Mume, mke mbaroni wakidaiwa kumficha mtoto wa jirani

Muktasari:
- Kaimu kamanda polisi Mkoa wa Songwe, Gallus Hyera amesema tukio hilo limetokea Januari 29, 2024.
Songwe. Jeshi la Polisi mkoani Songwe linawashikilia mume na mke kwa tuhuma za kumficha mtoto ambaye mwanafunzi katika shule ya msingi Hollywood iliyoko katika mji mdogo wa Mlowo wilayani Mbozi, mkoani Songwe.
Kaimu kamanda wa polisi mkoani humo, Gallus Hyera amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake leo Februari mosi, 2024 kuwa tukio hilo limetokea Januari 29, 2024.
Amesema mtoto huyo wa kike (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka minane, siku ya tukio akiwa anatoka shuleni akiwa na rafiki, walifika nyumbani kwa watuhumiwa ambao ni wazazi wa rafiki wa mtoto huyo na hakurudi nyumbani kwao.
Kamanda Hyera amesema wazazi wa mtoto huyo anayesoma darasa la tatu, walitoa taatifa ya kupotea kwa mtoto wao na uchunguzi ulipoanza walimkuta nyumbani kwa watuhumiwa akiwa amefichwa chumbani akiwa amefunikwa blanketi, ili asionekane.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha mtoto huyo aliogopa kurudi nyumbani akihofia kuchapwa na wazazi baada ya kuchelewa na kutoenda nyumbani, hivyo kufichwa na rafiki yake,” amesema kaimu kamanda Hyera.