Msururu wa magari wafunga barabara msafara wa Lema

Muktasari:

Msafara wa magari na pikipiki katika mapokezi ya aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema umefunga barabara ya Arusha-Moshi.

  

Arusha. Msafara wa magari na pikipiki katika mapokezi ya aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema umefunga barabara ya Arusha-Moshi.

Lema amewasili leo Jumatano Machi 1, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjarao (KIA) akitokea Canada alikokimbilia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Lema amewasili mchana akiwa na familia yake na kupokewa na mamia ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mapokezi ya Lema yameanza katika uwanja wa KIA na kuelekea Arusha na kusababisha foleni ya magari yanayotoka Arusha na Moshi.

Lema licha ya kupokelewa na umati wa watu amekuwa akishuka vituo kadhaa kufungua matawi ya chadema na kuzungumza na Wananchi waliofurika barabarani.

Akizungumza na Wananchi wa eneo la kituo cha mabasi cha KIA na King'ori wilaya ya Arumeru, Lema amesema amerudi nchini kwa mapenzi ya Mungu.

"Nashukuru sana leo nimerejea nchini, haya ni mapenzi ya Mungu wapo ambao hawakupenda lakini wameshindwa nimerejea kuungana na Makamanda wengine wa Chadema kuleta demokrasia amani na upendo kwa wote.

Msafara wa Lema bado haujafika Arusha ambapo atakuwa na mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Relini na atapokelewa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, freeman Mbowe.