Mwalimu wa hisabati jela maisha kwa kulawiti mwanafunzi

Muktasari:
Mahakama ya Rufani imebariki kifungo cha maisha alichohukumiwa mwalimu wa Shule ya Msingi Chomvu iliyopo Wilaya ya Mwanga, Elibariki Mchomvu kwa kulawiti mwanafunzi wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa.
Moshi. Mahakama ya Rufani imebariki kifungo cha maisha alichohukumiwa mwalimu wa Shule ya Msingi Chomvu iliyopo Wilaya ya Mwanga, Elibariki Mchomvu kwa kulawiti mwanafunzi wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa.
Mchomvu, aliyekuwa akifundisha hisabati, alipatikana na hatia kwa mara ya kwanza mwaka 2019 ya kumlawiti mwanafunzi huyo chooni na kuhukumiwa na hakimu mkazi Mwanga, Mariam Lusewa kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo, mwaka huohuo akakata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi kupinga adhabu hiyo, lakini Jaji Susan Mkapa si tu kwamba alitupilia mbali sababu zake za rufaa, lakini aliongeza adhabu na kuwa kifungo cha maisha. Hakuridhika na kukata tena rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania, jopo la majaji watatu walitoa hukumu na kubariki kifungo hicho cha maisha jela.
Mfungwa huyo aliwasilisha hoja 10 kupinga kutiwa hatiani na adhabu ambazo hata hivyo zilipanguliwa na upande wa jamhuri ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Verdiana Mlenza aliyesaidiana na wakili Sabitina Mcharo.
Katika hukumu yao iliyotolewa wiki iliyopita na nakala ya hukumu kupatikana jana,majaji hao, Dk Gerald Ndika, Ignas Kitusi na Omar Makungu walisema sababu za rufaa hazikuwa na mashiko na kubariki adhabu hiyo.
“Kwa kuzingatia kuwa mlalamikaji alikuwa na umri wa miaka tisa wakati wa tukio, Mahakama Kuu Moshi ilikuwa sawa kuingilia kati na kutoa kifungo sahihi cha maisha jela,” inasema hukumu hiyo.
Tukio lilivyofanyikia chooni
Kwa mujibu wa ushahidi uliopo katika mwenendo wa shauri hilo, siku ya tukio Julai 31, 2017 katika Shule ya Msingi Chomvu, mtoto huyo aliyekuwa mwafunzi wa darasa la tatu, alikwenda chooni kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo.
Wakati huo ilikuwa saa 5:00 asubuhi, mwalimu huyo (mshtakiwa) naye aliingia katika choo hicho hicho na kumshika mtoto huyo kisha kumziba mdomo kwa kutumia mkono ili asiweze kupiga kelele, ambazo zingesikika nje ya choo.
Hapo ndipo ndipo alipomvua mtoto huyo kaptula yake, kisha kumuingilia huku mtoto huyo akipata maumivu makali. “Nilitembea polepole kurudi nyumbani nikiwa na maumivu na nilikuwa natokwa na damu. Mshitakiwa aliniambia kama nitasema aliniingilia ataniua na kwamba niseme (damu) ilitokana na kuanguka,” sehemu ya ushahidi wa mtoto.