Mwisho wa enzi wabunge, madiwani kupita bila kupingwa

Dar es Salaam. Unaweza ukawa mwisho wa utaratibu wa wabunge na madiwani wanaopita bila kupingwa katika chaguzi, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kubatilisha vifungu vya sheria vinavyoruhusu kuwapo kwa wabunge na madiwani wa aina hiyo.

 Uamuzi huo wa mahakama umekuja wakati Bunge la sasa hivi likiwa na wabunge 28 waliopita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, wakiwamo mawaziri kadhaa na wabunge kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kulingana na uamuzi huo, mawakili wa kujitegemea Daimu Halfani na Dk Rugemeleza Nshalla walilileza Mwananchi kuwa kuanzia sasa hata ukitokea uchaguzi mdogo, hakuna mgombea yeyote kwa nafasi hizo ambaye atatangazwa kupita bila kupingwa.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Felesh hakuweza kutoa msimamo wa Serikali kuhusiana na uamuzi huo, akisema kuwa ni mapema, kwani uamuzi huo hauna muda mrefu na kwamba unahitaji utafiti kwanza kabla ya kutoa msimamo wa Serikali.


Hukumu

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo katika hukumu yake ya kesi ya kikatiba, iliyofunguliwa na mwanasiasa, mwanachama wa chama cha ACT–Wazalendo, Joran Lwehabura Bashange, baada ya kukubaliana na hoja zake.

Bashange alifungua kesi hiyo Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akipinga kuwepo kwa wabunge na madiwani wanaotangazwa kupita bila kupingwa.

Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 19 ya mwaka 2021, Bashange alikuwa akihoji uhalali wa kikatiba wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (NEA), Sura 343 kinachoruhusu kuwepo kwa wabunge wanaopita bila kupingwa.

Pia alikuwa akihoji uhalali wa kikatiba wa vifungu vya 45(5) na 13 (7) vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292 vinavyoruhusu kuwepo kwa madiwani wanaopita bila kupingwa.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo; John Mgetta (kiongozi wa jopo), Dk Benhajj Masoud na Edwin Kakolaki, mahakama hiyo imesema vifungu hivyo vinakinzana na Katiba.

Hivyo imesema ni batili kwa kukiuka masharti ya Ibara ya 21(1) (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ambavyo imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara.

“Hivyo tunaendelea kuvitupilia mbali vifungu hivyo kutoka katika vitabu vya sheria,” inasomeka sehemu ya hitimisho la hukumu hiyo.


Madai ya Bashange

Bashange katika kiapo chake na hoja za mawakili wake, Mpale Mpoki, Halfan na Melchzedeck Joachim wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, alikuwa akidai kuwa kuwepo kwa vifungu hivyo vinavyoruhusu kuwepo kwa wagombea wanaotangazwa kupita bila kupingwa katika nafasi hizo, vinakiuka Katiba ya nchi.

Pia walisema kwamba Bunge lilikwenda nje ya mamlaka yake kutunga vifungu hivyo.

Walifafanua kuwa vifungu hivyo vinakiuka haki ya wananchi ya kupiga kura kuchagua wawakilishi wao na kushiriki katika masuala ya umma kupitia wawakilishi waliochaguliwa bungeni na katika Serikali za Mitaa.

Pia walidai kuwa vifungu hivyo vinakinzana na Katiba ibara za 21(1), (2) pamoja na vyombo mbalimbali vya kimataifa na vya kikanda, yaani mikataba na matamko mbalimbali kuhusiana na haki mbalimbali.

Vilevile walisema vinaweka ubaguzi, kwani wakati vifungu hivyo vinaruhusu wagombea pekee katika nafasi hizo kutangazwa kupita bila kupingwa, mgombea urais ni tofauti, kwani mgombea huyo hata kama anagombea peke yake, atalazimika kupigiwa kura kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha NEA.

Bashange na mawakili wake walidai kwa kuwa Katiba haitambui kuwepo kwa wabunge na madiwani wa kupita bila kupingwa, bali wa kupigiwa kura, hivyo aliiomba mahakama hiyo itamke kuwa vifungu hivyo ni batili na iamuru vifutwe katika vitabu vya sheria nchini.


Majibu ya Serikali

Wakati wa usikilizaji, Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a alipinga hoja zote za mawakili wa Bashange, akidai kuwa kwa kuwa shauri hilo lina madai mazito ya uvunjaji Katiba, wanapaswa kuthibitisha madai yao kwa kiwango kisichoacha mashaka.

Hata hivyo, alidai kuwa mdai alishindwa kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachotakiwa, akidai kuwa hakuweza kutoa ushahidi kuonesha kuwa vifungu hivyo alivyokuwa akivilalamikia vinakiuka haki hizo za kikatiba.

Wakili Chang’a alidai kuwa haki ya kupiga kura haiwezi kuchukuliwa kuwa imekiukwa, isipokuwa kwa kuonyesha kuwa mchakato wa uteuzi na utangazaji wa wagombea wanaopita bila kupingwa, unakinzana na sheria za uchaguzi.

Vilevile alidai kuwa suala la wagombea wanaopita bila kupingwa haliwezi kutolewa na mdai pekee, wakati utaratibu huo unawahusu wapiga kura walio wengi, ambao hawaonekani kulalamikia vifungu hivyo.

Alisisitiza kuwa vifungu hivyo havikiuki Katiba kwa kuwa vinalinda maslahi ya umma kwa kuokoa gharama za kuendesha uchaguzi zisizo za lazima kwa wagombea wasiokuwa na mpinzani, na kwamba hivyo vinalindwa na ibara ya 30(1) (2) ya Katiba.

Badala yake Wakili Chang’a alidai kuwa utaratibu huo wa kumpigia kura mgombea pekee, unatumika kwa nafasi ya urais tu kutokana na nafasi yake ya kuwa Amiri Jeshi Mkuu.

Alidai kuwa utaratibu huo unatumiwa katika nchi kama vile Uganda, Pakstan, Malawi, Kenya, Zambia, Zimbabwe na Ghana.

Vilevile Chang’a alidai kuwa ibara ya 77(1) ya Katiba inalipa mamlaka kutunga sheria za kusimamia uchaguzi na kwamba vifungu hivyo ni sehemu ya sheria hizo.


Uamuzi wa Mahakama

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote, ilitupilia mbali hoja za Serikali pamoja na mambo mengine ikisema kuwa masharti ya vifungu hivyo yanamnyima mwananchi haki ya kupiga kura.

Ilisema kuwa ibara ya 66(1) inataja aina ya wabunge, lakini haijumuishi wabunge waliopita bila kupingwa, ambapo ibara ya 61(1) (a) inataja wabunge wa majimbo (waliochaguliwa kuwakilisha majimbo na kwamba 76 na 77(1) zinaelezea uchaguzi wa wabunge katika majimbo.

Pia imesema kuwa inatambua kuwa ibara ya 5 inaeleza hali au sababu ambazo chini ya sheria iliyotungwa, zinaweza kuondoa haki ya mwananchi kupiga kura, na kwamba katika sababu hizo hakuna inayoakisi vifungu hivyo.

Vilevile imesema kuwa wadaiwa hawakuonesha ni namna gani gharama zinazookolewa na Serikali kwa kutoendesha uchaguzi kwa wagombea wasio na wapinzani, kunakidhi masharti ya ibara ya 30(2) ya Katiba.

Hivyo imesema kuwa imeshawishika kwamba mbunge wa jimbo ni lazima awe amechaguliwa kwa uhuru na wananchi isipokuwa kama kuna kizuizi kinachoruhusiwa na Katiba, ikielezea kumwondelea mwananchi haki ya kupiga kura.

“Kwa hiyo tunakubaliana na mdai kuwa vifungu vinavyopingwa vinakiuka Katiba inayotoa haki ya kupiga kura chini ya ibara ya 21,” imesisitiza mahakama hiyo.


Maoni ya wanasheria

Baada ya mahakama kutoa hukumu hiyo, wakili Halfan alisema Bunge linapaswa kukifuta kifungu hicho na kuweka kifungu kinachoeleza kuwapigia kura wagombea pekee.

“Hata wasipofanya hivyo Tume ya Uchaguzi haipaswi kuwatangaza wagombea wanaopita bila kupingwa. Hata ukitokea uchaguzi wowote mdogo kuanzia sasa hivi,” alisema wakili Halfani na kuongeza:

“Kuanzia sasa akitokea mgombea pekee katika jimbo au kata kutokana na sababu zozote zile, huyo mgombea naye lazima apigiwe kura.”

Alifafanua kuwa hata Bunge lisipofanya marekebisho hayo ya kuwapigia kura, masharti hayo yanaweza kuwekwa hata kwenye kanuni tu zinazotungwa na waziri mwenye dhamana.

Naye Dk Nshala alisema kuwa baada ya uamuzi huo wa mahakama, tayari kifungu hicho kimeshafutwa na kwamba hakuna haja hata ya kusubiri kwenda bungeni kukifuta.

“Kwa hiyo kuanzia sasa ukitokea uchaguzi kwa mgombea asiye na mpinzani, tunapaswa kumpigia kura ya ndio au hapana,” alisema Dk Nshalla.

Hata hivyo, alisema kuwa wale ambao tayari walishapita bila kupingwa katika uchaguzi uliopita, wao wamesalimika na kwamba ubunge wao ungeweza kuwa batili kama nao wangekuwa wameunganishwa kwenye kesi na kupingwa ubunge wao.