Mwanafunzi ataka kujiua akidaiwa kumeza vidonge 21

Wednesday August 04 2021
vidongepicc
By Jesse Mikofu

Zanzibar. Mwanafunzi wa darasa la tano wa shule ya msingi Chwale Mkoa wa Kaskazini Pemba amenusurika kifo baada ya kumeza vidonge 21 aina ya Panadol.

Kaimu kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Jerome Ngowi amesema hayo leo Jumatano Agosti 4, 2021 kwamba sababu za mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 14 kutaka kujiua bado hazijafahamika.

"Mtoto huyu analelewa na shangazi yake ambaye alimwomba kwa wazazi wake ili aishi naye lakini inaonekana mwenendo wake haukuwa mzuri," amesema

Ngowi amesema tukio hilo lilitokea Agosti 2, wilayani Wete baada ya mtoto huyo kutakiwa kwenda shule lakini akaenda kuvua samaki aina ya kambale na alipotoka huko alinunua vidonge hivyo 21 kisha akavimeza vyote.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda Ngowi, mwanafunzi huyo alipomeza vidonge hivyo alidondoka chini akazimia ndipo alipobebwa na wasamaria wema akapelekwa katika hospitali ya wilaya ya Wete kwa ajili ya matibabu.

"Tunaendelea na upelelezi kujua kwanini alimeza vidonge hivi, lakini uchunguzi wa awali unaonyesha mtoto huyo alikuwa mtundu sana na hakupenda kwenda shule wala madrasa," amesema

Advertisement

Amewataka wazazi kuacha kukwepa majukumu yao akisema 'malezi ya mtoto ni jukumu la baba na mama, kama tumekubali kuzaa basi na kulea tukubali vilevile. Wazazi wa mwanafunzi huyu bado wapo kila mmoja anaishi kivyake lakini bado hawajatengana.

Advertisement