Njombe DC yapitisha bajeti 30.6 bilioni

Muktasari:

  • Wakati Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ikipitisha Sh30.6 bilioni kama rasimu ya bajeti ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/24, madiwani wa halmashauri hiyo wametakiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi.

Njombe. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Njombe limepitisha Sh30.6 bilioni kama rasimu ya bajeti ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 31 na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Valentino Hongoli kwenye kikao cha bajeti cha halmashauri hiyo kilichofanyika wilayani Njombe.

Amesema madiwani wanatakiwa kusimamia vizuri miradi inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo na kutenga fedha asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na asilimia 30 ya miradi ya maendeleo.

"Ili tuweze kutekeleza vizuri bajeti ijayo tunahitaji kukamilisha miradi yote ambayo tumeipanga hasa kupitia mapato ya ndani," amesema Hongoli.

Amesema katika kutekeleza miradi ya kimkakati inatakiwa ushirikiano na usimamizi mkubwa wa makusanyo ya mapato na kupeleka fedha kwa wakati katika miradi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Njombe Sharifa Nabalang'anya amesema kupitia bajeti hiyo wanatarajia kutekeleza na kubuni miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuongeza mapato ya halmashauri.

Amesema kabla ya kupitishwa kwa bajeti hiyo asilimia 70 ya mapato ya ndani yalikuwa yanategemea eneo moja pekee la misitu lakini sasa wanakwenda kuondokana na hali hiyo.

Amesema kutokana na mafunzo waliyoyapata baada ya kutembelea halmashauri za Chalinze na Dodoma yameleta matokeo makubwa na yameanza kuonekana.

"Kwasababu ni nadra sana kwa madiwani kukubali kupeleka zaidi ya milioni 600 kwenye miradi ya uwekezaji kwa mwaka mmoja wa fedha" amesema Nabalang'anya.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo akiwemo Neema Mbanga amesema shule ya sekondari Lupembe inakabiliwa na changamoto ya bweni hivyo pamoja na jitihada za wananchi katika kuchangia ujenzi lakini wanahitaji nguvu kutoka serikalini.

"Bweni la sekondari Lupembe nguvu ya wananchi imetumika na maeneo yaliyobakia kama vyoo na rangi wananchi hawawezi,” amesema Mbanga.