Mwili wa Mstaafu wetu unapohitaji kukatiwa bima!

Muktasari:

  • Alipokuwa kijana, Mstaafu aliaminishwa kuwa, bima hukatwa kwa ajili ya vyombo vya moto tu likiwamo gari, pikipiki na meli, sijui ndege!

Alipokuwa kijana, Mstaafu aliaminishwa kuwa, bima hukatwa kwa ajili ya vyombo vya moto tu likiwamo gari, pikipiki na meli, sijui ndege!

Baadaye sana akafahamu kuwa hata ‘vyombo vya baridi’ kama maghala na hata majengo makubwa ya ofisi hukatiwa bima!

Anaomba kukiri kuwa, hakujua kuna siku mwili wake, utakuja hitajika kukatia bima!

Ilianza na kauli awezazo kuziita za ‘kisiasa’, ilipotangazwa kuwa wazee wa nchi njema hii ya Tanzania wanaofikisha miaka 60 ya kuzaliwa, watakuwa na haki ya kupata matibabu bure! Yaani Mstaafu akiamka kichwa kinamgonga, ni kiasi tu cha yeye kuwasilisha makunyanzi yake dirisha la zahanati yoyote nchini na angeandikiwa kadi, angemuona daktari na angepata dawa bila kulazimika kuonyeshwa ‘pharmacy’ inayotizamana na zahanati husika akanunue dawa alizoandikiwa huko!


Matibabu ya bure kwa wazee!

Mstaafu wetu akajikuta anafurahi kupita kiasi na kuisifu Serikali njema ya nchi yake. Alikuwa amekwisha staafu na magonjwa nyemelezi ya wazee ya kisukri, shinikizo la moyo na tezi dume yalikuwa hayachezi mbali na yanakipukutisha zaidi kipensheni chake cha ‘laki si pesa.’

Naam, matibabu ya bure! Hatimaye Serikali yake ilikuwa imewafanyia kitu ambacho ingeweza kujidai nacho kwamba imewafanyia wazee wake! Usipomtunza mzee wako katika uzee wake utamtunza nani tena? Kwa hakika Mstaafu wetu sasa akawa na jeuri ya kuyaambia magonjwa yanayongoja afike uzeeni ya kisukari, shikizo la damu na tezi dume, sasa yakae chonjo, saa mbaya! Alikuwa na matibabu ya bure!

Kabla hata hajayafaidi vizuri, katikati hapo likachomekwa jingine la Bima ya Afya, kwamba Mstaafu wetu sasa inambidi achimbe zaidi kapensheni kake ka ‘laki si pesa’ ili ajiandikishe Bima ya Afya yeye na nyumba yake.

Yaani anapoamka kichwa kinamgonga tena na ndani hana hata senti tano mbovu, aende zahanati kupata matibabu yanayosemekana ni ya bure lakini ameishatumia sehemu ya pensheni yake kuikatia bima! Naam, Bure iliyo gharama!

Na akaambiwa kabisa hata Bima ya Afya yenyewe ina madaraja kutegemea na pochi. Kuna Bima ya Afya inayoshia kutibu kichwa kinachogonga au tumbo la kuendesha. Kuna Bima ya Afya inaishia kwenye ‘hivyo vidonge hatuna’! na kuna Bima ya Afya inayoweza hata kutibu kwa oparesheni na vidonge vya bei mbaya.

Sio wewe uko daraja la ‘kichwa kinagonga’ au ‘tumbo kuendesha’ utake matibabu ya oparesheni! Kinondoni inakuhusu!

Mstaafu wetu alilielewa somo hili vizuri yalipomkuta ya kumkuta. Ilikuwa alifajiri ya Novemba 23 mwaka jana wakati alipoingia bafuni kujiswafi ili kujiandaa na shughuli za siku hiyo. Akaingia bafuni na kushangaa sana viungo vyake vya mwili vikimfanyia ‘mgomo baridi’! Mikono yake anaiangalia lakini ‘akiitaka’ kufunga bomba ili maji yasimwagike, ni kama imefungwa kamba! Akitaka kutoa sauti ili kuita watu, koo lake linaishia kukoroma badala ya kuita! Akaishia kuanguka chini bafuni!

Ni vijana wake walioshtuka mbona Mstaafu amekaa sana bafuni na maji yanawagika tu na kuna sauti kama ya mtu anakoroma walioamua kufungua mlango kwa nguvu a kumkuta Mstaafu wetu yupo katikati ya maandalizi ya kuelekea Kinondoni!

Ikawa mshike mshike wa kumuwahisha Mstaafu kwenye zahanati ya karibu ya huku Mbezi mwisho aliko, walipomungalia tu na kumpa huduma ya kwanza wakawataka vijana wamuwahishe haraka Taasisi ya Moyo ya JK wakipita kwanza Hospitali ya Mwananyamala kuchukua makaratasi ya nini sijui! Inawezekana Mzee wetu aliisha kata tiketi ya ‘Mwendokasi’ kuelekea Kinondoni!

Anashukuru sana kwamba siku ile ya Novemba 23 njiani kulikuwa hakuna foleni. Labda kwa vile ilikuwa ni Jumamosi, safari nzima akaishia kuota ndoto za misalaba na makaburi tu! Hatimaye akafikishwa Taasisi ya Moyo ya JK na madaktari na wauguzi wakapambana vilivyo Mstaafu wetu asiwe mkazi wa kudumu wa Kinondoni na kwa vile Kinondoni ina wenyewe na Mstaafu wetu sio mmoja wao basi angalau Mabwepande!

Akalazwa Mwaisela kule Muhimbili kwa wiki nzima. Anawashukuru sana madaktari na wauguzi wa wodi ile waliohakikisha hahamii Kinondoni au Mabwepande. Anawashukuru zaidi mno vijana na wajomba zake kwa kuchimba mifukoni mwao ili kumtibu mzee wao. Mstaafu anakumbuka kuwa kila alipofika kitu cha kwanza walimuuliza yuko bima gani na yeye kuwajibu kuwa ni Mzee wa miaka 63 na ana matibabu ya bure! Waliokuwepo waliishia kutabasamu tu!

Baada ya wiki moja Mstaafu wetu akaruhusiwa kutoka Muhimbili lakini akakazaniwa sana kufanya mazoezi kwa kuwa ndio moja ya tiba yake.

Akawaelewa sana alipotaka kutembea au kuandika kwa kalamu neno ‘Mstaafu’ nini jina lake! Yeye mtu wa miaka 63 leo anajifunza kutembea na kuandika! Hakika wajukuu zake wana haki pale wanapomuimbia “Simama dede nikupe Mkate!” pale anapojifunza kutembea!

Mstaafu anaishukuru sana teknolojia. Bado hawezi kuandika kwa kalamu lakini angalau teknolojia inamuwezesha kuandika ‘Kona ya Wastaafu’ japo kwa siku mbili tatu za kubonyeza kizenji kwenye tarakilishi yake tofauti na saa mbili au tatu aliyotumia enzi zake. Lakini ndio mazoezi yenyewe!

Mkasa mzima umemfanya Mstaafu aizidi kuamini kwamba sera ya ‘Matibabu ya Bure kwa Wazee’ Ipigiwe debe zaidi kushinda ya ile ‘Bima ya Afya.’

Angalau Serikali itakuwa na kitu cha kujivunia nacho kwamba nayo imewafanyia kitu wazee na Wastaafu walioijenga nchi hii na kuifikisha ilipo.

0754 340606 / 0784 340606