Polisi aliyeshambulia mwanaye afikishwa mahakamani

Askari polisi Abati Benedicto Nkalango(aliyevaa shati nyeupe) anayetuhumiwa kumfanyia ukatili mtoto wake akiwa anarejeshwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana

Muktasari:

  • Askari Polisi mwenye namba H4178 PC Abati Nkalango (27) Januari 15, 2023 alimshambulia kwa fimbo na kumsababishia majeraha mtoto wake Benedicto Abati (7) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu.

Bariadi. Askari Polisi mwenye namba H4178 PC Abati Nkalango (27) aliyemshambulia mtoto wake Benedicto Abati (7) Januari 15, 2023 leo amefikishwa mahakamani.

Akitaja kesi hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi leo Februari 16, Mwendesha mashtaka wa Serikali, Daniel Masambu amesema mtuhumiwa anashtakiwa kwa kosa moja la kufanya ukatili dhidi ya mtoto ambaye alikuwa chini ya malezi yake.

Amesema mtuhumiwa ametenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 169(A) kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo 2022.

"Januari 15, 2023 mtuhumiwa alitenda ukatili kwa mtoto wake Benedicto Abati (7) kwa kumchapa sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia majeraha madogo na makubwa sehemu za mgongoni na masikioni," amesema Masambu.

Baada ya kusomewa shtaka mtuhumiwa alikana na wakakili wa Serikali aliieleza mahakama kuwa upelelezi juu ya shauri hilo umekamilika na kuomba kutajiwa tarehe ya kuanza kusoma hoja za awali.

Kesi hiyo itaendelea tena Machi 2, 2023 kwa hoja za awali ambapo Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi Mariam Nyangisi amemueleza mtuhumiwa kuwa dhamana ipo wazi.

Hata hivyo, mtuhumiwa alishindwa kutimiza sharti la dhamana la kuwa na wazamini wawili wenye vitambulisho pamoja na bondi ya Sh3 milioni na kurejeshwa mahabusu.