Mwakyembe: Kitabu kimesahihisha mambo yaliyopindishwa

Muktasari:
- Kiongozi wa jopo lililoandika Kitabu cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Dk Harrison Mwakyembe amesema kitabu hicho kinasahihisha mambo yaliyopindishwa kuhusu muungano huo.
Dodoma. Kiongozi wa jopo lililoandika Kitabu cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Dk Harrison Mwakyembe amesema kitabu hicho kinasahihisha mambo yaliyopindishwa kuhusu muungano huo.
Dk Mwakyembe ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 26, 2022 wakati wa sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanzania.
Amesema uandaji wa kitabu hicho ni ubunifu wa ofisi ya Makamu wa Rais na Makamu wa pili wa Rais Zanzibar kwa lengo la kuelimisha na kusambaza elimu sahihi kwa umma ambayo ni tunu ya Taifa.
Amesema ingawa kuna machapisho mengi yaliyotolewa na Ofisi hiyo lakini chapisho hilo linautofauti na zilizotangulia.
“Mbali na mafanikio, kitabu hiki kimeelezea misingi ya muungano imara na si kwa kunukuu mifano kutoka nchi nyingine bali kwa kuangalia uzoefu walionao.
“Tunasahihisha mambo mengi yanayopindishwa pindishwa kusimulia Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 na muungano wetu. Tunasahihisha hayo katika kitabu hiki,”amesema.