Mwanafunzi chuo kikuu autaka uspika

Muktasari:

  • Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) jijini Dar es Salaam amejitokeza katika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam akitaka kujua taratibu za kuchukua fomu za kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Dar es Salaam. Wakati hatua ya uchukuaji fomu za kuomba uteuzi wa kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania ikiwa imeingia siku ya tatu, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Amos Sollo (26) ajitokeza kuitaka nafasi hiyo.


Sollo amefika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam leo Jumatano Januari 12, 2022.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kutoka katika ofisi hizo, Sollo amesema yeye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu chuoni hapo akisomea shahada ya uchumi na maendeleo na amefika ofisini hapo kujua utaratibu wa kupata fomu ukoje na kuambiwa kuwa gharama ni Sh1 milioni.


"Niliamua kufika hapa ofisi za chama kujua utaratibu wa kupata fomu ili nami nitie nia ya kugombea uspikana ndipo nikaambiwa ni Sh1 milioni.

" Lakini mpaka sasa nina Sh300,000  ambapo Sh100,000 nikiwa nayo taslimu na Sh200,000 ikiwa benki, hivyo naenda kuomba kwa wadau wengine wanichangie ili itimie niweze kuchukua fomu kwa kuwa nia na sifa ninazo za kukalia kiti hicho cha uspika na vijana tunaweza," amesema Sollo.

Akielezea uzoefu wake katika uongozi, amesema ameshawahi kuwa Mbunge Wizara ya Uchumi katika chuo hicho na pia amewahi kutia nia nafasi ya urais akiwa chuo cha Maswa na hivi karibuni kastafu Uenyekiti wa chama cha Wanafunzi wanaosomea uchumi chuoni hapo.