Uteuzi Mahera mjadala mzito, Mbatia ashtuka

Dk Charles Mahera

Muktasari:

  • Hisia hasi za uchaguzi Serikali za Mitaa zaibuka

Moshi/Dar. Uteuzi wa Dk Charles Mahera kuwa Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeibua hisia hasi dhidi ya uteuzi huo.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaona kwa kuwa mapendekezo ya kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa uchaguzi huo usimamiwe na Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) na hilo halijajibiwa kikamilifu, hivyo huenda Tamisemi ikausimamia.

Hata hivyo, mwanasiasa mkongwe nchini, James Mbatia alisema mfumo ndio una tatizo, hivyo bila mfumo na sheria kuwekwa sawa, tuhuma zinazojitokeza sasa dhidi ya Dk Mahera zitajitokeza mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

“Japokuwa nimeona kule Tamisemi portfolio yake anashughulika na afya, lakini Watanzania ni kama vile wameumwa na nyoka wakiona tu jani wanashtuka. Hii ni kwa sababu ya jinamizi lililotukumba katika Uchaguzi Mkuu 2020,” alisema.

“Hata hili la Rais kuteua mkurugenzi mpya wa uchaguzi katikati ya maridhiano halina afya sana. Hii iwe ni wake up call (iwaamshe) wadau wa demokrasia kupaza sauti. Uchaguzi ni kesho tu hapa, siku zimeshaisha,” alisisitiza Mbatia.

Katika Uchaguzi Mkuu 2020 ambao umelalamikiwa na vyama vya upinzani hususan Chadema, Dk Mahera alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC hadi wiki iliyopita alipobadilishwa kwenda Tamisemi.

Uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 28, uligubikwa na malalamiko mengi hadi Chadema wakauita “uchafuzi” na si uchaguzi na kulishuhudiwa mawakala wengi wa vyama vya upinzani wakiondolewa katika vituo vya kupigia na kuhesabu kura. Katika tangazo la Serikali (GN) namba 917 lililochapwa Oktoba 16, 2020, wagombea 28 wa ubunge kutoka CCM walipita bila kupingwa, ingawa upinzani ulidai uwepo wa mizengwe kwa wagombea wao.

Baadhi ya wagombea wa upinzani walidaiwa kutekwa na kunyang’anywa fomu ili wasizirudishe ndani ya muda uliowekwa, kuwekewa mapingamizi waliyodai hayakuwa na mashiko na baadhi ya rufaa zao kutotiliwa maanani na NEC.

Miongoni mwa waliotangazwa kupita bila kupingwa na majimbo yao kwenye mabano ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (Ruangwa), aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai (Kongwa), Nape Nnauye (Mtama) na January Makamba (Bumbuli).

Katika uchaguzi huo, CCM iliibuka na ushindi wa kishindo ambapo kati ya majimbo 264, wapinzani waliambulia majimbo manane kutoka CUF (watatu), ACT (wanne) na Chadema mmoja.

Hali ilikuwa hivyo hivyo katika nafasi za udiwani, kwani CCM iliibuka na ushindi zaidi ya asilimia 90 na hilo pengine ndilo linaloibua hisia kuwa pengine kupelekwa kwa Dk Mahera Tamisemi ni mkakati mahususi, ili baadaye asimamie uchaguzi 2024.

Wakati hisia zikiwa hivyo, ripoti ya matokeo ya tathmini iliyofanywa na NEC katika mikoa 24 ya Tanzania Bara, inaonyesha tume ilitekeleza majukumu yake ya kikatiba na kisheria kwa ufanisi katika Uchaguzi Mkuu 2020.

Hivyo, ripoti hiyo inadhihirishwa na uwepo wa kesi chache zilizofunguliwa kupinga matokeo au mwenendo wa uchaguzi na kwa ujumla kesi 15 zilifunguliwa huku kesi za ubunge zikiwa nne na kwa madiwani kesi 11.


Walichosema wasomi

Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Victory Lihuri alisema uteuzi wa mkurugenzi wa uchaguzi NEC unaashiria uchaguzi umekaribia kwa wale wenye mamlaka ya kuteua huwa wanajaribu kupanga safu zao upya.

“Wanafanya hivyo kujiimarisha ikiwa ni maandalizi uchaguzi unakaribia na tukumbuke maoni ya vyama vingi vilikuwa vimeomba NEC iweze kusimamia uchaguzi wa Serikali za mtaa, lakini hadi sasa NEC haijathibitisha,” alisema.

Dk Lihuri alisema kwa kuwa NEC haijathibitisha ni Tamisemi itakwenda kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa au la na sasa haijulikani utaratibu wa wizara hiyo kujua iwapo Dk Mahera atakwenda kusimamia uchaguzi huo.

“Utaratibu mzima aliopewa Rais kikatiba haujakaa vizuri kwa sababu katika uchaguzi unaohusisha vyama vingi, sasa mmoja kati ya washiriki wa uchaguzi yeye anateua refa, ni kosa kubwa kwa sababu huwezi kuwa na mshiriki ambaye ana refa wake,” alisema Dk Lihuri, akirejea uteuzi wa mkurugenzi wa uchaguzi.

Mtazamo huo uliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga aliyesema mabadiliko hayo hayaleti taswira yeyote kama sheria zipo vilevile.

“Sijajua wakati Rais anawapangia hizo kazi alikuwa anawazaje, tusitegemee kitu kipya mambo yatakuwa yaleyale kwa sababu ni watu walewale katika nafasi zilezile isipokuwa wanazungushwa tu,” alisema Henga.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF)-Bara, Magdalena Sakaya alisema mabadiliko hayo yanaweza kusaidia kwenye uchaguzi ujao kama Kailima (Ramadhani-Mkurugenzi wa Uchaguzi) ataendelea kuiishi misingi aliyokuwa nayo kipindi akishika nafasi hiyo.

“Akiwa kwenye nafasi hiyo wakati wa kampeni alikuwa anazunguka kwenye majimbo mbalimbali na wagombea tulikuwa tunakwenda kuongea naye na alikuwa anaonekana kuijua kazi yake na alitaka kuona haki inatawala,” alisema.