Ofisa kilimo Moshi atupwa jela kwa kumjeruhi binti wa kazi

Ermina Clement Marandu (40), Ofisa kilimo wa Wilaya ya Moshi ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela, baada ya kukutwa na hatia ya kumjeruhi Msaidizi wake wa kazi za ndani (house girl) katika mahakama ya Wilaya ya Moshi.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Mahakama pia imemuamuru kumlipa fidia ya Sh500,000 mwathirika wa tukio hilo.
Moshi. Ofisa Kilimo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Ermina Marandu (40), amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kutiwa hatia kwa kumjeruhi msaidizi wake wa kazi za ndani mwenye miaka 16.
Mahakama ya Wilaya Moshi, mbali na kifungo imemuamuru mshitakiwa kumlipa fidia ya Sh500,000 mwathirika wa tukio hilo (jina linahifadhiwa), ambaye ni mwenyeji wa Nyakanazi mkoani Kagera.
Mshitakiwa, mkazi wa Kilototoni, kata ya Njiapanda, Mji mdogo wa Himo alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Machi 13, 2024 mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Ruth Mkisi akikabiliwa na kosa la kumpiga na mti wa fagio na mateke na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake msaidizi huyo wa kazi za ndani.
Akitoa hukumu Septemba 20, 2024 hakimu Mkisi alisema baada ya mahakama kujiridhisha pasi na shaka na ushahidi uliotolewa mahakamani, mshitakiwa alitiwa hatiani kwa kutenda kosa hilo na kuhukumiwa.
"Mshitakiwa ametiwa hatiani na kuhukumiwa kutumia kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kumlipa fidia ya Sh500,000 mwathirika," amesema hakimu alipoulizwa na Mwananchi kuhusu hukumu hiyo.
Mshtakiwa alidaiwa kwa nyakati tofauti kati ya Januari na Februari, 2024 alimjeruhi msaidizi wake wa kazi za ndani kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia fimbo, fagio na kumpiga mateke hivyo kumsababishia majeraha makali.
Katika kesi ya jinai namba 6654 ya mwaka 2024, upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa Serikali, Imelda Mushi uliwasilisha mahakamani mashihidi saba. Upande wa utetezi mshitakiwa alijitetea peke yake.
Machi 5, 2024 kabla mshtakiwa hajafikishwa mahakamani Mwananchi lilifika nyumbani anakofanya kazi binti huyo ambaye alidai alikuwa akiteswa kutokana na vipigo huku mwili wake ukiwa na majeraha.
Alisema baada ya kumaliza darasa la saba mwaka 2022, katika Shule ya Msingi Kasato iliyopo wilayani Biharamulo, mkoani Kagera alishindwa kuendelea na masomo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi katika familia hivyo akaamua kufanya kazi za ndani.
"Baba yangu na mama yangu wote ni wakulima na hawana uwezo, hivyo nilipomaliza darasa la saba na kufaulu nilishindwa kuendelea na masomo maana wazazi wangu hawana uwezo," alisema.