NCCR- Mageuzi yaitumia ujumbe NBS kuhusu Sensa

Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini

Muktasari:

Tanzania itafanya Sensa ya Watu na Makazi nchi nzima Agosti 23, 2022 huku NCCR- Mageuzi kikiitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kutoa dodoso za mfaano kwa wananchi ili zoezi hilo liweze kufanikiwa.

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku 11 kabla ya kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi, Chama Cha NCCR-Mageuzi kimeitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kutoa dodoso za mfano kwa wananchi ili shughuli hiyo iweze kufanikiwa.

 Agosti 23, 2022, Serikali imepanga kuanza kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi nchi nzima.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Agosti 11, 2022 Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini amesema ili wananchi waweze kujibu kwa ufasaha maswali watakayoulizwa zingetolewa dodoso zenye maswali hayo.

"Sisi NCCR Mageuzi tuko tayari kuhesabiwa na viongozi wetu mikoani wanahamasisha wananchama kujitokeza kuhesabiwa, lakini nivizuri Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ingegawa dodoso zenye maswali hayo,"amesema Selasini.

Amesema ili Serikali iweze kuwa na idadi kamili ya watu na kujua aina ya huduma wanazopaswa kupewa, ni vyema shughuli ya uhamasishaji ifanyike samamba na kugawa dodoso hizo kama inavyofanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu.

“Wakati wa uchaguzi zimekuwa zikitolewa karatasi za mfano na kuelekeza, watu namna ya kupiga kura na kwenye Sensa tungeshauri ifanyike hivyo ili wananchi waweze kutoa taarifa sahihi,”amesema.

Akijibu hoja ya NCCR-Mageuzi, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa amesema makarani watakapomaliza mafunzo yao Agosti 15, 2022 watakuwa na jukumu la kuzunguka kaya kwa kaya kwaajili ya kuwaelimisha namna ya kutoa hizo taarifa.

Amesema miongoni mwa taarifa hizo ni majina kamili, umri, jinsia uraia, elimu na shughuli wanazofanya, hali ya ugavi kwa kina mama, na mambo mengine kama hayo.

 “Hiyo iko kwenye ratiba ya Sensa, watapatiwa vipeperushi kwa kwa sasa wenyeviti wa mitaa na watendaji wa kata, wameshaanza na makarani watakapomaliza mafunzo watashirikiana hilo lifanyike,” amesema Dk Chuwa.