Mvua  ilivyoacha maumivu mmoja adaiwa kufa Dar

Muktasari:

Miongoni mwa athari iliyosababishwa na mafuriko ni kusombwa kwa mali, uharibifu ikiwemo wa magari ambayo mengine yalisombwa na maji, makazi kujaa maji na kuezuliwa mapaa, miundombinu kuharibiwa kama madaraja na barabara kukatika. 

Dar es Salaam. Mvua kubwa iliyoambana na upepo mkali iliyonyesha kwa saa sita kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa nne asubuhi ya leo Jumamosi, Januari 20, 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, imeacha maumivu kwa wakazi wa mkoa huo, huku mkazi mtu mmoja akidaiwa kupoteza maisha katika eneo la Mbezi Aficana.

Miongoni mwa athari iliyosababishwa na mafuriko ni kusombwa kwa mali, uharibifu ikiwemo wa magari ambayo mengine yalisombwa na maji, makazi kujaa maji na kuezuliwa mapaa, miundombinu kuharibiwa kama madaraja na barabara kukatika. 

Pia, miundombinu ya umeme na mawasiliano nayo ilikutana na changamoto hiyo kwa nguzo kusombwa na maji hivyo kusababisha baadhi ya maeneo huduma hiyo kutokuwapo kwa saa kadhaa.


Maeneo yaliyokatika mawasiliano, ni Daraja la Kunduchi kwenda Bahari Beach, Daraja la Panga Boyi mtaa wa Mbopo Kata ya Mabwepande, Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani. 

Kukatika kwa mawasiliano Jangwani, kumesababisha wasafiri wa mabasi ya mwendo haraka hususan wanaotokea Kimara kwenda maeneo ya Kariakoo na Posta kushushwa eneo la Magomeni wakielezwa safari inaishia hapo.

Mwananchi imetembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kujionea namna wananchi mbalimbali wakinusuru mali zao kwenye maji wengine wakiondoa vitu vyao vya thamani ndani ya nyumba zilizovamiwa na maji.

Kilio zaidi ni kwa wakazi waliojenga karibu na mito kwani mbali na nyumba kubomoka viwanja vyao viligeuka madimbwi ya maji huku mali zao zote zikibebwa na maji.


Katika taarifa kwa umma ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) iliyotolewa leo Jumamosi imetoa tahadhari ya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na visiwa vya Unguja na Pemba zinazotarajiwa kunyesha kesho Jumapili.

Pia, TMA imetabiri mvua kama hizo Jumatatu ya Januari 22, 2024 kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Njombe na Ruvuma.

TMA imetoa angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili kwa maeneo ya ukanda wa Pwani ya bahari ya Hindi (mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Tanga na Pwani.

Licha ya kutothibitishwa na Jeshi la Polisi, ilidaiwa mtu mmoja alifariki eneo la  Mbezi African. Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Kamugisha Makwinya alisema kijana huyo ambaye jina lake halikufahamika alisema alikuwa akivuka kando ya barabara yalimsomba. 

Makwinya alisema kijana huyo alikuwa anatokea Mbezi African akafika eneo la Juliana ambapo walimzuia asipite kando ya barabara kuna maji mengi lakini hakusikiliza na alipoendelea maji yalimchota.


Walichokisema Polisi, RC Chalamila

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salam, Jumanne Muliro akizungumza na Mwananchi Digital amesema: “maeneo yaliyoathirika tumechukua hatua ya tahathari ya  kuweka vizuizi watu wasipite hadi maji yatakapopungua.Kuhusu vifo ni mapema kueleza kama kuna matukio hayo kwa kuwa bado tunafuatilia kwa karibu hali ilivyo.’’

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila katika mapokezi ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi kushughulikia changamoto za mafuriko yaliyotokea katika jiji hilo kabla ya Nchimbi kugusia jambo hilo akitaka hatua zifanyike kwa haraka.

“Namshukuru kutoa ahadi aliyoitoa ya kushughulikia changamoto za mafuriko zilizotokea katika maeneo mbalimbali ya mkoa wake. Nilikusudia kumwomba afanye kazi kwa haraka kiongozi makini hasubiri maelekezo,’’ amesema Dk Nchimbi 

Mbunge wa Mbagala (CCM), Abdallah Chaurembo akizungumza na Mwananchi Digital amesema kwa jimbo lake wananchi wengi wameumia na miundombinu ya barabara imeharibika kwa kiwango kikubwa.

“Mabati yameezuliwa na barabara hazipitiki hivyo mvua hii imeleta athari kubwa kwa wananchi,” amesema

Tanroads mguu sawa

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta baada ya kufika na kukagua miundombinu iliyoathirika katika daraja linalounganisha Kunduchi - Bahari Beach – Ununio na maeneo ya Jirani alisema:-

“Mazingira ya dharura yanahitaji hatua za dharura na sisi tumejipanga kwamba pale inapotokea dharura tunakuwa tumeshajitayarisha na kabla dharura haijatokea tunakuwa tunachukua hatua za awali.’’

Alitolea mfano kusafisha na kuondoa udongo kwenye makalvati na madaraja na kuufanya mto usipoteze njia na hivyo kuathiri miundombinu hiyo.


‘’Hizo ni moja wapo hatua za dharura tunazochukua katika kipindi hiki cha mvua za El-nino,’’ amesema


Kilio cha wananchi, mwanamke asombwa

Shaban Manamba, mkazi wa Tegeta darajani amesema alfajiri saa 11 alisikia mvua na baada ya muda mfupi maji yalianza kumuingilia ndani jambo ambalo hakuwahi kulishuhudia.

“Tulikimbia nje kuangalia mazingira yakoje, mimi nimefanikiwa kuokoa mali zangu, kwengine nilipata taarifa jirani yetu mmoja na mwanawe wamesombwa na maji japo mtoto aliokolewa,” amesema Manamba akibainisha wanaendelea kumtafuta mama huyo 

“Kwa eneo hili la Tegeta darajani kulikuwa na nyumba za kulala wageni na ukumbi lakini zote zimevunjwa na maji,” amesema.

Veronika Simon, mjane na mkazi wa Tegeta amesema kwa sasa hana makazi ya kuishi na watoto wake watatu baada ya mvua kusomba nyumba yake.

Mama huyo amesema alianza kusikia upepo mkali na alipotoka nje hakukuwa na dalili za kunyesha mvua kubwa lakini baada ya muda mfupi mvua kubwa ilianza kunyesha.


“Niliposikia radi na mvua kubwa nilitoka kwa mara nyingine na niliona mto umejaa, niliingia ndani na kuwachukua watoto wangu na kuondoka katika eneo hili, sikuona nyumba yangu tena wala mali zangu sijui nitaishi wapi mume wangu alifariki mwaka jana,” amesema.

Simulizi zao zinafanana na ya Joyce Mbikilwa, mkazi wa Tegeta Azania aliyesema maisha ya kuingiliwa na maji ndani hawajapendi bali ni hali ngumu ya maisha ndiyo inayowasukuma kukimbilia maeneo yanayouzwa kwa gharama ndogo.


Kutokana na mkasa huo, Joyce amewatupia lawama viongozi wanaomiliki maeneo makubwa ndani ya Wilaya ya Kinondoni akisema hakuna uendelezaji wa maeneo hayo huku wananchi wakipata tabu na wanapochukua hatua ya kwenda kujenga huitwa wavamizi.

“Kuna viongozi wana maeneo makubwa na hawaendelezi watu wakienda kujenga  wanaambiwa wamevamia sasa kama wanatumikia wananchi kwa nini wasiwape wananchi waishi,” amesema. 

Joyce alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan awaangalie viongozi hao wanaomiliki maeneo makubwa ili wananchi wapate nafasi ya kuishi bila mateso.

Kwa upande wa Mbezi Beach chini mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda cha kufyatulia matofali ambacho kiliathiriwa na maji Mohamed John alisema zaidi ya tofali 6,000 zimeharibika.

“Hayo matofali mengine yamepasuka na mengine kwenda na maji, tunakofyatulia hapa lakini maji yamekuja kwa nguvu na kufanya uharibifu huu mkubwa wa matofali na mashine nne za kufyatulia,” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitonga, Bakari Kanyongo alisema katika mtaa wake nyumba 10 zimeezuliwa mapaa.

“Hii mvua ni kubwa sana imeezua mabati na tayari tumetafuta mafundi kwa ajili ya kufanya ukarabati na wakazi wangu wapo nje,” amesema.


Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbopo kata ya Mabwepande alisema mvua hizo zimeharibu daraja la Panga boyi.

“Lipo eneo linguine linaitwa Kidogoya, Kasumuni na kwa bichi huku kote kumeharibika kutokana na mvua iliyonyesha,” amesema.

 Kwa upande wa usafiri, Mkazi wa Kimara, Aisha Salehe ameiambia Mwananchi Digital  wamepanda usafiri huo wa haraka  kuanzia  Kimara na walipofika maeneo ya Jangwani waliambiwa na dereva kuwa gari hilo haliwezi kwenda Kariakoo kutokana na mafuriko yaliyopo eneo la Jangwani.

"Nipo hapa Jangwani nasubiria maji yapungue kidogo Ili niende Kariakoo kwa ajili ya kufanya biashara maisha yangu nategemewa niuze nguo ili familia yangu iweze kula na maisha yasonge mbele," amesema.

…nyumba 15, hekari 20 zaharibiwa


Wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, zaidi ya nyumba 15 na ekari 20 za migomba ya ndizi, kahawa na mahindi ziliharibiwa na upepo mkubwa ulioambatana na mvua ya mawe.


Mvua hiyo ya mawe iliyodumu kwa zaidi ya saa moja  ilileta athari kubwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ambapo kitongoji kimoja cha Marukeni, kilichopo kata ya Machame Kaskazini kiliathiriwa vibaya na mvua hizo huku zikiachwa wananchi bila mazao.


Mwandishi wa gazeti hili, alifika katika kitongoji hicho na kushuhudia mashamba makubwa ya mazao ya ndizi, kahawa na mahindi yakiwa yamelala chini baada ya kuangushwa na upepo mkali uliosababishwa na mvua hizo.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Nshara, Laurence  Swai amesema mvua hizo zilizoanza kunyesha muda wa saa tisa alasiri na kudumu kwa saa moja zilisababisha madhara makubwa ikiwemo migomba yenye ndizi, kahawa, mahindi  kuangushwa chini huku nyumba zikiangukiwa na miti mikubwa na kuharibu makazi ya watu.


"Jana ilinyesha mvua kubwa ya mawe ambayo iliambatana na upepo mkali ambao uliangusha miti, migomba ya ndizi na miti, kahawa pamoja na miti mikubwa ambayo iliangukia kwenye nyumba za makazi ya wananchi na kuleta madhara makubwa," alisema


"Nyumba zaidi ya 15 katika Kijiji changu zimeangukiwa na miti mikubwa pamoja na mashamba ya migomba yote imelala chini katika kitongoji cha Maruweni kutokana na mvua kubwa na upepo mkali, ambao ulidumu kwa zaidi ya saa moja," amesema


Naye Manase Nkya, mmoja wa wananchi wa kitongoji cha Maruweni alisema shamba lake la migomba ya ndizi na kahawa lenye ukubwa wa ekari nne limeathiriwa na mvua hizo ambapo mazao yake yote yamelala chini kwa kuangushwa na mvua hizo za mawe zilizoambatana na upepo mkali.


Imeandikwa na Baraka Loshilaa na Pamela Cholongola (Dar) na Janeth Joseph (Moshi)