Mwanajeshi kunyongwa

Muktasari:

  • Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha 08/691 KJ Chandarua mkoani Ruvuma, Sajenti Batsin Sanga amehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuwaua kwa risasi mtalaka wake na mwanajeshi mwenzake.

Songea. Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha 08/691 KJ Chandarua mkoani Ruvuma, Sajenti Batsin Sanga amehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuwaua kwa risasi mtalaka wake na mwanajeshi mwenzake.

Desemba 27 mwaka 2018 katika lango kuu la kambi hiyo, askari huyo mwenye namba za kijeshi MT81337 akiwa na bunduki aina ya AK47, aliwashambulia kwa risasi Veronica Kayombo na Aaskari mwingine na kusababisha wafe papo hapo.

Ingawa jina la askari aliyeuawa pamoja na Veronica halitajwi kwenye hukumu, ushahidi unaonyesha askari huyo alifyatua risasi 10 kati ya 30 alizokabidhiwa huku miili ya marehemu ikikutwa na majeraha ya risasi kichwani.

Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 28 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea, Yose Mlyambina aliyesema adhabu kwa anayepatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia ni moja tu, nayo ni kunyongwa hadi kufa.

Awali, kesi iliendeshwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Shaban Mwegelo akisaidiana na Amina Mawoko ila baadaye ikaendeshwa na Wakili Hebel Kihaka akisaidiwa na Lugano Mwasubiria na Tumpare Lawrence.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mlyambina alisema kulingana na ushahidi uliotolewa, mshitakiwa alimpiga risasi ya kichwa Veronica na akamlenga risasi ya kichwa na mkono askari mwenzake.

“Pia silaha iliyotumiwa na mshitakiwa ilikuwa ni ya hatari. Hiyo inadhihirisha mshitakiwa alidhamiria kuwaua marehemu. Mshitakiwa angeweza kuwapiga risasi maeneo mengine ya mwili kama miguuni lakini hakufanya hivyo. Upande wa mashitaka umethibitisha pasipo kuacha mashaka kwamba mshitakiwa aliwaua watu hao akiwa na dhamira ovu,” alisema Jaji Mlambina katika hukumu yake.

Ukiacha ushahidi huo, jaji alisema mshitakiwa alikanusha kuwaua marehemu ila alikiri kutokea mauaji katika eneo lake la kazi ambako watu wawili walipigwa risasi.

“Mapenzi ni hisia kali sana za ndani ambazo hazielezeki. Kwa lugha rahisi mapenzi ni kitu kizuri sana na chenye harufu nzuri ya kuvutia na ambacho kinadumu milele bila kujali mazingira. Ingawa siku hizi jamii imethibitisha kinyume chake. Mapenzi yamekuwa bidhaa inayoharibika, inaoza na kuzama. Utamu umekuwa uchungu kiasi cha kusababisha wapendanao kuuana wao kwa wao,” alisema jaji akihukumu.

Siku mauaji hayo yanatokea, ilikuwa ni karibu miaka mitatu tangu mshitakiwa atalikiane na Veronica na jana yake Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea ilitoa haki ya mke kutunza mtoto.

Veronica akiwa na rafiki yake aitwaye Jamila Said walienda kwenye kambi hiyo alikokuwa akifanya kazi mshitakiwa ili kupeleka amri hiyo.

Wakiwa lango kuu, mshitakiwa alimuona mtalaka wake na kwenda alipokuwa akiwa ameshika bunduki na kumuuliza amefuata nini na akamjibu wameshahudumiwa.

Ghafla mshitakiwa alichukua bunduki aliyokuwa nayo na kumfyatulia risasi Veronica kisha akaanza kumkimbiza askari mwenzake aliyekuwepo eneo hilo na kumfyatulia risasi pia na wote wawili kufariki.

Jamila alifanikiwa kutoroka kupitia kibanda kilichokuwapo jirani na alipokuwa anakimbia alisikia milio mingine ya risasi kule alikokuwa ametoka baadaye alijulishwa rafiki yake ameuawa na mtalaka wake.

Mshitakiwa akiwa na bunduki alielekea ofisi kuu ya kambi akiendelea kufyatua risasi kabla askari wawili hawajamdhibiti.