Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtanzania anayeishi Afrika Kusini adai shangingi la wahamiaji haramu ni lake

Muktasari:

  • Baada ya gari hilo kukamatwa, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga alisimulia namna wahamiaji hao walivyokamatwa wakiwa katika gari hilo na kuwa dereva aliyekuwa akiliendesha alifanikiwa kutoroka.

Moshi. Mtanzania anayeishi Afrika Kusini, Jackson Ngalya amejitokeza mahakamani na kueleza kuwa gari aina ya Toyota Landcruiser V8 lenye nambaT888 BTY lililotaifishwa baada ya kukamatwa na wahamiaji haramu mkoani Kilimanjaro ni mali yake.

Kesi hiyo ilitajwa Ijumaa Agosti 23, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Opotuna Kipeta na kuahirishwa hadi Septemba 5, 2024 maombi hayo ya kurejeshewa gari yatakaposikilizwa.

Tangu kukamatwa kwa gari hilo Juni 4, 2024 eneo la Njipanda ya Himo, hakuna mtu aliyejitokeza kudai kuwa mmiliki wa gari hilo na Julai 2, 2024 Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, ilitoa amri ya kulitaifisha gari hilo na kuwa mali ya Serikali.

Gari hilo ambalo taarifa za awali zilieleza hadi linakamatwa, rekodi yake katika vyombo mbalimbali vya kiserikali na vya kiuchunguzi, zilizonyesha umiliki wake ulikuwa unasoma jina la mbunge mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani.

Kulingana na taarifa hizo, gari hilo liliingizwa na kusajiliwa nchini mwaka 2011 na rekodi hizo zinaonyesha Juni 24,2024 ikiwa ni baada ya siku 20 tangu lilipokamatwa, umiliki wa gari hilo ulibadilika na kuwa mali ya Ngalya anayeishi Afrika Kusini.

Hata hivyo, Mtanzania huyo amejitokeza na kueleza kuwa gari hilo ni mali yake na kwa kuwa anaishi Afrika Kusini, aliliacha nyumbani kwake hapa Tanzania likiwa mikononi mwa walinzi, hadi Juni 2024 alipojulishwa kuwa gari hilo lilikuwa halionekani.

Ameyaeleza hayo katika maombi aliyoyawasilisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ambayo yatasikilizwa Septemba 5, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi, Opotuna Kipeta, akiomba arejeshewe gari lake huku akijiweka kando na uhalifu uliotendeka.


Alichokieleza kwenye kiapo

Katika maombi hayo dhidi Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kama mjibu maombi wa kwanza na raia 7 wa Ethiopia waliokuwa wakisafirishwa na gari hilo, kama wajibu maombi wa 2 hadi wa 8, Ngalya anasema yeye ndio mmiliki halali wa gari husika.

Ngalya anaeleza katika kiapo chake kuwa kuanzia mwaka 2016 hadi sasa, amekuwa akiishi Afrika Kusini na aliliacha gari hilo chini ya uangalizi wa walinzi na ameambatanisha viza na hati yake ya kusafiria kuthibitisha anachokisema.

Kwa mujibu wa mleta maombi huyo, Juni 2024, alijulishwa kuwa gari hilo lilikuwa halijulikani lililo na kuwa Juni 3, 2024 alikwenda Kituo cha Polisi cha Oysterbay Dar es Salaam na kutoa taarifa juu ya gari lake hilo.

Baada ya hapo, ameeleza kuwa kupitia vyombo vya habari, alikuja kugundua kuwa gari lake hilo lilihusika katika usafirishaji wa wahamiaji haramu na linashikiliwa kuhusiana na kesi ya jinai 16397 ya 2024 iliyokuwa ikiwakabili wahamiaji hao.

Kulingana na maelezo hayo, anadai alikuja kushangaa baada ya ufuatiliaji na kubaini kuwa limehusika katika kesi hiyo ya jinai na kusisitiza kuwa gari hilo ni mali yake na hana ufahamu wa aina yoyote na jinai ambayo ilitendwa na watuhumiwa.


Gari lilivyokamatwa, kutaifishwa

Baada ya gari hilo kukamatwa, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga alisimulia namna wahamiaji hao walivyokamatwa wakiwa katika gari hilo na kuwa dereva aliyekuwa akiliendesha alifanikiwa kutoroka.

"Jana (Juni 4, 2024), tukiwa kwenye majukumu yetu ya kazi maeneo ya Himo tulikamata raia saba wa Ethiopia waliokuwa wakielekea Afrika Kusini. Tunaendelea na taratibu za uchunguzi na baadaye kuwafikisha mahakamani," alieleza Nyakunga.

"Mpaka sasa tunaendelea na uchunguzi kufahamu mmiliki wa gari ni nani, kwani dereva alikimbia na kwa mujibu wa sheria za nchi gari hilo likibainika kutumika kusafirisha wahamiaji haramu, litakuja kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali," aliongeza.

Wahamiaji hao walifikishwa kortini Juni 14, 2024 na kusomewa mashtaka mawili na Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya mashitaka (NPS), Issack Mangunu, ambapo walikiri kutenda makosa hayo ya jinai.

Washtakiwa hao ni Tensa Matwis, Abi Arose, Buruk Helobo, Arigudo Aromo, Sisy Abera, Mirhetu Sulore na Sharifan Betiso na usikilizwaji wa awali ukawa umepangwa Julai 2,2024.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa Juni 4, 2024 huko Njiapanda katika Wilaya ya Moshi, washtakiwa hao wakiwa raia wa Ethiopia, waliingia nchini kinyume cha sheria wakitumia gari lenye namba za usajili T888 aina ya Toyota Land Cruiser.

Katika kosa la pili, ilidaiwa kuwa siku hiyo hiyo katika eneo hilo hilo, washtakiwa walikutwa kinyume cha sheria wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania bila kuwa na hati halali za kusafiria au nyaraka yoyote ya kisheria inayowaruhusu kukaa nchini.

Julai 2, 2024, Hakimu Mkazi, Rehema Olambo aliwahukumu raia hao wa Ethiopia kulipa faini ya Sh500, 000 kila mmoja au kwenda jela mwaka mmoja na wote walishindwa kulipa faini hiyo na kupelekwa gerezani.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Agatha Pima, aliiomba mahakama itoe amri ya kutaifishwa kwa gari lililotumika kuwasafirisha, ombi ambalo mahakama ililikubali na kutoa amri hiyo.