Mtaalamu wa mashine za EFD arudisha fomu ya uspika

Mtaalamu wa mashine za EFD arudisha fomu ya uspika

Muktasari:

  • Kujiuzulu kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kumetoa nafasi kwa CCM kuruhusu wanaotaka kuwania uspika kupitia chama hicho kuchukua na kurudisha fomu kuanzia Januari 10 hadi 15, 2022 ambapo hadi sasa makada 49 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Dar es Salaam. Msimamizi wa mashine za kutolea risiti za malipo kimtandao (EFDs) mkoa wa Dar es Salaam, Hamidu Chamani amerudisha fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya uspika.

Chamani ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kodi, alichukua fomu hiyo Januari 10 na leo Ijumaa Januari 14, 2022 amerudisha fomu hizo katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba jijini hapa.

Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hizo, Chamani amesema anaamini anao uwezo wa kuongoza Bunge na kukisaidia chama chake katika kuleta maendeleo ya nchi.

Januari 6, 2022, Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kuwepo kwa taharuki juu ya utata wa kauli yake juu ya mikopo inayochukuliwa na serikali chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kujiuzulu kwa Ndugai kumetoa nafasi kwa CCM kuruhusu wanaotaka kuwania uspika kupitia chama hicho kuchukua na kurudisha fomu kuanzia Januari 10 hadi 15, 2022 ambapo hadi sasa makada 49 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Chamani aliyewahi kuwania ubunge katika jimbo la Kyerwa mkoani Kagera mwaka 2020, amesema licha ya idadi kubwa ya waliojitokeza kuwania nafasi hiyo haimpi tabu kwa kuwa anaamini yeye ni bora zaidi yao.

“Nimefanya kazi za kukitangaza chama tangu mwaka 2010 nimehamasisha vijana wengi wa vyuo vikuu wapatao 500 kujiunga na CCM wapo wengine niliowapatia kadi kwa mkono wangu, hivyo ninaamini nina kila sifa ya kuteuliwa kukalia kiti hicho,” amesema Chamani.