Mtoto aliyechomwa moto na mama yake afariki dunia
Muktasari:
- Mtoto Shamsudini Jamadu Msemo (13) aliyemwagiwa mafuta ya taa na kisha kutiwa kiberiti na mama yake mzazi amefariki dunia katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini (KCMC) alikokuwa akipatiwa matibabu.
Moshi. Mtoto Shamsudini Jamadu Msemo (13), aliyemwagiwa mafuta ya taa na kisha kuchomwa kiberiti na mama yake mzazi, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) alikokuwa akipatiwa matibabu.
Agosti 31, mwaka huu mtoto huyo ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Reli Juu, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, alidaiwa kufanyiwa ukatili huo baada ya kuchukua fedha za mama yake na kwenda kununua viazi vya chipsi na kisha kupika na kula wakati alipohisi njaa.
Inadaiwa kuwa, baada ya mama yake kubaini mwanaye huyo amechukua fedha zake, alimfunga mikono na miguu kwenye mti ambao upo nyumbani kwao na kisha kumuagiza mtoto wa jirani kwenda kununua mafuta ya taa na ndipo alipotenda tukio hilo la kikatili.
Ikiwa zimapita siku 34 tangu mtoto huyo afanyiwe ukatili huo na mama yake mzazi, mpaka sasa hajulikani alipo huku Jeshi la Polisi likiendelea kumsaka bila mafanikio.
Hata hivyo, baada ya mtoto huyo kufikishwa katika Hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu, wataalam wa majanga ya moto hospitalini hapo walibaini kuwa mwili wa mtoto huyo uliungua kwa asimilia 65 kutokana na majeraha ya moto aliyopata.
Akithibitisha kufariki kwa mtoto huyo, Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Gabriel Chisseo amesema Shamsudini amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Oktoba 3, 2023 wakati jopo la madaktari likiendelea kupambania uhai wake.
"Sisi kama hospitali kitengo chetu cha majanga ya moto tunasikitika baada ya kijana tuliyempokea akiwa na majeraha ya kuungua moto kufariki leo, hali yake ilibadilika jana usiku hivyo Madaktari wetu walipambana lakini kwa mapenzi ya Mungu akawa amefariki,"
"Hospitali inatoa pole kwa familia na Watanzania walioonyesha kuguswa na huyu kijana kwa namna ambavyo alipata hili tatizo la kuungua moto...ni tukio ambalo limemgusa kila mtu, wataalam wetu walipambana kadri wawezavyo na alikuwa anaendelea vizuri sana, aliweza kutoka ICU na kwenda wodi ya kawaida lakini baadaye hali ilibadilika," amesema na kuongeza;
"Kama hospitali tumepatwa na hali ya majonzi kwa sababu wataalam walijitoa kwa kila namna kuhakikisha huyu mtoto anapona na anarejea katika hali yake ya kawaida... yote ni mapenzi ya Mungu."
Awali alipotafutwa baba mzazi wa mtoto huyo, Jamadu Msemo alisema taarifa alizozipta kutoka kwa majirani ni kwamba mke wake huyo aliamua kufanya kitendo hicho kwa madai kuwa mwanaye huyo alimchukulia mama yake Sh20,000.