Naibu Waziri ashangaa mbunge wa Chadema alishindaje

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mpendae, Toufiq Salim Turky (CCM) ambaye amehoji kuna mkakati gani wa kutoa elimu kuhusu Ugonjwa wa Saratani nchini Jumatatu April 24,2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Muundo wa jimbo la Nkasi Kaskazini, umemfanya Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel kumpongeza kwa ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Dodoma. Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amemshangaa Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani ameshindaje katika uchaguzi mkuu kutokana na muundo wa jimbo hilo.

 Dk Mollel ametamka hayo leo Juni 5, 2023 wakati akijibu swali la nyongeza la Aida.

Aida amehoji baada ya Serikali kukiri kuwa kuna changamoto katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ina mkakati gani wa kumaliza changamoto hizo ili wananchi waondokane na kutoona haja ya kujiunga na mfuko huo.

“Kwanza nipongeze Mbunge kwa ulivyo karibu na nilipopita kule nilishangaa ulishindaje kule kwa ile ‘structure’ (muundo) nikajua kuwa wewe ni mwanamke wa shoka kwa ushindi uliooupata,”amesema Dk Mollel.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema wanashirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuona kuwa katika kipindi hicho cha mpito kuelekea bima ya afya kwa wote wanakaaje kuweza kuboresha eneo hilo.

“Kuna taasisi inayofanya eneo hilo tumeshawaita tuweze kukaa ili kuona fedha wanazotumia kwenye warsha wanawezaje kuboresha kitita wakati tunangojea muswada. Hata mimi mwenyewe sidhubutu kulipigania kwa sasa kwasababu halitoi matokeo tunayotaka,”amesema.

Amesema kwa ushirikiano wao na Tamisemi wataboresha eneo hilo muda si mrefu.