NCCR-Mageuzi wamuomba Rais Samia kumfukuza kazi Jaji Mutungi

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa NCCR Mageuzi, Samwel Ruhuza

Muktasari:

  • NCCR upande wa Mbatia wamuomba Rais Samia kumfuta kazi Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Mutungi kwa madai kwamba ameshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia ofisi hiyo kwa weledi hivyo sababu hiyo anapoteza sifa na uhalali wakubakia.

Dar es Salaam. Chama cha NCCR-Mageuzi, upande wa Mwenyekiti James Mbatia umemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kumfuta kazi Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi wakidai inashindwa kutekeleza majukumu yake kwa weledi ikiwamo kusuluhisha mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho.

Chama hicho kimegawanyika katika pande mbili wa Mbatia na ule unaomuunga mkono makamu Mwenyekiti Zanzibar, Ambar Khamis uliojitokeza kufuatia kikao kilichofanyika Mei 21, 2022 maeneo ya Kurasini na kutangaza kuwasimamishwa baadhi ya viongozi akiwamo Mbatia kwa makosa ya kugombanisha viongozi wenzao.

Upande huo umesema kitendo cha ofisi hiyo kushindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene Agosti 15, 2022 yaliyowataka kumaliza mgogoro unaowatafuna kwa zaidi ya miezi mitatu kwa kuzingatia katiba ya chama hicho ni wazi amekosa sifa ya kubakia katika nafasi hiyo.

Hata hivyo, Jaji Mutungi amekiri kupokea maagizo ya Waziri kwa barua huku akidai ukimya wake juu ya mgogoro huo si kwamba ameshindwa kusuluhisha, isipokuwa alikuwa anafanya maandalizi kisha awatumie wito wa kuwaita kwenye kikao cha pamoja kuzungumzia suala hilo.

“Nashangaa kwenye mkutano wao badala wanitake niharakishe kuwaita wao wanaanza kunishambulia lakini wanapaswa kutambua ofisi yangu inafanya shughuli zake kwa kuzingatia utaratibu si kama wanavyofikiri wao,” amesema Jaji Mutungi

Akizungumza  leo Jumapili Agosti 28, 2022 katika mkutano wao na vyombo vya  habari, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa NCCR Mageuzi, Samwel Ruhuza amesema wanawasiwasi na uwezo wa Jaji Mtungi na kushindwa kuisimamia ofisi hiyo vyema kunaondoa uhalali wa kuendelea kubakia.

“Rais anavyombo vingi vinavyoweza kumsaidia uchunguzi, anapaswa kumuondoa Jaji Mutungi ameshindwa kutekeleza wajibu wake na badala yake anachochea migogoro ambayo ni hatari kwa taifa na inaenda tofauti na falsafa ya Rais ya kujenga umoja na mshikamano kwa Watanzania,”amesema

“Jaji ameshindwa kutimiza majukumu yake unajua pamoja na nafasi yake tunamchukulia kama Jaji lakini kwakile kinachoendelea tunapata mashaka,”amedai Ruhuza ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu

Ruhuza amesema Jaji huyo hasikilizi maamuzi yanayotolewa na upande huo licha ya kwamba maamuzi yanayopelekwa kwake yanakuwa yamepitishwa na wajumbe asilimia 70 lakini anawajibika upande wa Katibu mkuu ambao maamuzi yanayotolewa hayakubaliki kwa msingi wa Katiba.

“Chama chetu kina wajumbe 81 kati ya hao sisi tuna wajumbe 47 na waobakia hawana nguvu ya kufanya maamuzi na yakakubalika lakini kinachoshangaza Ofisi ya Msajili imekuwa ikiyatilia mkazo na yanayotolewa na wajumbe wengi yanapuuzwa,”amesema