Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndani ya Habari: Simulizi mtoto aliyepigwa na walimu kwa madai kuiba keki

Raulence Nicholous Mwanafunzi anayedaiwa kupigwa na mwalimu hadi kujeruhiwa kwa tuhuma za wizi wa maandazi manne

Mbeya. Mwanafunzi anayedaiwa kupigwa na mwalimu hadi kujeruhiwa kwa tuhuma za wizi wa maandazi manne, aeleza alivyokimbia viboko na kukatwa na vioo vya dirisha.

Tukio hilo linamuhusu mwanafunzi wa kidato cha nne, Raulence Nicholous anayesoma Shule ya Sekondari Ruhila.

Mwanafunzi huyo alida kuwa alishawishika kuchukua maandazi hayo kutokana na kuhisi njaa.

Alisema kabla ya udokozi huo, aliomba chakula kwa mwalimu anayetuhumiwa kumshambulia, lakini walimu wenzake walikataa hivyo aliendelea kusoma akiwa na njaa.

“Wakati nimezima taa na kufunga madirisha na mlango wa darasa njaa ilikuwa inazidi kuniuma, akili ikaniambia angalia dukani hapo nikakuta dirisha lake liko wazi nikachukua keki nne” alisema Nicholous.

Baba mzazi wa Nicholous na baadhi ya wanafunzi wenzake wameeleza mwanafunzi huo hana tabia ya udokozi, huku yeye mwenyewe akisema majeraha aliyoyapa yametokana na kukatwa na vioo vya dirisha wakati akitoroka viboko vya mwalimu.

Tukio hilo lilitokea Februari 12 shuleni hapo muda wa saa tano usiku na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidaiwa mwanafunzi amejeruhiwa kwa kuiba maandazi matano yenye thamani ya Sh1,500 katika duka la shule hiyo na kupigwa hadi kulazwa hospitali teule ya Mbalizi Mbeya.

Watuhumiwa wa tukio hilo ni mwalimu Peter Emmanuel na mlinzi wa shule, Haruna Issa ambao wanaendelea na mahojiano na polisi kwa ajili ya uchunguzi.


Njaa ilivyomponza

Nicholous aliliambia gazeti hili kuwa ni kweli aliiba keki nne na wala haikuwa maandazi kama ilivyodaiwa na hilo ilitokana na njaa aliyokuwa nayo, kwani siku hiyo hakupata chakula cha jioni.

Alisema Jumapili kabla ya tukio, mwanafunzi aliyekuwa zamu ya kupeleka chungu kwa ajili ya kupewa chakula hakuwasilisha chombo chake kwa sababu kilikuwa kichafu.

“Utaratibu wa shule tunakula mara tatu kwa siku, saa 4 asubuhi, saa 8 mchana na saa 12 jioni na huwa tunakula kwa makundi chombo kimoja wanafunzi watano.

“Siku hiyo sisi hatukupata chakula cha jioni, japokuwa baadaye nilienda kwa mwalimu Emmanuel (aliyeshikiliwa na polisi) kunifundisha baadhi ya maswali ya hesabu nikaona pembeni kuna chakula nikamuomba akaniruhusu, lakini walimu wengine wawili wakanikataza.

“Usiku tukaenda kujisomea na wanafunzi wengine ila nilikuwa wa mwisho kutoka darasani wakati nimezima taa na kufunga madirisha na mlango njaa ilikuwa imezidi kuniuma, akili ikaniambia angalia dukani hapo nikakuta dirisha liko wazi nikachukua keki nne.

“Kumbe mlinzi wa shule, Issa aliniona na na akaniuliza na nikakiri na kuomba msamaha ambapo alionyesha dalili za kunisamehe,”alisema.

Nicholous alisema alipokuja mlinzi mwenzake wote jamii ya kimasai walianza kupiga simu kwa msimamizi ambaye alifika eneo hilo na mwanafunzi mwingine na kuelezwa alichokifanya.

“Msimamizi akapiga simu kwa mwalimu Emmanuel aliyeniruhusu awali kuchukua chakula na wale walimu wakagoma, alipofika alikuwa na fimbo akaanza kunipiga ovyo sehemu mbalimbali za mwili.

“Wakati anaendelea kunipiga, msimamizi akaonyesha kumpa hamasa ili aendelee kunipiga hadi wakafunga mlango na madirisha, mlinzi mmoja akasimama mlangoni mwingine akanishika huku yule mwalimu ananipiga,” alisema Nicholous.

Alisema baadaye alibahatika kupata upenyo akapanda madawati na kupiga mguu dirisha la kioo na kutoka nje na kuanguka hadi kukatwa na kioo hicho maeneo mbalimbali ya mwili na kupelekwa hospitali.

Hata hivyo Mkuu wa shule hiyo, Aginiwe Mahenge hakutaka kuelezea chochote, akisema bado wanafuatilia tukio hilo akifafanua kuwa zipo taarifa nyingine si sahihi, hivyo wakiziweka sawa ataelezea umma.


Baba mzazi

Nicholous Mwangake ambaye ni baba mzazi wa mwanafunzi huyo, alisema alipokea kwa masikitiko taarifa za mwanaye kuadhibiwa kiasi hicho, kwani hana tabia mbaya kiasi cha kudhibiwa namna hii.

“Mwanangu hajawahi kuwa na tabia za namna hiyo kwa sababu hata darasani walimu wenyewe wanasema alivyo safi, imenishangaza ila nashukuru ameruhusiwa hospitali,” alisema Mwangake.

Kwa upande wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali teule Mbalizi, Dk Khamis Bakari alisema mwanafunzi huyo mbali ya kuwa na majeraha ya kukatwa na vioo, walimkagua mwili mzima na kumfanyia vipimo, hawakuona jeraha lolote lililohusishwa na viboko.

“Kwa siku ya kwanza Februali 12 alishughulikuwa majeraha kwa sababu mfupa ulikuwa unaonekana ila siku ya pili tulimkagua hakuna ilipoonekana dalili za viboko,” alisema Dk Bakari.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Ernest Hinju alisema baada ya tukio hilo wanaendelea kutoa elimu ya kuwajenga wanafunzi kinidhamu na kuwambusha walimu sheria za kazi.

Hinju alisema kuwa pamoja na kwamba adhabu zipo kisheria shuleni, ila lazima iangaliwe kosa na adhabu yake na kwamba hakuna anayefurahia mwenendo huo kwa walimu na wanafunzi.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani humo kupitia kwa Kamanda wake, Benjamin Kuzaga ilieleza mwalimu Emmanuel na mlinzi Issa wanashikiliwa kwa uchunguzi kwa tuhuma za kumshambulia mwanafunzi huyo.

“Jeshi la Polisi kupitia wasiri wake, lilipata taarifa na kufuatilia na kubaini tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote na upelelezi wa shauri hili unaendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.