Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanafunzi kidato cha nne adaiwa kujinyonga hadi kufa

Alily Alphan (15) mwanafunzi kidato cha Nne Shule ya Sekondari Bakoba Manispaa ya Bukoba Mkoa Kagera Enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Aligunduliwa na mwenye nyumba aliyokuwa akiishi na wadogo zake wawili.

Bukoba. Alily Halphan (15), mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Bakoba, Manispaa ya Bukoba, Mkoa wa Kagera, anadaiwa kujinyonga hadi kufa akiwa chumbani kwake.

Inadaiwa Alily amejinyonga kwa  kutumia vipande viwili vya pazia na tukio hilo limetokea leo Jumatatu Juni 10, 2024 katika Mtaa wa Kafuti, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Maiti yake imegunduliwa saa tano asubuhi, chumbani alikokuwa akilala na wadogo zake wawili wa kike--- Rauswath (13) na Shani (12).

Akizungumzia tukio hilo, Mjumbe wa Serikali za Mtaa wa Kata ya Bakoba, Stevin Lupapulo, amesema alipokea simu kutoka kwa Faraj Mgaye (mwenye nyumba) akimuarifu kuhusu tukio hilo.

Baada ya kufika, walishirikiana kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na kata, kisha polisi walifika na kuvunja mlango na wakamkuta Alily akiwa  amejinyonga kwa kutumia vipande viwili vya pazia alivyotengeneza kama kamba na kujitundika kwenye dari.

“Mwenye nyumba alikuwa anataka pasi aliyoazima mwanafunzi huyo, hivyo akagonga hodi bila kujibiwa maana mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani. Baada ya kugonga dirishani bila majibu, aliita uongozi na tukakuta Alily amejinyonga kwa kutumia vipande viwili vya pazia aliyochana,” amedai Lupapulo.

Mgaye amesema mtoto huyo alikuwa akiishi na wadogo zake wawili wa kike katika chumba kimoja alichopangiwa na baba yao baada ya kutengana na mama yao miaka 10 iliyopita.

“Asubuhi saa tano nilikuwa nyumbani nikimuita kumtaka anipatie pasi na ajiandae kwenda shule baada ya kuona amechelewa. Nilimchukulia kama mwanangu na imenishangaza kukuta amejinyonga,” amesema Mgaye.

Amesema watoto hao walikuwa wakiishi bila mzazi yeyote, baba yao alikuwa amewapangia chumba kimoja baada ya kutengana na mama yao.

Rauswath, mdogo wa marehemu Alily, amedai kwamba kaka yake amejinyonga baada ya kutokea ugomvi kati yake na baba yao.

Amedai baba yao alimgombeza baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yake.

“Baba alikuwa hapendi kaka ashindwe kwenye mitihani yake. Alikuwa akimgombeza sana kwa nini anafanya vibaya kwenye masomo, kaka alikuwa ananuna sana, ila alikuwa hasemi,” amedai binti huyo.


Baba azungumza

Halpha Willson (40), baba wa mtoto huyo amesema jana jioni alipofika kumuona mtoto wake, hakumkuta akaambiwa ameenda kucheza mpira.

Aliporudi alimuuliza kwa nini anacheza mpira wakati muda ile ulikuwa wa kujisomea, alimjibu kuwa akikaa peke yake nyumbani anahisi upweke.

Hata hivyo, amesema aliondoka na ilipofika saa moja usiku, Alily alimfuata mjini alikokuwa akiishi akamambia amefuata fedha ya kununulia karatasi. “Nikampatia Sh2,000 akaondoka.”

Amesema alikuwa hakai na watoto wake nyumba moja baada ya kutengana na mke wake miaka mingi iliyopita, baada ya ugomvi wa mara kwa mara.

“Mwanangu alikuwa hafanyi vizuri kwenye masomo kutokana na mimi kuwa na majukumu mengi, licha ya kumpatia matumizi yote. Nilioa mwanamke mwingine nikaona ni bora niwapangie chumba,” amesema baba huyo anayefanya kazi za usafi katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Bukoba.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa hayuko ofisini.

Hata hivyo, Mwananchi Digital imezungumza na

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba, Museleta Nyakiroto ambaye amethibitisha kupokea mwili wa mwanafunzi huyo.

Amesema wanaufanyia uchunguzi mwili huo na ukikamilika utakabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya kuendelea na utaratibu wa mazishi.

“Ni kweli tumeupokea mwili wa mwanafunzi huyu saa 11:30 jioni hii, tunaufanyia uchunguzi tutatoa taarifa ya kile tulichokibaini tukimaliza,” amesema Dk Nyakiroto.