Mwili wa anayedaiwa kufa kwa kipigo cha polisi wachunguzwa

Enos Misalaba enzi za uhai wake

Geita. Sakata la mwili wa Enos Misalaba (32), anayedaiwa kupoteza maisha akiwa Kituo cha Afya Mganza wilayani Chato na wananchi kugomea kuuzika kwa kuupeleka kituo cha polisi, limechukua sura mpya baada ya kulazimika kufanyiwa uchunguzi kujiridhisha na sababu za kifo chake.

Enos alifariki Machi 28 na juzi mwili wake ulishindikana kuzikwa baada ya historia ya marehemu kusomwa na kuelezwa kijana huyo amefariki kwa kuugua kifua, kitendo kilichopingwa na wananchi.

Wananchi walilibeba jeneza lenye mwili wa kijana huyo na kulipeleka kituo cha polisi wakitaka kujua chanzo cha kifo chake, ndipo vurugu zikaibuka na polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Vurugu hizo zilisababisha wananchi kukichoma moto kituo hicho cha polisi huku mwili wa kijana huyo ukipelekwa eneo ambalo halikufahamika na polisi hadi jana ulipoanza kuchunguzwa Hospitali ya Wilaya ya Chato.

Inadaiwa Enos alikamatwa Machi 27 akituhumiwa kuiba betri ya gari na kupelekwa kituoni hapo na alipoteza maisha siku iliyofuata akiwa Kituo cha Afya Mganza alikokuwa akitibiwa.

Kutokana na kadhia hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay alisema mwili huo unafanyiwa uchunguzi upya katika hospitali ya wilaya kabla ya kwenda kuuzika nyumbani kwao huko Kata ya Mganza.

Alisema wamelazimika kuufanyia uchunguzi upya ili kujiridhisha sababu za kifo cha kijana huyo.

“Hali sasa (ilikuwa mchana) ni tulivu, tunajiandaa kuuhifadhi mwili wa huyu kijana. Tupo kwenye mchakato wa kurudia postmortem, kwa sasa tunajaribu kuhakikisha hali inakuwa nzuri ili tuweze kuuhifadhi mwili na taratibu nyingine zitafuata,” alisema Berthaneema.

Mazishi hayo yalitarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale, uongozi wa polisi na wananchi wa Mganza.

Akizungumzia vurugu zilizosababisha kuchomwa moto kwa kituo cha polisi, Kamanda Berthaneema alisema hadi sasa hakuna anayeshikiliwa, ila baada ya mazishi watafanya uchunguzi kuwabaini waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake.

Alisema vurugu hizo zilisababisha watu wanne kujeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa matibabu.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa wananchi wa Mganza zinasema baadhi yao wameanza kukimbia wakihofia kukamatwa kutokana na kadhia iliyotokea, kwani vurugu hizo ziliwafanya polisi kutoka maeneo mengine ya Chato kwenda kuongeza ulinzi.

“Kuna familia zimekimbia, kuna watu wamekimbia, vijana wa hapa hasa waliokuwepo wametokomea. Si unajua kuchoma kituo cha polisi si jambo zuri,” alisema mwananchi mmoja aliyeomba asitajwe jina.

Akizungumzia malalamiko dhidi ya polisi wanaodaiwa kumpiga kijana huyo na tuhuma za uonevu dhidi ya wananchi, Kamanda Berthaneema alisema “tuhuma zinahitaji kuchunguzwa ili kujiridhisha kuwa anayetuhumiwa anahusika. Kwa hiyo Jeshi la Polisi tumefungua jalada la uchunguzi ili tuone kama kweli vijana wetu walihusika au kuna mtu mwingine na kuna sababu zilizochangia kutokea kwa tukio hilo,” alisema.

Berthaneema alisema vurugu zilizotokea zilisababishwa na madereva bodaboda ambao ndio walioubeba mwili uliokuwa tayari kwa ajili ya maziko na kusababisha vurugu zilizochoma kituo na baadhi ya watu kujeruhiwa.

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamedai ndugu zao kukimbia wakihofia kukamatwa na Jeshi la Polisi kutokana na vurugu hizo.

Bertha Malongo, mama mzazi wa Simon Misalaba alisema alipata taarifa kwa jirani yake saa mbili usiku akimueleza amemuona mwanaye akisukumwa kuingia kituo cha polisi, lakini hakujua sababu za mwanaye huyo kukamatwa hata kupoteza maisha baada ya muda mfupi.

Alisema asubuhi ya siku iliyofuata alikwenda kituoni kumwona na kuelezwa amepelekwa hospitali na alipofika hospitalini alimkuta akiwa amelala huku amefungwa pingu na hawezi kupumua vizuri.

“Daktari aliniambia nitoe Sh3,000 ili aweze kutibiwa...nikarudi kwa ndugu na kuomba fedha hizo. Nilienda kwa mwanamume anayedai kuibiwa betri akasema yeye hakumpiga bali alipigwa na askari. Baada ya kuandikisha kwenye jalada niliambiwa nitoe Sh9,000 za kununua dawa. Nilirudi wodini na nilipofika niliuliza afya ya mwanangu inaendeleaje nikaambiwa amekufa,” alisema Bertha.

Mama huyo alisema mwanaye hakuwa mgonjwa wakati wa uhai wake mpaka anakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi.

Enzi za uhai wake, alisema mwanaye alikuwa dereva wa bodaboda na wakati mwingine alikuwa anaendesha bajaji na hakuwahi kuambiwa kilichosababisha kifo cha mwanaye.