Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtikila alivyoanzisha mapambano kudai wagombea binafsi (1)

Mtikila alivyoanzisha mapambano kudai wagombea binafsi (1)

Muktasari:

  • Ingawa amefariki takriban miaka sita iliyopita, mbegu aliyopanda mwanasiasa machachari na aliyekuwa kiongozi wa Kanisa la Full Salvation Church, Christopeher Mtikila, ya kutaka Mtanzania yeyote mwenye nia ya kugombea nafasi ya kisiasa awe huru kufanya hivyo bila kulazimika kupitishwa na chama cha siasa, bado haijafa.

Ingawa amefariki takriban miaka sita iliyopita, mbegu aliyopanda mwanasiasa machachari na aliyekuwa kiongozi wa Kanisa la Full Salvation Church, Christopeher Mtikila, ya kutaka Mtanzania yeyote mwenye nia ya kugombea nafasi ya kisiasa awe huru kufanya hivyo bila kulazimika kupitishwa na chama cha siasa, bado haijafa.

Mtikila, ambaye mara kadhaa majaji walimwelezea kama ‘mtu jasiri’, alianza mapambano ya kudai haki hiyo mwaka 1993, pale alipofungua kesi ya kihistoria katika Mahakama Kuu, Dodoma, akiomba itamke kuwa raia wa Tanzania wana haki ya kugombea nafasi ya urais, ubunge na udiwani bila kulazimika kujiunga na chama cha siasa.

Mtikila alishinda kesi kupitia hukumu iliyotolewa na Jaji Kahwa Lugakingira (marehemu) baada ya mnyukano mkali wa hoja za kisheria kati ya mawakili wa Serikali na wale waliomwakilisha mwanasiasa huyo.

Serikali haikuridhishwa na kukata rufaa dhidi ya uamuzi, labda kwa kujua kuwa rufaa hiyo ingepata ugumu kushinda, iliamua kuiondoa mahakamani na kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria bungeni yaliyozuia raia kugombea nafasi ya kisiasa kama mgombea binafsi.

Katika kesi yake, Mtikila alikuwa akipinga, katazo la wagombea binafsi kugombea urais, ubunge na udiwani lililoletwa na Sheria ya Mabadiliko ya Nane ya Katiba ya mwaka 1992.

Mabadiliko hayo yaliifumua na kuibadili Ibara ya 39 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo awali iliainisha kuwa:-

(a) Hakuna mtu atakayekidhi kugombea nafasi ya urais wa Tanzania isipokuwa awe amefikisha miaka 40 .

(b) Kwamba, lazima awe anakidhi vigezo vya kuchaguliwa kuwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (Zanzibar).

Mabadiliko hayo ya nane yaliibakisha aya (a) na (b) lakini ikazipa herufi mpya za (b) na (d) na kuongeza aya (a) na (c) zilizotamka:

(a) Ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa.

(b) Ni mwanachama wa chama cha siasa na awe amedhaminiwa na chama cha siasa.

Takwa hilo kuwa mwanachama wa chama cha siasa na kudhaminiwa na chama cha siasa ilihusisha pia uchaguzi wa wabunge, chini ya Ibara ya 67 na 77 ya Katiba ya Tanzania na chaguzi za serikali za mtaa chini ya kifungu cha 39 Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, 1979.

Hoja ya Mtikila iliyokuwa mezani kwa Jaji Lugakingira ni kwamba sharti la kutaka raia wa Tanzania anayetaka kuwania nafasi ya uongozi wa kisiasa lazima apitie na kufadhiliwa na chama cha siasa, ilikiuka haki ya raia kushiriki katika masuala ya kitaifa ya umma kama inavyoelezwa katika Ibara ya 21 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Takwa hilo la kupitia na kufadhiliwa na chama cha siasa ili kugombea nafasi ya kisiasa inahusisha pia uchaguzi wa wabunge chini ya Ibara ya 67 na 77 na pia chaguzi za Serikali za mitaa chini ya kifungu cha 39 cha Sheria ya uchaguzi ya Mamlaka za Mitaa ya mwaka 1979.

Ibara ya 21 (1) inatamka kuwa bila kuathiri masharti ya ibara ya 5, ya 39 na ya 67 ya katiba na ya sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.

Akionyesha kuguswa na hoja za mpambano kati ya Serikali na Mtikila, Jaji Lugakingira alihitimisha hukumu yake kwa kutamka:

“Kwa kila kitu nilichokielezea na bila kujali mambo ya kipekee yanayotokana na Ibara ya 39, 67 na 77 ya Katiba pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mtaa, natamka na kuelekeza kwamba itakuwa na halali kisheria kwa wagombea binafsi, pamoja na wagombea wanaofadhiliwa na vyama vya siasa, kugombea urais, ubunge na chaguzi za serikali za mitaa.”

Jaji Lugakingira alikwepa kutamka kuwa baadhi ya vifungu vya katiba, kama alivyoeleza Mtikila kwenye maombi yake, yalikuwa kinyume na katiba licha ya kuwa aliombwa kufanya hivyo.

Baada ya hukumu hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye ndiye mshauri mkuu wa Serikali wa masuala ya kisheria alifanya mambo mawili kwa wakati mmoja.

Kwanza, alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani na wakati huo huo akapeleka bungeni Sheria ya Mabadiliko ya Saba ya Katiba namba 34 ya mwaka 1994 ambayo madhara yake yalikuwa ni kutengua tamko na maelekezo ya Jaji Lugakingira na kuuendeleza msimamo ya katiba wa kuzuia wagombea binafsi kushiriki uchaguzi.

Kabla ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Ibara ya 21 (1) ilikuwa ikitamka kuwa: “Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupita wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.”

Kufuatia mabadiliko hayo, Ibara hiyo ndogo ilisomeka karibu vilevile isipokuwa iliwekewa maneno ya utangulizi kama ifuatavyo:

“Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 39, 47 na 67 ya Katiba hii na ya sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, kila raia…

Wakati akifungua kesi ya kutaka wagombea binafsi waruhusiwe kushiriki chaguzi za kisiasa, Mtikila alikuwa bado anahangaika kusajili chama chake cha Democratic Party (DP).

Baada ya kupata usajili wa chama chake, Mtikila alikimbilia tena Mahakama Kuu, zamu hii akifungua kesi ya kupinga Sheria ya Mabadiliko ya Saba ya Katiba.

Katika kesi hiyo aliyoifungua mwaka 2005, mwanasiasa huyo ‘jeuri’ aliiomba mahakama itamke kuwa mabadiliko ya katiba ya kifungu cha 39 na 67 yaliyoletwa na Sheria namba 34 ya 1994 yalikuwa kinyume cha katiba.

Aliiomba pia, Mahakama itamke kuwa yeye (Mtikila) anayo haki ya kikatiba chini ya Ibara ya 2 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kugombea nafasi ya urais, ubunge kama mgombea binafsi. Msingi wa malalamiko ya Mtikila yalikuwa kwamba mabadiliko hayo ya katiba yalikiuka haki za msingi za binadamu kama zilivyotamkwa katika Ibara ya 21 (1) ya Katiba.

Pili, alidai mabadiliko hayo ya katiba yalikiuka Ibara ya 9 (a) na (f) ya Katiba na pia yalikiuka Ibara ya 20 (4). Pia, alidai kuwa mabadiliko hayo yalikiuka makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za binadamu ambayo Tanzania ilikuwa imeyaridhia.

Kwa mujibu wa Mtikila, madhara ya jumla ya mabadiliko hayo ni kwamba yalikuwa yakimlazimisha mwananchi wa kawaida kujiunga na chama cha siasa ili apate kibali cha kushiriki shughuli za utawala wa nchi yake na ili aweze kuchaguliwa kuwa rais au mbunge.

Katika mfululizo wa mapitio ya kesi za kutaka wagombea binafsi waruhusiwe kugombea urais, ubunge na udiwani, tutaona jinsi Mwanasheria Mkuu wa Serikali alivyopambana kupinga kesi hiyo.

Itaendelea kesho