Polisi aliyejichimbia kaburi sasa anunua jeneza la Sh3 milioni

Muonekano wa kaburi alillojenga, Patrick Kimaro, ambalo ameagiza akifariki azikwe hapo. Picha na Flora Temba

Hai. Kuishi kwingi kuona mengi, ndivyo unavyoweza kusema juu ya tukio la askari mstaafu Patrick Kimaro, kujichimbia kaburi na kujinunulia jeneza la Sh3 milioni.

Tukio la aina hii ni nadra kufanywa na mwanadamu ambaye kwa hulka, imani na tamaduni huogopa kifo na hata anapozushiwa kifo huwa ni ugomvi mkubwa, lakini si kwa Kimaro, aliyejichimbia kaburi akiwa hai.

Kimaro, maarufu kwa jina la Sabasita, amejichimbia kaburi ikiwa ni sehemu ya kujiandalia maisha yake akiondoka hapa duniani, sasa yuko katika hatua za mwisho za kukamilisha jeneza lake na wosia.

Sabasita ambaye ametengeneza kaburi lake kwa gharama ya Sh7 milioni, sasa amechagua na kuweka oda ya jeneza litakalogharimu Sh3 milioni, ambalo tayari amelipia nusu ya fedha na kuandaa chumba maalumu kwa ajili ya kulihifadhi.

Sabasita anaishi kijiji cha Mbosho, kata ya Masama Kati, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Kwa wasiofahamu nyumbani kwake, ukiingia getini kushoto kwako unakutana na kaburi lake alilojenga mwaka mmoja na nusu uliopita, ambalo amelijengea vizuri na kuweka paa la kuzuia mvua, gril na taa pande zote nne na kulifanya livutie.

Lakini pia ukutani mwa uzio wa nyumba yake, mbali na kuweka na kuchora picha yake na kueleza wasifu wake tangu ameanza kazi hadi anastaafu, pia ameweka picha za marais wa awamu zote sita.

Chini ya picha hizo za kuvutia za viongozi hao wakuu wa nchi, ameweka maandishi yanayoelezea ni awamu ipi ameongoza, tarehe aliyozaliwa kiongozi huyo, kipindi alichoongoza, kauli mbiu yake kwa wakati huo, na kama amefariki ni lini.


Gharama za jeneza lake

Akizungumza na wanahabari waliofika nyumbani kwake kufuatilia maandalizi ya jeneza na wosia ambavyo aliahidi akimaliza kaburi, Sabasita anasema tayari amechagua jeneza lake ambalo atazikwa nalo siku Mungu akimchukua.

Sabasita, ambaye alikuwa mtumishi katika jeshi la polisi kwa miaka 36 hadi alipostaafu Februari mwaka huu, alizaliwa Februari 2,1963, na kuajiriwa na Jeshi la polisi 1987 na amefanya kazi kwa miaka 36, ambapo amepitia vyeo mbalimbali na mpaka anastaafu alikuwa Superintendent of Police (SP).

Anasema wataalamu wanakamilisha jeneza lake na muda ukifika atalipeleka nyumbani na kuliweka kwenye chumba maalumu.

“Kaburi ni nyumba na ndani yake linaingia jeneza na tayari nimechagua jeneza ninalolitaka, ambalo thamani yake ni Sh3 milioni, bidhaa yoyote inatofautiana bei kutokana na uzuri au uimara wa bidhaa yenyewe,” alisema Sabasita.

“Majeneza nayo ni vivyo hivyo na mimi nimechagua hilo kwa sababu ni zuri na juu halina mbao, ni kioo kuanzia kichwani mpaka miguuni na limewekwa marumaru nzuri, limetengenezwa kitaalamu na nimependezwa nalo,” anasema.

“Sikuona kama kuna umuhimu wa kulileta nyumbani mapema maana nilitaka familia nayo itambue baba ameenda kwenye hatua nyingine na izoee jeneza kama ilivyozoea kaburi na tayari nimewaeleza na wanafahamu,” alisema

“Nimeshachagua na liko kwenye hatua za mwisho. Wakati ukifika jeneza litakuja hapa nyumbani. Jeneza hilo litakuwa sehemu ambayo imeandaliwa kwani kuna chumba nimekiandaa kwa ajili ya kuliweka,” alisisitiza Sabasita.

Anaeleza kwa sasa kaburi si mjadala kwenye familia, bali imekuwa sehemu ya vitu alivyonavyo nyumbani kwake kama ilivyo redio, televisheni na vitu vingine.

Kwa nini ameandaa kaburi na jeneza? Anasema hiyo yeye anaamini kifo kipo na hilo alilielewa mapema kuwa hata iweje ni lazima atakufa, hivyo aandae bajeti mapema kama vile ambavyo watu huandaa bajeti za sherehe mbalimbali.


Kuhusu wosia

Sabasita anasema tayari amewasiliana na wakili wake yuko hatua za mwisho za kuukamilisha wosia, tofauti na watu wengine, yeye atawapa watoto wake waupitie na kujiridhisha kama uko sawa na kila mmoja atabaki na nakala.

“Wosia ni jambo muhimu na wosia wangu nitataka niuandae tofauti na ilivyozoeleka, nahitaji niukamilishe niwape watoto wangu wausome na waniambie ni kipi kimekosekana na ni yupi kwenye mgawo anaona amepunjwa au amepewa ambacho hakutaka, na baada ya wao kuupitia na kurekebishwa nitampa kila mtu nakala yake,” alisema Sabasita.

“Wosia ni siri ya mwandishi na anayepokea, sasa mimi nafikiri kama naweza kuandika wosia nikaupeleka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), kwa mwanasheria au kanisani, sasa kwa nini uwe siri kwa watoto na familia yangu mpaka nife, kwa nini nisikae nao mezani nikawapa wakauona na tukajadiliana na tukakubaliana kila mmoja ili kuondoa maneno ya ulimpendelea fulani na vurugu kwa familia baada ya kifo,” alihoji.


Ni muda wa kuwa karibu na Mungu

Akizungumzia maisha yake kwa sasa, Sabasita anasema pamoja na mapumziko ya kustaafu na maandalizi ya kaburi, jeneza na wosia, pia amejipanga kurekebisha mambo yake, kuwa karibu na Mungu, kubadilika kiroho na kufanya kila kinachowezekana kusogea zaidi karibu na Mungu kitabia, kimatendo na kutubu kwa pale alipofanya makosa.

“Hakuna jinsi, kifo kipo na anayepanga ratiba ni Mungu, akiamua kuvuna mavuno yake hakuna wa kumzuia na umri unavyozidi kusogea ndipo muda wa mavuno nao unakaribia, hivyo najiandaa vizuri na kwa sasa namcha sana Mungu, nampenda sana Mungu wangu, na namuomba akiamua kunichukua anichukue kwenye kifo chema,” anasema askari huyo mstaafu wa Jeshi la Polisi.


Mtoto, ndugu wazungumza

Akizungumzia uamuzi huo wa baba yake, mtoto mkubwa wa Sabasita, Doreen Kimaro, anasema wazo la baba yao kujenga kaburi liliwaogopesha mwanzoni baada ya kuanza kujenga walihofia kwenda nyumbani, lakini kwa sasa wameona ni jambo la kawaida, hivyo hata akileta jeneza lake watalizoea.

“Mwanzo aliposema atajenga kaburi, tuliogopa sana na hata alipoanza kujenga na tukatumiwa picha tilipata shida na kuona labda baba anaweza kufa kesho na hata nyumbani tuliogopa kuja, lakini kwa sasa tumezoea hili na tunaweza kukaa hapo tukapika na kula bila shida,” anaeleza.

Doreen, ambaye ni dada yake msanii Tunda, anasema jambo hilo limewapa ujasiri na kwa sasa na yeye anaona upo umuhimu wa mtu kuandaa kaburi.

Naye Prosper Kimaro, ambaye ni ndugu wa familia hiyo, anasema Sabasita kufanya hivyo amepunguza mzigo kwa familia na migogoro ya maeneo ya kuzika ambayo hutokea baada ya kifo.

“Alichokifanya ni jambo lililopunguza mzigo kwa familia na kuleta ahueni kwenye familia, maana ikitokea akafariki, hakutakuwa na migogoro alisema azikwe wapi, ameshachagua mwenyewe pa kuzikwa na kujiandalia nyumba yake ya milele.

“Lakini pia hii imepunguza gharama, badala ya kuwaza kuandaa kaburi na jeneza, tutawaza mambo mengine,” amesema Kimaro.