Polisi lawamani kwa kutesa watuhumiwa

Askari polisi wakimdhibiti mtuhumiwa katika moja ya matukio ya kutuliza ghasia. Polisi wanalaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kuwatesa watuhumiwa wanapokuwa mikononi mwao. Picha na maktaba

Muktasari:

Licha ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro kutoa kauli ya kutaka watuhumiwa kutendewa haki wawapo mikononi mwa polisi, malalamiko ya watuhumiwa kuteswa yameendelea kuwepo, huku waliodai kuteswa wakitoa ushuhuda wa waliyotendewa.

Dar es Salaam. Licha ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro kutoa kauli ya kutaka watuhumiwa kutendewa haki wawapo mikononi mwa polisi, malalamiko ya watuhumiwa kuteswa yameendelea kuwepo, huku waliodai kuteswa wakitoa ushuhuda wa waliyotendewa.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN-Women) na Mtandao wa Polisi Wanawake wa jeshi hilo, yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro Novemba 21, mwaka huu, IGP Sirro alisema watuhumiwa wanatakiwa kuheshimiwa na kutendewa haki kama watu wasio na hatia mpaka itakapobainika vinginevyo.

“Hakuna kitu muhimu kwetu kama kusimamia sheria na kutenda haki, kuwa wanyenyekevu na kuheshimu watu. Sisi leo tumevaa majoho haya na kesho tunarudisha kwa wenyewe na wenyewe ni Watanzania wanaolipa kodi inayotufanya tufanye kazi,” alisema Sirro.

Pamoja na kauli hiyo, matukio ya utesaji unaofanywa na polisi kwa watuhumiwa yameendelea kuripotiwa.

Tukio la hivi karibuni ni la Issa Kassimu (22) anayedaiwa kushambuliwa na askari wa kituo cha polisi Goba Novemba 10, 2021 baada ya kukamatwa kwa tuhuma za wizi wa runinga.

Issa alijeruhiwa na ndugu zake walipokwenda kufuatilia hali yake na utaratibu wa dhamana inadaiwa waliombwa rushwa ili aachiwe.

Inadaiwa kipigo hicho kilimsababishia majeraha yaliyomfanye alazwe katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema hizo ni tuhuma nzito na kwamba wameshafungua jalada la uchunguzi na mifumo ya kisheria itatumika ili kupata ukweli wa jambo hilo na ikibainika ni kweli hatua za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wahusika. Tayari uchunguzi huo umeanza.

Tukio jingine lilitokea Septemba mwaka huu, ambapo askari polisi jijini Dodoma walidaiwa kumfanyia vitendo vya ukatili dereva wa bodaboda kwa kumuingiza mti wa ufagio sehemu ya haja kubwa na kumsababishia majeraha.

Dereva huyo wa bodaboda ambaye pia ni mcheza muziki, Ally Bakari (21) mkazi wa Kata ya Mkonze alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, General kwa ajili ya matibabu.

Bakari alidai kufanyiwa ukatili huo kwa kupigwa, kunyofolewa nywele (rasta), kuteswa na kutobolewa utumbo kwa kuingizwa mti wa ufagio sehemu ya haja kubwa na watu aliodai ni polisi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga licha ya kuthibitisha kuwapo kwa tukio hilo, alisema bado haijajulikana kama waliofanya tukio hilo ni askari polisi, lakini wanaendelea kuchunguza.

Tukio jingine lilitokea Mei mwaka huu, mkoani Kilimanjaro ambapo polisi wilayani Mwanga walidaiwa kuwashushia kipigo wananchi wawili hadi kumvunja mmojawao mikono miwili, wakiwalazimisha kukiri kosa la wizi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Amon Kakwale alipoulizwa kuhusu tukio hilo lililotokea mwezi uliopita, alisema kuwa taarifa ya tukio hilo ipo na kwamba uchunguzi wake bado unaendelea.

Mateso hayo yanadaiwa kufanyika ghorofani katika kituo kikuu cha Polisi Wilaya ya Mwanga, lakini hata hivyo, uchunguzi wa ofisa mwandamizi wa Polisi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI) jijini Dar es Salaam ulibaini hawahusiki na tukio hilo.

Tukio jingine lilitokea Desemba 21, 2020 ambapo Stella Moses (30) inadaiwa alijinyonga akiwa katika Kituo cha Polisi cha Mburahati, Dar es Salaam.

Stella ambaye ni mama wa watoto wa wawili, anadaiwa kujinyonga Desemba 21, 2020 katika mahabusu ya polisi, huku ndugu wa marehemu wakitilia shaka taarifa hiyo ya polisi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi Wilaya ya Kinondoni, Ramadhan Kingai alisema tukio hilo lilitokea Desemba 21, 2020 lakini ndugu wa mwanamke huyo waliliambia Mwananchi kwamba, Stella alifariki Jumapili Desemba 20, 2020 siku ambayo alijisalimisha kituoni hapo baada ya kupata taarifa kwamba anatafutwa.

Walidai kuwa walipompelekea mtuhumiwa huyo chai Jumatatu saa 2 asubuhi, waliambiwa na polisi kuwa wamechelewa na hivyo wakatakiwa kurudi saa tano, walipokwenda tena muda walioahidiwa waliambiwa ndugu yao alijaribu kujinyonga na amepelekwa Muhimbili, hivyo wamfuate huko.

Alipoulizwa kuhusu matukio hayo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema matukio hayo yote yalishatolewa ufafanuzi na makamanda wa Polisi wa mikoa husika.

“Kwa sababu mimi nikitaka kuzungumza sasa hivi ni lazima nirudi kwenye kumbukumbu zetu, tukio gani lilizungumzwaje na hatua zilizochukuliwa. Naweza nikazungumza tu nikazua jambo kwa wananchi,” alisema Misime.


Ripoti ya LHRC

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2020 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), mwaka huo kulikuwa na matukio sita ya utesaji na kutendewa isivyo kati ya raia na vyombo vya dola.

Matukio hayo yaliripotiwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro, Dar es Salaam na Mara. Katika utafiti wa haki za binadamu, asilimia 8.8 ya washiriki walidai kwamba uwezekano wa kufanyiwa utesaji/kutendewa vibaya wakiwa chini ya ulinzi ni mkubwa kiasi, huku asilimia 33.5 wakisema ni mkubwa.


Wadau wafunguka

Mratibu wa mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alitaja mambo manne yanayoweza yakaondoa vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na askari, ikiwemo Serikali kuridhia mkataba wa kimataifa unaopinga ukatili wa aina zote kwa wananchi.

Alisema endapo Serikali itaridhia mkataba huo itapunguza kwa asilimia kubwa unyanyasaji na ukatili kwa raia wanapokuwa chini ya ulinzi.

“Lakini pia sheria hairuhusu polisi kutesa watu, bali wanatakiwa watumie nguvu ambayo ni ya kiungwana kama itatokea mtu ataleta fujo, hata hivyo kama mtuhumiwa hana fujo wanapaswa kumkamata kwa utaratibu.

“Pia inatakiwa tuwe na mabadiliko ya kisheria na katiba ambayo yatazingatia ulinzi wa watu wote ambao wanahukumiwa na kusimamia vizuri vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema Olengurumwa.

Vilevile, alisema inapaswa kuwe na mfumo au chombo huru ambacho kitaruhusu kamati huru kukagua matukio au malalamiko yanayofanywa na polisi.

“Tukiwa na vitu kama hivyo tutasaidia kupunguza kwa asilimia kubwa ukatili dhidi ya raia. Lakini hawa wanaofanya matukio haya wanapaswa kuchukuliwa hatua, hiyo itasaidia kupunguza kwa asilimia kubwa changamoto hiyo,” aliongeza.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema tafiti wanazozifanya zinaonesha matukio hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa ni Serikali kushindwa kuridhia mkataba wa kimataifa dhidi ya mateso kwa raia.

Pia alisema Katiba haijatoa mamlaka maalumu itakayofanya uchunguzi dhidi ya polisi na sio kujichunguza wenyewe.

“Inatakiwa mabadiliko ya sheria ya Katiba ambapo hili ni jambo la muda mrefu, jambo la muda mfupi ni tume ya utawala bora ifanye hiyo kazi, lakini pia iunde jopo maalumu ambalo halihusiani na polisi ambao hawatakuwa na mgongano wa kimaslahi kwasababu mengi yanachunguzwa lakini husikii yameishia wapi,” alisema Henga.