Nida: Msitafute vitambulisho kwa matukio

Baadhi ya wananchi wakiwa katika foleni ya kufuatilia vitambulisho vya Taifa ofisi ya Nida Ilala, Iliyopo Gongo la Mboto, Dar es Salaam. Picha na Nasra Abdallah
Muktasari:
- Kumekuwepo na ongezeko la watu katika ofisi za Nida, kutokana na kutangazwa kwa ajira katika sekta mbalimbali za Serikali na wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na JKT.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imesema wananchi wanapaswa kuacha kufuatilia kupata vitambulisho hivyo kwa matukio na badala yake kuhakikisha wanakuwa navyo mapema.
Wito huo umetolewa na Ofisa Habari wa Mamlaka hiyo, Geofrey Tengeneza, alipozungumza na Mwananchi Digital, iliyokuwa inafuatilia ongezeko la watu wanaofika kupata huduma katika ofisi mbalimbali za mamlaka hiyo jijini humo.
Tengeneza alikiri kuwepo kwa ongezeko la watu hivi karibuni na kueleza limechangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo kutangazwa kwa nafasi mbalimbali za kazi zikiwemo zile za Jeshi la Polisi zilizotolewa hivi karibuni.
Sababu nyingine amesema ni kumaliza kwa wanafunzi wa kidato cha sita ambapo baadhi yao wanatakiwa kwenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na wale wa kidato cha nne ambao wengine wanaenda kujiunga na vyuo vya kati.
“Hivyo ukiangalia vyote hivi ni kama mtu alikuwa anasubiri kutokee jambo fulani ndio aende kufuatilia kitambulisho hicho wakati sheria inamruhusu mtu yeyote aliyetimiza miaka 18 kuwa na kitambulisho hiki,” amesema Tengeneza.
Ili kupunguza usumbufu aliwataka wananchi kutumia njia ya mtandao kuomba vitambulisho hivyo ambapo inakamilisha asilimia 75 ya maombi huku asilimia 25 zilizobaki ndizo atakwenda kumalizia katika ofisi zao.
Ofisa Msajili wa Nida Wilaya ya Temeke, Zulfa Mnyika amekiri kuwepo ongezeko hilo na kueleza kuwa wao wamefanikiwa kupunguza tatizo la msongamano kwa kuwapa vijana hao kipaumbele.
“Baada ya vijana wengi kufurika hapa siku chache zilizopita tulijitahidi na maofisa wangu kuwahudumia kwa haraka, na tulikuwa tukifanya kazi hadi Jumamosi ili kuhakikisha hatuweki msongamano hapa,” anasema Zulfa.
Hata hivyo amesema kutokana na wananchi kuwa wazito wanakwenda kufuatilia vitambulisho hata pale wanapokuwa wametimiza vigezo, ofisi yake inatarajia kwenda kutoa huduma hiyo kwa makundi mbalimbali wakiwemo bodaboda, mama lishe kwenye maeneo ambayo wanafanyia shughuli zao.
Amesema tayari hilo wameanza kulifanya kwa kwenda kwenye vyuo vikuu na vile vya kati licha ya kuwa mwitikio haukuwa mkubwa, lakini aliahidi kuendelea kufanya kazi hiyo.
Naye Ofisa Msajili Nida wa Ilala, John Itimba, amesema mashine walizonazo zina uwezo wa kuwahudumia watu 250 kwa siku, lakini wanaofika kupata huduma kwa siku ofisini kwake hapo ni zaidi ya 600 kwa sasa ukilinganisha na 200 waliokuwa wakifika awali.
Itimba naye anaunga mkono watu kufanya usaili kupitia mtandao kwa kueleza kuwa endapo wengi watafanya hivyo, watakuwa wanaweza kuhudumia hata watu 500 kwa siku, kwa kuwa kazi zinazokuwa zimebaki ni kupiga picha, kuweka alama za vidole na uhamiaji kujiridhisha taarifa za muombaji alizojaza.
Walichosema wananchi
Wananchi waliozungumzia suala hilo, akiwemo Ruben Geofrey, amesema siyo kila mtu anaweza kuingia mtandaoni kujaza lakini pia ni gharama kwenda kufanyiwa kazi hiyo kwenye ‘stationary’ ndiyo maana watu wanaamua kwenda wenyewe Nida.
“Ukienda kujaziwa hizi, itakutoka sio chini ya Sh5,000, kwa kuwa pale unatumia MB za watu kuingia mtandaoni, hivyo kwa wasio na uwezo huo wanaona bora waje Nida ambapo fomu hizo zinapatikana bure,” amesema Geofrey.
Nuruel Mbaga mkazi wa Gongo la Mboto, amesema kuna haja ya wanaokuwa wamejaza kwa njia ya mtandao wanapofika katika ofisi hizo wawekwe foleni tofauti na ambao wamejazia hapo.
“Haiwezekani mimi niliyebakiza asilimia 25 kumaliza na tayari wana taarifa zangu zote tuhudumiwe sawa na anayeanza kujazia fomu hapa. Mfano mimi tangu saa moja nipo hapa na waliojaza fomu kawaida mpaka sasa hivi saa nane sijahudumiwa, hii siyo sawa,” amesema Nuruel.
Jenifer Joseph mkazi wa Tabata amesema kinachoonekana kuna uhaba wa wafanyakazi katika ofisi hizo na kuomba serikali iangalie namna ya kuwaongezea watu ili waweze kufanya kazi hiyo kwa wepesi.
Jenifer aliyekwenda kufuata kitambulisho hicho baada ya kuhitajika kujiunga na JKT, amesema watu wakiingia wanapopata huduma, inaweza kuchukua saa mbili ndiyo waitwe wengine waliopo kwenye foleni na hivyo kujikuta wanapoteza muda mwingi.
Sakina Maua anasema huduma siyo nzuri kwa wanaoanza kujaza fomu za kuomba kitambulisho na kueleza kuwa yeye ameenda kufuatilia namba ya kitambulisho kama tayari au la, lakini imemchukua saa zaidi ya tatu.
Sakina ametaka kuwepo na uwazi kwa kuwaeleza siku husika wataweza kuwahudumia idadi kadhaa ya watu, kuliko kuwaweka watu siku nzima halafu mwisho wa siku huduma pia hawapati.
Caroline Urio amesema licha ya kuwepo changamoto katika ofisi hizo, ni vizuri watumishi pia wakawa wanatumia lugha nzuri katika kuwaelewesha wananchi wanaofika kupata huduma.
“Yaani kuna wakati hata ukitaka kuuliza tu jambo, unaonekana mbaya na saa zingine unajibiwa kama hutaki kusubiri nenda nyumbani, hii sio sawa, kwa kuwa bila sisi wasingekuwepo hapo, hivyo ni wajibu wao kutumia lugha nzuri wanapotuhudumia,” amesema.