Ombaomba mfupa mgumu, Mzee Makamba atoa neno

Watu wenye ulemavu, Grace Hamis (23) na Grace Jackson (21) wakazi wa Msamvu wakipelekwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Morogoro baada ya kukamatwa nyumba ya kulala wageni wakati wa operesheni maalumu ya kuwasaka wanaokusanya fedha mtaani kwa kuombaomba. Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na Sh1.5 milioni.
Dar/Moro. Wakati mamlaka jijini Dar es Salaam zikisisitiza kutokomeza ombaomba mitaani, tatizo hilo limeonekana kuwa mfupa mgumu ulioishinda Serikali kwani hujirudia kila baada ya muda.
Akizungumza na Mwananchi jana, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge alisema wamezifungia nyumba 11 za kulala wageni na kuwasafirisha watu wenye ulemavu waliokuwa wakitumikishwa kuomba mtaani ikiwa ni juhudi za kutokomeza tatizo hilo.
“Tumeanza kazi na tumezifungia hizo lodge 11. Utaratibu wa kuwaondoa ombaomba mjini umefanyika, tumewaondoa jana (juzi) na tumewalipa posho wanaowapeleka.
“Tumesema wanapowapeleka kule wawape sehemu ya mikopo ili waweze kuendesha maisha yao huko.”
Hata hivyo hakuwa tayari kutaja mikoa wanayotoka watu hao, akisema watapelekwa hadi Shinyanga.
“Kutoka pale watapelekwa mikoa mingine, kila mtu ametaja mkoa anakotoka, wote wanatoka Tanzania,” alisema.
Katika Mtaa wa Tandale Uzuri jana, gazeti hili lilikuta baadhi ya nyumba zilizokuwa zikiwahifadhi watu hao zikiwa zimefungwa.
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Ummy Nderiananga akiwa ameambatana na mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo walifanya operesheni maalum iliyofichua nyumba zinazohifadhi watu wenye ulemavu wanaotumika kuomba jijini Dar es Salaam.
Pamoja na hatua hizo zilizochukuliwa, bado ombaomba wameendelea kuwepo katika mitaa ya jiji hilo la kibiashara wakipita huku na kule kuomba chochote kutoka kwa wasamaria.
Francisca Richard, mwenye ulemavu wa macho anayeomba katika Barabara ya Bibi Titi jijini Dar es Salaam alisema amelazimika kufany ahivyo baada ya kuambiwa na wenzake kuwa wamefanikiwa kupitia shughuli hiyo hivyo akaona na yeye aje kujaribu bahati yake.
Kwa upande wake, Hamis Hamis anayefanya kazi hiyo jijini hapa alisema “watu kama sisi huwa tunanyayapaliwa ndio maana ni vigumu kufanya shughuli nyingine, naomba ili nipate hela kwa ajili ya kusomesha watoto wangu. Si kwamba tunapenda kuomba ni hali tu ya maisha na hatuwezi kufanya shughuli yoyote kwani tumezaliwa na ulemavu.
Mkoani Morogoro nako operesheni ya kuwakamata watu waliojiajiri kama ombaomba mitaani imefanywa na Jeshi la Polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu alisema walifanya misako ya kawaida na kuwaakamata watuhumiwa 23 wakiwamo watu wenye ulemavu wawili katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Mtaa wa Msamvu.
Mfupa mgumu
Miongoni mwa viongozi waliopambana na ombaomba siku za nyuma ni aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Mzee Makamba alisema operesheni ya kuwaondoa ombaomba ina mizizi mirefu kwani ilianza wakati wa ‘Operesheni Nguvukazi’ mwanzoni mwa miaka 1980 wakati John Mhavile akiwa mkuu wa mkoa huo.
“Yeye (Mhavile) hakushughulika na ombaomba tu bali aliwarudisha mikoani vijana ambao hawakuwa wakiishi Dar es Salaam, waliokuja kutafuta kazi.
“Alifanikiwa kuwarudisha. Lakini, kazi hiyo ilifanyika siku moja, kesho yake mji umejaa. Kwa mfano, vijana waliotoka Tanga walipakizwa kwenye basi linaloitwa Zafanana na jingine Hongera. Walipofika Tanga hawakurudi nyumbani, kesho yake wakapanda mabasi hayohayo kurudi Dar,” alisema Makamba.
Kuhusu operesheni aliyoisimamia alisema hawakuwafukuza vijana wasio na kazi bali waliwatafutia cha kufanya.
“Nakumbuka tulisaidiwa na Airtel na Vodacom wakatupatia mahema, wale vijana wakajiajiri kwenye kazi mbalimbali ikiwamo mama na baba lishe,” alisema.
Kuhusu ombaomba, Makamba alimtaja mtu aliyekuwa akijulikana kwa jina la Paul Mawezi maarufu kama Matonya.
“Hii ya ombaomba ya kina Mzee Matonya tulishughulika nayo lakini tulichofanya, tuliwaorodhesha wanapotoka. Baada ya kumaliza tuliwapeleka na kuwakabuidhi kwa mkuu wa mkoa,” alisema.
Akizungumzia utaratibu unaotumika sasa, Mzee Makamba amewapongeza viongozi na kuwapa ushauri.
“Ninaipongeza Serikali kwa hatua walizochukua ila ni lazima pawepo ushirikiano kati ya viongozi wa Dar es Salaam na wa mikoani.
“Kwamba wakishawatambua ombaomba, wafanye kama tulivyofanya sisi, kuwapeleka mikoani na kuwakabidhi wa kwa wakuu wa mikoa.
“Nakumbuka Matonya tulimkabidhi kwa mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Unakumbuka Matonya alisema simpendi Makamba ila naipenda CCM. Kwa hiyo wakuu wa mikoa nao wahakikishe wanawakabidhi kwa ndugu na jamaa zao au taasisi zinazolea yatima,” alisema Mzee Makamba.
Juhudi za kuwaondoa ombaomba jijini Dar es Salaam pia zilivaliwa njuga na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda aliyetangaza operesheni kuanzia Aprili 12 mwaka 2016.
Februari 2020, Manispaa ya Ilala ilipitisha sheria inayotoa adhabu kwa watu watakaokutwa wakiwapa fedha ombaomba ili kukomesha utaratibu huo.
Kwa mujibu wa sheria hiyo atakayekutwa akimpa hela ombaomba atatozwa faini ya Sh200,000 papohapo, akishindwa atapelekwa mahakamani na faini yake ni Sh300,000 au kifungo cha miezi 12 jela.
Mkurugenzi mtendaji wa Ilala, Jumanne Shauri alisema sheria hiyo imekuja baada ya kuona hatua za kuwakamata na kuwatoza faini ya Sh50,000 haijafanikiwa kwani walikuwa wakilipa.
Maoni
Ofisa ustawi wa jamii, Mathias Njimba alisema tatizo hilo linaendelea kutokana na kukosekana kwa mkakati wa kudumu ambao ni endelevu.
Alisema kuwakusanya ombaomba na kuwarudisha makwao bila kujua kiini kinachosababisha watoke huko kwenda kuomba mjini haitasaidia.
“Ni lazima ufanyike utafiti kubaini chanzon inawezekana ni imani, mtazamo au utamaduni hivi vyote vitabainika kwenye utafiti. Kwa nini watoke kule waje mjini, wanachokitaka wanakipata? Inakuwaje wanashawishiana,” alisema Njimba.
Naye mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema ili kuondokana na tatizo hilo nchi inapaswa kuwawekea mazingira mazuri kupitia kamati za wenye ulemavu kuanzia ngazi ya kata na wilaya ili watatue changamoto zinazowakabili kwenye maeneo waliyopo.
Olengurumwa alisema mabaraza ya wenye ulemavu yangewekwa vizuri ingeondoa kwa kiasi kikubwa tatizo hilo nchini kwani wangekuw ana mahali salama pa kujadiliana yanayowasibu na majibu ya uhakika.
Pia aligusia suala la takwimu, “lazima viongozi wajiulize kama tunzao takwimu za kutosha za watu wenye ulemavu. Hata tafiti za uhakika hatuna wengi hawajasajiliwa na hawajulikani wako wapi. La pili wahakikishe wanatumia mabaraza kuhakiki kundi hilo nchini.”