Polisi yakamata gari Mradi wa SGR likitafutiwa mteja Tabora

Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda akiwaonyesha waandishi wa habari gari lililokuwa limeibiwa katika mradi wa SGR kambi ya Malampaka wilayani Maswa mkoani hapo. Picha na Samirah Yusuph.
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limekamata gari aina ya HOWO tani 12 lenye thamani ya Sh180 milioni likiwa katika harakati za kutafutiwa mteja ili liuzwe mkoani Tabora.
Bariadi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limekamata gari aina ya HOWO tani 12 lenye thamani ya Sh180 milioni likiwa katika harakati za kutafutiwa mteja ili liuzwe mkoani Tabora.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda aliyoitoa kwa waandishi wa habari leo Februari 6, 2023, inaeleza kuwa gari hiyo mali ya Kampuni ya ujenzi ya CCECC ilikamatwa Mabama wilaya ya Urambo.
"Ilipotea Januari 27, 2023 katika Kambi ya Malampaka ikapatikana Januari 29, 2023 ikiwa inapelekwa kwa mnunuzi, katika hali ya kawaida gari haliwezi kutoka ndani ya fensi ikapotea maana yake kuna watu wa ndani wameshirikiana na walinzi kuhakikisha kwamba gari linatoka," amesema Chatanda.
Amesema katika operesheni iliyokuwa inafanyika katika mradi wa ujenzi wa reli ya ya SGR, jumla ya watuhumiwa saba walikamatwa wakiwa na vifaa mbalimbali vya ujenzi vilivyoibiwa katika mradi huo.
Amevitaja vitu vilivyokamatwa kuwa ni mafuta lita 560, pikipiki 8 zilizokuwa zinatumika kubebea mafuta, mifuko ya saruji 79, mirija ya kunyonyea mafuta 21, baiskeli 8, na mabomba ya chuma 19.
Vingine ni mapipa tupu mawili, madumu tupu 20, wavu 10 aina mbalimbali, nondo vipande 4 pamoja na vipande 5 vya red copper.
"Ninatoka wito kwa wakazi wa Simiyu kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi sambamba na kutoa taarifa sahihi za uhalifu na waharifu ikiwemo ikiwemo taarifa zitakazowezesha kupatikana Kwa watu hao na kujua mahala walipo," amesema Chatanda.