Ofisi ya mtendaji wa kijiji yachomwa moto

Ofisi ya mtendaji wa kijiji yachomwa moto

Muktasari:

  • Ofisi ya mtendaji wa kijiji cha Mwabagalu kata ya Nyabubinza wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu imechomwa moto alfajiri ya leo Oktoba 17, 2021 na watu wasiojulikana.

Maswa. Ofisi ya mtendaji wa kijiji cha Mwabagalu kata ya Nyabubinza wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu imechomwa moto alfajiri ya leo Oktoba 17, 2021 na watu wasiojulikana.

Ofisi hiyo ambayo ilikuwa ikitumiwa na mtendaji wa kijiji na sehemu nyingine ikitumika kama darasa la wanafunzi wa awali imeteketea pamoja na nyaraka zote za Serikali zilizokuwa zimehifadhiwa katika jengo hilo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ambaye pia ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama katika wilaya hiyo amesema sababu za kuchomwa ofisi hiyo bado haijajulikana lakini tukio hilo limetokea wakati ambao mtendaji wa kijiji alikuwa akipokea meseji za vitisho kwa njia ya simu.

Amesema wamemtia nguvuni mwanamme mmoja anayefahamika kwa jina la Damas Masaba ambaye amekuwa akituma ujumbe wa vitisho kwa njia ya simu pamoja na kuandika maneno yasiyofaa katika jengo la ofisi ya mtendaji.

Amesema sio mara ya kwanza kwa  bwana huyo kuwekwa chini ya ulinzi, awali alikamatwa kwa tuhuma za kumtishia mtendaji wa kijiji na baadaye aliachiwa huru lakini aliendelea na vitisho vyake.

"Jengo hilo ni mali ya Serikali hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuharibu kwa hasira zake kama kuna vitu haviendi sawa vishughulikiwe kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu za nchi."

Amewaonya wananchi wanaojichukulia sheria mkononi kwa kuharibu mali za Serikali na kusema haiwezi kuvumilia vitendo hivyo na hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.