Mtoto afariki kwa kugongwa na gari

Friday June 24 2022
mtotopiic
By Suzy Butondo

Shinyanga. Mwanafunzi wa shule ya msingi Samuu iliyopo katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga, Godlight Chisawilo (4) amefariki dunia baada ya kugongwa na gari aina ya Coasta katika Mtaa wa Majengo Mapya

Akizungumzia tukio hilo, kamanda wa polisi mkoani wa Shinyanga, George Kyando amesema ajali hiyo imetokea juzi Jumanne, Juni 21, 2022 saa 12 jioni ambapo gari hilo lilikuwa likitokea Shule ya ya Msingi Samuu na kuelekea majengo mapya likiwa limebeba wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Godlight ambaye alikuwa akisoma darasa la awali katika shule hiyo.

Kyando amesema baada ya kipindi cha masomo kwisha, mtoto huyo alipanda gari pamoja na wanafunzi wenzake baada ya kufika Mtaa wa Majengo mapya anakoishi, Godlight alishuka na kuvuka barabara ambapo dereva wa gari hilo Kassim Said (40) alimgonga na kumsababishia kifo papo hapo.

“Natoa wito kwa madereva wote kuchukua tahadhari kwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima,” amesema Kyando.

Kamanda huyo amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kutochukua tahadhali kwa watumiaji wengine wa barabara na kutokana na kosa hilo tayari amekamatwa kwa maelezo zaidi na taratibu za kisheria zinaendelea.

Advertisement