Muswada Bima ya Afya kwa wote waahirishwa bungeni

Muktasari:

 Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ambao ulikuwa ujadiliwe bungeni leo Ijumaa na kukamilisha hatua zote tatu, umeahirishwa hadi hapo mashauriano kati ya Bunge na Serikali yatakapokamilika.


Dodoma. Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ambao ulikuwa ujadiliwe bungeni leo Ijumaa na kukamilisha hatua zote tatu, umeahirishwa hadi hapo mashauriano kati ya Bunge na Serikali yatakapokamilika.

Akizungumza leo Novemba 11, 2022 Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kuna mambo ambayo hawajaafikiana na Serikali hivyo umeondolewa katika ratiba ya shughuli za leo ambapo Bunge linaahirishwa.

Amesema katika orodha ya shughuli za Bunge za leo kulikuwa na hati za kuwasilishwa mezani na kwamba hati hizo zilitakiwa kuwasilishwa na Waziri wa Afya  na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

“Sasa hati hii haitawasilishwa leo mezani kwasababu Bunge pamoja na Serikali tunaendelea na mashauriano juu ya mambo ambayo hatujaafikiana vizuri,”amesema.

Amesema Bunge hilo halitautazama muswada huo tena ambao kwa mara ya kwanza ulisomwa katika mkutano uliopita na kupelekwa kwa kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Amesema kwa ratiba muswada huo ulikuwa uingie leo bungeni leo kwa ajili ya mjadala na kumaliza kazi ya kuitunga sheria.

Amesema wanaendelea na mashauriano katika hoja kadhaa ambazo zimeibuliwa na wabunge, wadau mbalimbali waliojitokeza katika kamati na nyingine Serikali inaendelea kuzitazama namna bora ya kuwahudumia kwenye eneo hili la Bima ya Afya kwa Wote.

Amesema muswada huo utapelekwa bungeni mara watakapokuwa wameshakamilisha mashauriano hayo.

Muswada huo uliwasilishwa bungeni katika mkutano wa Bunge wa nane uliofanyika Septemba mwaka huu,  baada ya kuahirishwa kwa miaka kadhaa.

Kuwasilishwa kwake kulikuja baada ya tamko la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Septemba 11, 2022 wakati akiwa katika Jublee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata).