoka Serikalini, ili kuepukana na adha inayowakuta wananchi wa mitaa yangu," amesema Goha.

Pia Goha amesema alishawasiliana na viongozi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya la Ilala ili wawasaidie katika kuweka vifusi kwa maeneo mengine ambayo yana makorongo yaliyosababishwa na mvua.

Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kata ya Msongola Ibrahimu Marwa amesema kwa mateso waliyopata kwa kipindi chote hawana budi kumuunga mkono juhudi za mwenyekiti huyo na kwamba baadhi ya vitu akitumia fedha zake binafsi.

"Katika jambo la maendeleo tunaweka siasa pembeni na kuungana na wenzetu ili kufanyakazi kwa sasa tumeona anachokifanya ni kwa ajili ya wananchi na sisi tulikuwa tunapigania hili jambo kwa muda mrefu, hivyo tunaona umuhimu wa wananchi kujitokeza na kuungana naye katika kuleta maendeleo Msongola," amesema.

Amesema wakati wa mvua eneo hilo hujaa maji na hivyo kuwafanya wananchi wa Chakenge na mitaa mingine kukosa mawasiliano.

Pia amesema kipindi cha mvua wakazi wa Jumba la dhahabu wanashindwa kwenda na kurudi kwenye shughuli zao kwa kuhofia kuzolewa na maji yanayojaa kwenye eneo la daraja hilo.

Joel Samo mkazi wa Yangeyange amesema: "Sisi tumemuunga mkono mwenyekiti wetu kwa kuona namna anavyopambana, mvua zikinyesha watoto wetu tunawahurumia kwa sababu wanasoma shule upande wa pili na huduma zote za kijamii pia zipo huko, hivyo tunaomba Serikali iongeze nguvu," amesema.

Christina Okololo ameiomba serikali iwasidie kuongeza vifaa vilivyo imara: “Japo tumejitahiji kujenga haya madaraja, ila siyo ya kudumu hivyo tunaomba Serikali itusaidie vifaa zaidi na ikiwezekana kuwe na wataalamu,”

Ameongeza kusema kuwa: “...wakati mwingine tunashindwa kupata huduma kwa haraka hususani kwa wajawazito kutokana na njia tunazopita ni ngumu kwa kipindi cha mvua."