Mwigulu anafanya kile alichokikataa kwa wenzake

Muktasari:

  • Lewis E. Gleeck Jr, ni mtumishi wa zamani wa Idara ya Mambo ya Nje, Marekani. Baada ya kustaafu, akiwa amelitumikia taifa lake kwenye nchi mbalimbali duniani, aliweka makazi yake Ufilipino, akifanya kazi na Shirika la Marekani la Misaada (USAID).

Lewis E. Gleeck Jr, ni mtumishi wa zamani wa Idara ya Mambo ya Nje, Marekani. Baada ya kustaafu, akiwa amelitumikia taifa lake kwenye nchi mbalimbali duniani, aliweka makazi yake Ufilipino, akifanya kazi na Shirika la Marekani la Misaada (USAID).

Katika maisha yake, Gleeck aliandika vitabu 14. Imempendeza Mungu leo nichambue kimojawapo, kinaitwa “President Aquino: Sainthood Postponed” – “Rais Aquino: Utakatifu Uliahirishwa.”

Kitabu kinamhusu Rais wa 11 wa Ufilipino, Maria Corazon Aquino, ambaye aliingia madarakani mwaka 1986 baada ya mapinduzi yalimwondoa kwenye usukani, aliyekuwa Rais wa miongo miwili, Ferdinand Marcos.

Rais Aquino, ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Cory, ikiwa ni kifupi cha Corazon, nyakati za mwanzo za uongozi wake ulikuwa na majuto mengi. Watu ambao walijiona wao ndio waliomuingiza madarakani walikubuhu kwa vitendo vya rushwa.

Ndani ya Serikali yake, kulikuwa na marafiki, ndugu na jamaa waliosimama mstari wa mbele kuhamasisha maandamano yaliyomwondoa kitini Marcos. Cory aligundua hao ndiyo walikuwa kikwazo. Ilibidi awageuke.

Kitendo cha kuwageuka kikazaa uasi na uadui ndani ya Serikali aliyoiongoza. Ni hao washirika wake waliobadilika na kueneza propaganda chafu dhidi ya Cory. Kanisa Katoliki lilikaribia kumpa “Utakatifu,” ikaahirishwa kwa sababu ya hoja za waliokuwa washirika wake ambao walisema “alikuwa mtenda dhambi, hakuwa mtakatifu.”


Nasaha kwa Rais Samia

Cory alikuwa Rais mwanamke kama Samia Suluhu Hassan. Dunia haijabadilika sana kutoka Ufilipino wanaume walivyodhani wangemfanya Cory kuwa kivuli chao cha kupora nchi hadi Tanzania ya Samia.

Kipimo cha juu kabisa cha kuonyesha kuwa kuna namna ya kutaka kumfanya Rais ni kivuli ni pale maagizo yake yanapokiukwa au yanapogeuzwa maneno yenye kupita. Kauli ya Rais ni amri. Haipaswi kuchezewa. Ni dhambi kupewa changamoto na watendaji wa Serikali anayoongoza.

Mei 9, mwaka huu, Rais Samia, alilihutubia taifa na kutangaza nafuu ya mafuta. Moja ya maagizo yake ni kuwa lazima Serikali ijibane kwenye matumizi yake ya ndani.

Kauli hizo zilirudiwa na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nishati, January Makamba.

Wakati wa Hotuba ya Bajeti 2022-2023, Mwigulu alikazia hilo la Serikali kujibana kwenye matumizi yake ya kawaida. Na matarajio yalikuwa kuona Mwigulu na mawaziri wengine wawe mfano, halafu wasaidizi wao wafuate.

Hivi karibuni, nilishuhudia msafara wa makumi ya magari na pikipiki zaidi ya 80, kwenye mapokezi ya Mwigulu, Tarime, Mara. Mwigulu alikuwa na ziara ya kiserikali kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, Sirari.

Magari kwa kuyahesabu yalifika 15, karibu yote ni Land Cruiser na injini zake ni V8, hivyo ulaji wake wa mafuta ni mkubwa.

Pikipiki bila shaka zilikodiwa na kuwekewa mafuta. Fedha zote hizo kwa masilahi gani? Kumbuka; Rais ameagiza kubana matumizi.

Tafsiri; Land Cruiser 15 V8 na pikipiki zaidi ya 80. Msafara wa Waziri wa Fedha. Ni kitendo cha kejeli kwa wananchi. Unawaambia Serikali itapunguza matumizi bungeni, kisha nje ya Bunge unaongeza kasi ya matumizi.

Wananchi bado hawaelewi kuhusu tozo za miamala ya simu na benki ambazo Mwigulu kwa nafasi yake ya Waziri wa Fedha ndiye msimamizi mkuu. Halafu yeye anakwenda Tarime, ziara ya Serikali, kufanya maonyesho ya kisiasa kwa anasa na matumizi mabaya ya pesa. Je, ni kampeni?

Hivi karibuni, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Prof Mussa Assad, alishauri tozo kuondolewa kwa wananchi na badala yake mawaziri ndio watozwe kodi kwa sababu wanatumia magari yenye matumizi makubwa ya mafuta.

Kauli ya Assad ni ya kitaalamu. Waziri wa Fedha alipaswa kuichukua na kuitafakari. Badala yake, alikimbilia Tarime kufanya maonesho ya kisiasa. Msafara mkubwa sana. Je, ndio jicho la urais?

Kuna mahali unajiuliza ikiwa Mwigulu ni Waziri wa Fedha anafanya haya, je, akiwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au Rais? Si anaweza kutaka vifaru na helikopta za kijeshi kwenye msafara wa magari 200? Lengo ni kupata nini?


Kampuni kufungiwa madeni

Juni 9, mwaka huu, Rais Samia alikuwa ziarani mkoani Kagera, alitoa maagizo kwa mamlaka za kukusanya kodi kuacha kuwasumbua wafanyabiashara kwa madeni ya miaka ya nyuma.

Rais Samia alisema, malimbikizo ya madeni ni makosa ya mamlaka za ukusanyaji na wafanyabiashara. Ambacho huwa kinafanywa ni kwamba wakosaji ni wafanyabiashara peke yako.

“Suala la watu kupewa bili za nyuma za kodi walipe leo. Ndugu zangu, nataka kusema hivi, miaka yote hiyo watoza kodi wapo, kama halmashauri zipo, mmeachia watu hawakulipa. Leo unampelekea mtu bili ya miaka mitano sita nyuma, wakati ule ulikuwa wapi?” alihoji Rais Samia.

Akaendelea: “Kama hakulipa ndio ni kosa lakini kosa sio lake peke yake. Kosa na la mkusanyaji pia kwa sababu kama alilipa pungufu ndivyo ulivyotaka alipe, kama hakulipa kabisa maana yake hukufuatilia. Achaneni na hiyo biashara. Achaneni na biashara ya miaka mingi nyuma.

“Mnachoweza kufanya ni kurudi mwaka mmoja nyuma, kwa sababu inawezekana kabisa labda mwaka jana hamkumaliza pirikapirika za kufanya mahesabu, kwa hiyo wafanyabiashara walipe kuanzia mwaka jana na kuendelea. Lakini miaka mitatu nyuma na kuendelea achaneni na hiyo biashara.”

Kwa msisitizo kabisa, Rais Samia alisema: “Wapeni raha wafanyabiashara wafanye biashara zao. Sasa msisitize ukusanyaji wa mapato kuanzia tulipo kwenda mbele. Ule udhaifu uliokuwepo kule nyuma, hamwezi kuulipa kwa kuwapa adhabu wafanyabiashara.”

Mwisho wa kumnukuu Rais Samia; hoja inakuja kwamba tangu kutoka kwa kauli hiyo bado wafanyabiashara wanaendelea kufungiwa akaunti zao za benki kwa hoja za madeni ya zamani. Tena nyingi ni faini.

Swali; Rais Samia ana ndimi mbili? Kwamba kwenye mkutano wa hadhara Kagera alisema wafanyabiashara wasisumbuliwe kwa madeni ya nyuma, kisha ndani ya Serikali alitoa maagizo ya kuendelea kuwasulubu wafanyabiashara?

Je, maagizo ya Rais Samia hataheshimiki kwa wasaidizi wake? Kwamba yeye kama Mkuu wa Nchi na Mkuu wa Serikali ameona madeni ya kodi ya miaka mingi nyuma ni hayana maana, haoni msingi wake, zaidi anayachulia kuwa ni kero kwa wafanyabiashara.

Wakati huohuo, wasaidizi wa Rais na watendaji wa mamlaka za ukusanyaji kodi, wanaona Rais Samia anakosea, kwa hiyo wanaamua kumwendea kinyume na kuwasumbua wafanyabiashara kwa kufungia akaunti zao. Huu ni ukaidi. Na ni hatari sana.

Rais Samia alitoa maagizo ambayo umma ulisikia na kuona. Vyombo vya habari vilichukua na kusambaza maudhui. Wafanyabiashara wanapobanwa upya kwa madeni ya miaka mingi nyuma, tena nyingi ni faini, hakuna tafsiri zaidi ya ukweli kuwa kauli ya Rais ama inasalitiwa au inapuuzwa.

Hivi karibuni kuna mfanyabiashara alinionyesha barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwenda Benki ya CRDB, wakielekeza akaunti zake zifungiwe kwa madeni ya miaka ya mingi iliyopita.

Mfanyabiashara huyo (namhifadhi), akaniuliza: “Hivi Rais anaweza kutamka kitu halafu wasaidizi wake wakapuuza?” Nikabaki na mshangao. Nikarejea hotuba ya Rais ya Kagera. Nikashangaa zaidi.

Binafsi nilimwelewa sana Rais Samia alipotoa amri ya wakusanya kodi kutojihusisha na madeni ya miaka ya nyuma na kutaka waanze mwaka jana.

Kuanzia mwaka 2017, wafanyabiashara wengi walianza kupewa rundo la madeni ya kodi na ushuru, ambayo hayakuwa na msingi wowote. Ndio maana Rais Samia alihoji: “Siku zote hizo ninyi mlikuwa wapi?”

Mwigulu ndiye Waziri wa Fedha. TRA ipo chini yake na ndio inafungia akaunti za wafanyabiashara kinyume na maagizo ya Rais Samia. Hapohapo Mwigulu anafanya ziara kwa msululu wa magari na pikipiki, tofauti na matakwa ya Rais Samia kubana matumizi. Je, Mwigulu anamkaidi Rais?

Hii tabia ya maagizo ya Rais kutoheshimiwa, sio tu yanavunja heshima ya taasisi ya urais, bali yanaifedhehesha serikali, mifumo ya usalama na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndicho kinachotawala. Halafu Samia ndiye Mwenyekiti CCM.

Udhaifu wa kiusalama ni hatari zaidi. Lipo janga lilitokea Ufilipino Januari 25, 2015. Maagizo ya Rais Noynoy Aquino (mtoto wa Cory), hayakuheshimiwa na Jeshi la Polisi (PNP).

Ilifanyika oparesheni maalumu ya kupambana na magaidi wa kikundi cha Moro Islamic Liberation Front (MILF). Polisi walikaidi mwongozo wa Rais na kutekeleza oparesheni kivyao, matokeo yake raia wasio na hatia 44 walifariki dunia.

Kisha, Ofisi ya Rais na Polisi wakaanza kurushiana mpira. Polisi walilaumu Rais alikosea maagizo, wakati Ofisi ya Rais walitupia lawama PNP kwa kutotii maagizo ya Rais.

Mpaka hapo heshima ya Rais inakuwa wapi? Maagizo ya Rais Samia yanaweza kutenguliwa na Wizara ya Fedha, je siku ikitokea Wizara ya Mambo ya Ndani? Hayatajirudia ya Noynoy na PNP? Vipi ikifika siku Wizara ya Ulinzi nayo ikakaidi? Tutabiri hatari?