Polisi wazuia kikao cha Kamati Kuu ya NCCR- Mageuzi

Muktasari:

  • Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi limejipanga katika kila eneo linaloweza kuwa chanzo cha kuibua sintofahamu ya usalama.

Dar es Salaam. Kikao cha Kamati Kuu cha NCCR- Mageuzi kilichotarajiwa kufanyika leo Agosti 28, jijini Dar es Salaam kimeshindwa kufanyika baada ya Polisi kufika eneo kinapofanyika kukizuia.

Akizungumza kwa simu leo, Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kulikuwa na viashiria ya kuvunja amani.

Askari waliokuwa wamevaa sare za Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walivamia eneo la Msimbazi Centre ulipokuwa ufanyike mkutano huo, wakati baadhi ya viongozi wa NCCR Mageuzi walipokuwa wakiingia katika eneo hilo.

Polisi wazuia kikao cha Kamati Kuu ya NCCR- Mageuzi

Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi limejipanga katika kila eneo linaloweza kuwa chanzo cha kuibua sintofahamu ya usalama.

“Jukumu letu ni kuimarisha usalama, hatuwezi kusubiri mpaka hali hiyo itokee ndio tuanze kufuatilia,”amesema Kamanda Muliro alipokuwa akifafanua kuhusu zuio la kikao hicho leo Jumamosi kuanzia saa 3:00 katika Ukumbi wa Msimbazi Centre, uliopo wilayani  Ilala.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na uongozi wa chama hicho, kikao cha kawaida cha Kikatiba cha Kamati kuu kilitarajiwa kufanyika kujadili ajenda kuu ya ya maambukizi ya virusi vya korona(Uviko-19),  kubakwa kwa demokrasia na watawala pamoja na ufukara unaoendelea nchini.

Hata hivyo, baadhi ya askari leo wameonekana kutanda katika ukumbi huo wakizuia kufanyika kwa kikao hicho.

Alipoulizwa huenda agenda zinazojadiliwa na kikao hicho zimechagiza zuio hilo, Kamanda Muliro hakuwa tayari kutoa ufafanuzi akidai kuwa na muda mchache kutokana na kuwa kikaoni.